Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vijana wanaoishi na VVU waeleza jinsi wasivyoaminika waelezapo ukweli wa afya zao

20750 Pic+VVU TanzaniaWeb

Thu, 4 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Niligundua kuwa ninaishi na VVU katika harakati za kuchukua dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi. Utoto ulifanya nisijue kwa nini natumia dawa hizo, japo nilikata tamaa lakini nimeweza kujikubali,”

Ndivyo kijana Kelvin Wilson (23) alivyoanza kusimulia kuhusu afya yake baada ya kubaini kumbe aliambukizwa Virusi Vya Ukimwi (VVU) mara baada ya kuzaliwa.

Anasema wazazi wake walifariki akiwa mdogo na walezi wake hawakumweleza mapema wakihofia angeumia na kukata tamaa.

Yeye na wenzake wanaishi kwa furaha baada ya kuunganishwa kwenye Mtandao wa Vijana Wanaoishi na VVU (NYP+) unaofanya kazi chini ya Baraza la Watu Wanaoishi na VVU (Nacopha).

Kama ukibahatika kukutana na vijana hao utagundua kuwa furaha yao haifichiki na hawana wasiwasi wowote kuhusu maisha.

Mwenyekiti wa Mtandao huo, Pudensia George anasema Ukimwi si kifo ikiwa mtu atakubali afya yake na kutumia kwa usahihi dawa za kufubaza virusi.

“Unaweza kutimiza malengo yako kimaisha, kiuchumi na kifamilia. Unaweza kuoa au kuolewa na ukapata watoto wasio na maambukizi,” anasema na kuongeza;

“Binafsi niliona nijikubali au nisijikubali siwezi kubadilisha ukweli kwamba nilizaliwa nao. Huwa nawahamasisha wenzangu wasimame kwenye J nne; Jiamini, Jikubali, Jitambue na Jithamini,” anasema.

Anasema ikiwa mtu hatajikubali si rahisi kujithamini, kujiamini na kujitambua.

Mratibu wa NYP+ Nevala Kyando anasema kwamba kupitia mtandao huo wameweza kuwaunganisha vijana na sasa wapo tayari kujadili kwa uwazi kuhusu afya zao na kuwasaidia wengine walioshindwa kujikubali.

Pia, Pudensia anasema kwamba imekuwa rahisi kupambana na changamoto mbalimbali ikiwamo unyanyapaa, ubaguzi na matumizi yasiyo sahihi ya dawa kwa baadhi ya vijana.

Mtendaji Mkuu wa Nacopha, Deogratius Rutatwa anasema kwamba kupitia mradi wa Sauti Yetu, unaotekelezwa chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Watu wa Marekani (Usaid), wameweza kurejesha furaha kwa vijana wengi waliokuwa wamekata tamaa.

Anasema kila halmashauri kuna vijana wawili wanaoingia kwenye Baraza la Wilaya la Watu Wanaoishi na VVU (Konga).

“Vijana hawa huwa wanakutana na kujadili mambo yanayowahusu. Hii imesaidia kuleta mabadiliko kiafya na kiuchumi,” anasema.

Simulizi za vijana waishio na VVU

Katika simulizi yake Calvin Wilson (23) anasema kwa kuwa walezi wake hawakuweza kumweleza kuhusu afya yake, kadri alivyokuwa alianza kujiuliza kwa nini kila siku anatumia dawa.

Kijana huyo ambaye alikuwa akihudhuria kliniki yake katika Hospitali ya Palestina, Sinza jijini Dar es Salaam, aligundua ukweli akiwa na umri wa miaka 15.

“Baadaye niligundua mwenyewe kuwa zile ni dawa za kupunguza makali ya Ukimwi (ARV), kusema kweli niliumia na nilikata tamaa. Nikaanza kufanya vibaya kwenye masomo yangu darasani,” anasema.

Hata hivyo, anasema kwamba kadri alivyokuwa akihudhuria kliniki na kutambua kwa nini anahudhuria, alikutana na watu wengine walio na hali kama yake.

“Ilinichukua mwaka mzima kujikubali baada ya kuona kumbe siko peke yangu na maisha yanaweza kuendelea,” anasema.

Simulizi ya pili ni ya Isiaka kijana aliyejitambulisha kwa jina moja. Tofauti na Calvin, yeye alijua kuwa anaishi na VVU akiwa na miaka 14 baada ya kuugua na kwenda kupima.

“Nilipopima na kupewa majibu niliogopa sana, nilijiuliza nimepata wapi Ukimwi? lakini baadaye nilibaini kwamba nilikuwa nao tangu nazaliwa,” anasema.

Anasema alianza matumizi ya dawa lakini kwa sababu hakuwa na usimamizi mzuri kuna wakati alikuwa akisitisha.

“Kwa sababu ya kuacha dawa niliugua, daktari akaniambia nisiache kabisa. Hata hivyo, nilikuja kujikubali baada ya kukutana na vijana wenzangu,” anasema.

Jane Mashindi, mkazi wa Mwanza yeye anasema kwamba mama yake alimweleza mapema kuhusu afya yake tangu akiwa mtoto.

Anasema uwazi wa mama yake ulimsaidia kujitambua mapema.

“Ikawa rahisi kwangu kujiunga na wenzangu kwenye mapambano haya dhidi ya Ukimwi kwa sababu tayari najua nini maana yake na naweza kuishi vipi nisipate maambukizi mapya,” anasema.

Changamoto zao

Vijana hao wanasema vishawishi ndiyo changamoto kubwa wanayokutana nayo.

“Kuna wengine nikiwaambia naishi na VVU wanaelewa, wengine hawaamini hadi niwaonyeshe kadi yangu. Pia wapo ambao hata nikiwaonyesha kadi ni wabishi kukubali,” anasema Pudensiana.

