Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vikundi wanaoishi na virusi ni fursa ya kurefusha maisha

58110 Pic+ukimwi

Sun, 19 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ukimwi sio kifo. Unaweza kuishi miaka mingi ikiwa utaanza matumizi sahihi ya dawa za kufubaza virusi vya ugonjwa huo (ARVs).

Ni rahisi kupoteza maisha ikiwa utapuuzia matumizi sahihi ya dawa. Kati ya vikwazo vinavyowaumiza na kuwarudisha nyuma watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi ni unyanyapaa kutoka kwa ndugu na jamaa na wakati mwingine, wao wenyewe.

Baadhi walijinyanyapaa kwa kuona hakuna maisha mengine baada ya maambukizi hivyo kupoteza nguvu, uwezo wa kufanyakazi na kuandamwa na magonjwa nyemelezi.

“Nilinyong’onyea sana, sikuwa na matumaini na nilikata tamaa ya kuishi kabisa. Afya yangu iliyumba na uchumi wangu haukuwa mzuri,” anasema Gace Michael (45) mkazi wa Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam.

Grace na wenzake wanaoishi na VVU kutoka katika vikundi vya Dhahabu na Magereza vya manispaa ya Ilala walipata nafasi ya kutoa simulizi za maisha yao na namna walivyorejesha tabasamu baada ya kujiunga kwenye vikundi hivyo.

Wanachama hao walikuwa wakiwasimulia wenzao waliowatembelea kujifunza jinsi wamefanikiwa kuendesha vikundi hivyo kupitia Baraza la Watu wanaoishi na VVU nchini (Nacopha).

Pia Soma

Muuguzi msaidizi wa Hospitali ya Chanika jijini Dar es Salaam, Joyce Mwampyati anasema vikundi hivyo ni suluhu ya kupunguza mawazo kwa wagonjwa hao.

Anasema kikundi cha Dhahabu anachokisimamia kiliundwa na watu wanaoishi na VVU wanaopata huduma ikiwamo dawa, kutoka hospitali hiyo.

“Baada ya kupata majibu mtu mwingine anaweza kuchanganyikiwa na anakata tamaa ila akishawishiwa na akajiunga na wenzake wanambadilisha mtazamo, anaona kumbe yapo maisha zaidi ya Ukimwi,” anasema.

Mratibu wa Nacopha kanda ya Dar es Salaam, Edna Mwakalambile anasema utegemezi kwa watu wanaoishi na VVU ni hatari kwa sababu huongeza unyanyapaa.

“Ndio maana tulianzisha huu mfumo wa kuwakusanya pamoja, wakiwa huko watajadili unywaji wa dawa, lishe na mambo mengine muhmu kuhusu uchumi. Hapo upweke utaisha, nguvu zitarejea na watafanyakazi kwa bidii huku afya zikinawiri,” anasema Mwakalambile.

Simulizi

Betina Nimo anasema mwaka 2003 alipima na kugundulika ana maambukizi ya VVU. Kufahamu ukweli kuwa ameambukizwa anasema kulimkatisha tamaa na baada ya kujua hilo, hali yake ilikuwa mbaya zaidi.

“Nilikata tamaa nilinyanyapaliwa na wakasema sitapona nitakufa tu, hali ngumu lakini nilipojiunga na kikundi hiki nimebadilika,” anasema.

Anaeleza, alipojiunga na kikundi hicho alipewa mkopo wa Sh1 milioni ili ajiimarishe kiuchumi. Kutokana na fedha hizo, Nimo alinunua sungura, mbuzi na kuku alioanza kuwafuga akifuata masharti ya ufugaji bora.

“Wenzangu walinifariji wakanisimulia ya kwao nikaona kumbe yangu madogo basi nikashangaa furaha yangu imerejea. Nikaanza kuishi maisha kama kawaida,” anasema.

Anasema kwa sasa mtaji wake umekua na anao uwezo wa kumudu mahitaji yote muhimu ikiwamo kuwasomesha watoto wake na hakuna unyanyapaa anaokutana nao tena.

Kwa kuwa si tegemezi tena, anasema sasa si mtu wa kulialia hovyo kama ilivyokuwa zamani na anatumia dawa zake kama anavyoelekezwa na daktari. Anakula vizuri na anafanya kazi kwa bidii.

Mwenyekiti wa Kikundi cha Magereza, Tuli Mwambasi anasema mwaka 2011 alipopima hakuelezwa uweli kama anaishi na VVU japo aliambiwa anasumbuliwa na kifua kikuu.

“Nilishangaa TB inaendelea kunitesa na wala siponi, baadae nikarudi hospitali wakasema nimeambukizwa. Japo nilinyanyapaliwa, lakini sikujali niliamua kusimama niwaunganishe wenzangu,” anasema.

Anasema amefanikiwa kuwaunganisha wenzake na wamekuwa mfano wa kuigwa kwa kikundi chao kumiliki biashara yenye mtaji wa Sh45 milioni kutoka Sh3.5 milioni walizokopeshwa na Manispaa ya Ilala.

“Ukiwa na mtaji utaendesha biashara na utapata fedha hivyo utakuwa na uhakika wa kula vizuri hivyo dawa zitafanyakazi. Vikundi hivi ni dawa,” anasisitiza.

Dawa za ARVs

Mwenyekiti wa kikundi cha Dhahabu kilichopo Chanika, Lucy Nyambele anasema moja ya agenda kila wanapokutana ni matumizi sahihi ya dawa.

“Tusipokumbushana kunywa au kumeza dawa vikundi hivi havitakuwa na maana kwa hiyo kila tukikutana jambo la msingi ni kila moja kuzingatia hilo,” anasema.

Anasema imekuwa rahisi kuzingatia dawa hizo kwa sababu hawana msongo wa mawazo tena na wana uhakika wa kupata lishe inayokidhi mahitaji ya mwili.

“Tunakula matunda, mboga za majani, nyama, samaki na kila kinachotajwa kwenye lishe. Hatuna wasiwasi,” anasisitiza.

Kaimu mganga mkuu wa Hospitali ya Chanika, Mathias Njau anasema wanapokuwa pamoja wagonjwa hao wanaweza kuyafanya maisha kuwa mazuri zaidi kuliko wakitengwa au wakijitenga.

“Hili suala la (Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi) Waviu kuungana ni zuri mno ndio maana tukatoa nafasi wao kukutana na kujadili masuala yanayohusu afya zao,” anasema Dk Njau.

Chanzo: mwananchi.co.tz