Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vijana wasita kuchagia damu, wahofia kujua hali zao

Pic Damu Salama Vijana wasita kuchagia damu, wahofia kujua hali zao

Sat, 3 Jun 2023 Chanzo: Mwananchi

Licha ya kuwa vijana ndio kundi kubwa linalotegemewa katika kuchangia damu salama hapa nchini, kundi hilo linatajwa kuwa na hofu ya kuchangia damu kutokana kitendo hicho kuwawezesha kujua hali zao za afya.

Hayo yamebainishwa na Ofisa Uhamasishaji Damu Salama Kanda ya Kaskazini, Feisal Abubakar wakati akizungumza na waandishi wa habari, mkoani Kilimanjaro kuhusu kuanzishwa kwa kampeni ya siku 14 ya kuchangia damu ambayo imeanza Juni mosi hadi 14 mwaka huu kuelekea katika maadhimisho ya siku ya mchangia damu duniani. Kampeni hiyo ya siku 14 imelenga kukusanya chupa za damu 875 katika kituo cha Moshi Mjini, ambapo kila siku wamelenga kukusanya chupa 60 za damu ili kukabiliana na upungufu wa damu uliopo katika vituo vya kutolea huduma za afya Kanda ya Kaskazini.

Amesema uhitaji wa damu bado ni mkubwa katika vituo vya kutolea huduma za afya katika mikoa hiyo hivyo kupitia kampeni hiyo watapita katika maeneo mbalimbali kukusanya damu ikiwemo kwenye misikitini, makanisani na kwenye kambi za jeshi ili kukabiliana na uhaba wa damu salama katika vituo hivyo vya afya. "Uhitaji wa damu bado ni mkubwa sana kwasababu wagonjwa wanaongezeka, maradhi nayo yanaongezeka, kwa mfano hospitali zetu za jirani zinatoa matibabu ya wagonjwa wa saratani na uhitaji wa damu ni lazima uongezeke," amesama na kuongeza; "Uelewa wa watu kuhusu kuchangia damu uko chini sana, ukiangalia asilimia kubwa sana ya washiriki wa hizi kampeni za uchangiaji damu ni vijana lakini zipo imani potofu kuhusu kuchangia damu, watu ni waoga wanahofu kuwa kuchangia damu ni sehemu mojawapo ya kupima afya na hii ni kutokana na watu hawana utayari wa kujua afya zao, hii imekuwa ni changamoto kubwa kwetu.” Nao baadhi ya wananchi wa mkoa huo, wamesema changamoto iliyopo katika jamii ni kwamba baadhi ya watu hawana uelewa wa kutosha juu ya umuhimu wa kuchangia damu. Elly Samwel, ambaye ni mkazi wa Moshi amesema jamii inapaswa kuwa na uelewa na kutambua umuhimu wa kuchangia damu kwa wengine kwani uhitaji wa damu katika vituo vya kutolea huduma za afya ni muhimu. "Nimechangia damu mara nyingi sana na sijawahi kupata shida yoyote, hili la watu kuogopa kuchangia damu wakiogopa kujua hali zao za afya hofu hii inapaswa kuondoka kwenye jamii, niwaombe Watanzania wenzangu muendelee kujitoa kuchangia damu huu ni msaada mkubwa kwa ndugu zetu waliopo hospitalini na wanauhitaji mkubwa wa damu,"

Chanzo: Mwananchi