Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vijana 30 wafundishwa kuishi na kisukari

Dbf767fa458eeeca7e2e2b35b116b207 Vijana 30 wafundishwa kuishi na kisukari

Mon, 7 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

TAKRIBANI vijana 30 wanaoishi na ugonjwa wa kisukari wamepata mafunzo ya namna ya kuishi na ugonjwa huo na kujikinga wasipatwe na matatizo zaidi yanayoendana na kisukari.

Mafunzo hayo yametolewa kwa siku tatu na Chama cha Wagonjwa wa Kisukari, yakishirikisha vijana hao kutoka kliniki nane za kanda ya pwani zinazohudumia vijana hao, wakiwemo baadhi ya wazazi.

Akizungumza baada ya mafunzo hayo jana mjini Bagamoyo, Meneja Mipango wa Chama Wagonjwa wa Kisukari, Happy Nchimbi alisema lengo la kambi hiyo ni kuwapa elimu vijana hao kuhusu kisukari na kuwawezesha kujikubali kwa hali waliyonayo.

"Siku hizo tatu zilikutanisha vijana 32, wazazi saba, wataalamu waliobobea katika wa kisukari na chakula na michezo wanane, pamoja na watoa huduma. Lengo la kuwa na timu ya wataalamu hao ilikuwa kuwawezesha watoto wajue kwamba katika ugonjwa walio nao wanatakiwa kufanya kazi mbalimbali za kijamii, kusoma na kucheza kama watoto wengine wasio na kisukari, " alisema Happy.

Alisema watoto walipatiwa elimu ya darasani na nje ya darasa na walifanya shughuli zikiwemo za nyumbani, huku wakipimwa viwango vya sukari kabla na baada ya kazi.

Happy alisema, mpangilio huo wa mafunzo ya darasani na nje ya darasa, ulilenga kuwaelewesha kujua namna wanavyotakiwa kuishi, kuzijua na kudhibiti dalili zisizo rafiki wanapofanya kazi, hasa kuchoka na kupatiwa sindano ya 'Insulin' kuirudishia miili yao kiwango cha sukari kinachotakiwa.

"Mafunzo hayo yamesaidia kuondoa unyanyapaa kwa vijana hao kwani wamejua siyo peke yao wanaougua kisukari, lakini pia yamesaidia wazazi kujua namna bora ya kuishi na watoto wao wenye kisukari, pamoja na watoa huduma kujiimarisha kuwahudumia wagonjwa," alifafanua Happy.

Baadhi ya vijana walioshiriki mafunzo hayo ambao pia ni wanafunzi walisema hukosa amani wanapofikiria suala la kujichoma sindano za 'insulin; kuhofia kueleweka vibaya na wenzao, huku pia wakikumbana na changamoto ya kuzuiwa kufanya kazi kwa sababu ya tatizo hilo.

"Mafunzo haya yameniwezesha kuelewa namna bora ya kuishi na kisukari, najua njia nzuri ya kutumia dawa na kupima, jinsi ya kushiriki katika kazi na wenzagu nikiwa salama bila kuathirika kiafya, lakini pia namna ya kufanya mazoezi niweze kuwa na afya bora," alisema Emmanuel Mfinanga, mshiriki wa mafunzo hayo.

Chanzo: habarileo.co.tz