Msichana huyo mrembo anasema hajawahi kuacha kuwaeleza vijana wa kiume ukweli kuhusu afya yake lengo kubwa likiwa kuwalinda.

“Ujue huwa ninawaeleza ukweli, wasipokuwa makini na kufanya ngono kwa kuangalia watu usoni wataambukizwa,” anasema.

Anasema amekuwa akitumia nafasi hiyo kutoa elimu kwa vijana wenzake kuhusu Ukimwi.

Kama ilivyo kwa Pudensia, Pili naye amekuwa akiwaeleza ukweli vijana wa kiume wanapotaka kuanzisha naye uhusiano wa kimapenzi. “Wengine wanakubali na wanaondoka hawarudii, wengine hawaamini hadi niwathibitishie, lakini wengine hata wakiamini hawakati tamaa,” anasema.

Kwa upande wake Calvin anasema imekuwa rahisi kwake kuwafundisha wasichana kuhusu Ukimwi hasa wale wanaotaka kuanzisha uhusiano naye.

“Hata mimi nasumbuliwa na wasichana, mara zote nawafundisha kuhusu Ukimwi huku nikiwaambia ukweli,” anasema.

Pili anasema jambo kubwa kwa vijana ni kufanya uamuzi sahihi wa maisha kwa kutofanya ngono zembe au kuwa na mpenzi mmoja wanaye aminiana.

Kuhusu uhusiano

Kwa kuwa Ukimwi si kifo wala mwisho wa maisha, vijana wanaoishi na VVU wana ndoto za kutengeneza familia zao kama ilivyo kwa wengine.

“Nitaolewa na nitapata watoto wangu, nitatimiza ndoto zangu bila wasiwasi wowote. Inawezekana kupata watoto wasio na VVU kwa sababu najua namna ya kujilinda binafsi, mwenza wangu na watoto watakaozaliwa,” anasema.

Vijana wote waliozungumza wanasema wapo kwenye uhusiano salama wa kimapenzi. “Mchumba wangu hana VVU, siku zote namlinda na wakati wa kuoana utakapofika tutafanya hivyo tukitegemea watoto wazuri walio salama, namlinda,” anasimulia.

Mchumba wa Jane, Nikolaus Gidion (Ssio jina halisi) mkazi wa Sengerema Mwanza, anasema kwa sababu anampenda Jane kuishi na VVU si kikwazo kwenye uhusiano wao.

“Kama tutaachana ni kwa sababu nyingine lakini si VVU. Tuna miaka miwili ya uhusiano na tunaishi kwa kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya ikiwamo kutumia condom pale tunapokutana. Aliniambia ukweli tangu siku ya kwanza, nampenda sana,” anasimulia.

Wakikutana wanajadili nini?

Mratibu wa mtandao huo wa vijana, Kyando anasema jambo kubwa ambalo huwa wanajadili ni kuhusu afya zao.

“Wanakumbushana kuhusu matumizi sahihi ya dawa, wapo ambao huacha kuzitumia jambo ambalo ni changamoto,” anasema.

Anasema mbali na mikutano, vijana wamekuwa wakisambaa kwenye vituo vya kutolea huduma kwa watu wanaoishi na VVU kuwasaidia wengine elimu kuhusu Ukimwi.

Kyando anasema kwenye vituo kuna vijana ambao baada ya majibu hudhani huo ndio mwisho wa dunia kwao jambo ambalo si sahihi. Anasema mtandao huo ulioanza kufanya kazi mwaka 2003, umeweza kuwafikia vijana wengi na mpaka sasa kuna wanachama zaidi ya 300.

Kyando anasema dira yao ni kuwa na taifa ambalo vijana wenye VVU wanaheshimiwa, kupata mahitaji ya msingi na haki za binadamu. “Tunachotaka ni kuona hakuna unyanyapaa wala ubaguzi, pia kuendelea kuwasaidia vijana wengine kupima na kutambua afya zao,” anasema.

Kuhusu mikakati yao

Pudensia anasema mkakati wao mkubwa ni kuwafikia vijana wote wanaoishi na VVU ili waungane pamoja katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

Mwenyekiti huyo anasema kwanza wanataka kuona maambukizi yanapungua.

“Vijana wanatakiwa kupima ili wajue afya zao, wakijijua wataweza kuingia kwenye tiba ikiwa watakutwa na maambukizi au kujitunza,” anasema.

Kauli ya Nacopha

Mtendaji Mkuu wa Nacopha, Rutatwa anasema ni ukweli usiopingika kwamba dawa za kulevya na ngono zembe ni vichocheo vikubwa vya maambukizi ya VVU kwa vijana hasa wa kike ambao wapo kwenye hatari kubwa zaidi.

Anasema kuna haja ya kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya Ukimwi kwa kila kada kutimiza wajibu wake.

“Mashirika ya kijamii, wadau wa maendeleo, vyombo vya habari, viongozi wa dini na hata wa kisiasa kila mtu aongelee Ukimwi, bado upo na unaambukiza,” anasema.

Mwenyekiti wa Nacopha, Justine Mwinuka anasema kwamba kwa sasa bado ni vijana wachache walioweza kujitokeza na kupima afya zao.

“Tuwawezeshe vijana wawe na uhakika wa kupata dawa kwa magonjwa nyemelezi, pia tuhamasishe matumizi ya ARV,” anasema.

Mkakati wa Serikali ni kufikia asilimia 90 tatu yaani 90-90-90 ambapo ya kwanza ni watu kupima na kujua hali zao, waliopima kuanza matumizi ya dawa na ya mwisho walio kwenye dawa kufubaza virusi.

Chanzo: mwananchi.co.tz