Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vigodoro, bodaboda zinavyochangia mimba za utotoni, ukatili wa kijinsia

20594 Pic+kigodoro TanzaniaWeb

Thu, 4 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kigodoro! Kama ulidhani ni kifaa cha kulalia, basi umekosea. Wilayani Kisarawe na maeneo mengine ya mkoa wa Pwani pamoja na jijini Dar es Salaam, kigodoro ni sherehe inayohusisha muziki unaokesha.

Utamaduni huu wa sherehe za usiku uliopewa jina ‘kigodoro’ umetajwa kuwa chanzo cha ongezeko la mimba za utotoni na ubakaji Kisarawe.

Takwimu za mwaka 2016/17 wilayani Kisarawe zinaonyesha kulikuwa na matukio ya ukatili wa kijinsia na mimba za utotoni 157 wakati takwimu za mwaka 2017/18 zikionyesha matukio ya ukatili wa kijinsia yalikuwa 74.

Akizungumza hivi karibuni katika warsha iliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), iliyotoa elimu na kubadilishana mawazo na wadau kuhusu matukio ya ukatili wa kijinsia, Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo anasema wilaya hiyo ina matukio ya ukatili wa watoto kwa kiasi kikubwa.

Warsha hiyo ilihusisha wadau wakiwemo maofisa maendeleo, wanasheria, maofisa upelelezi, watendaji wa vijiji, kata, vitongoji, taasisi zisizo za kiserikali na viongozi wa dini ambao walieleza hali halisi ya matukio ya ukatili wa kijinsia wilayani humo na kushauri namna ya kukabiliana nayo.

Karibu wadau wote waligusia mila ya kuwacheza ngoma mabinti (unyago) na vigodoro kuwa ni chanzo cha mimba na ubakaji.

“Kuna kesi nyingi katika wilaya hii zinazohusu ukatli wa kijinsia kwa watoto na mimba za utotoni,” anasema Jokate.

INAENDELEA UK 26

INATOKA UK 25

Anasema serikali ipo tayari kushirikiana na Tamwa katika harakati za kutokomeza masuala ya ubakaji na ulawiti.

“Hatuwezi kusema Kisarawe ipo salama, kwa sababu watoto wananyanyaswa, wanatukanwa, tunataka matukio haya yatokomee kabisa,” anasema.

Aidha, anasema mimba za utotoni kwa kiasi kikubwa zinachangiwa na mfumo wa watoto kulelewa na babu au bibi zao, wakati wazazi wakiwa mjini.

“Asilimia 70 ya watoto wilayani hapa wanalelewa na babu na bibi zao,” anasema.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Eda Sanga anasema wameungana na wadau hususani jamii ya watu wa Kisarawe ili kushirikiana nao katika kupeana taarifa kuhusu ukatili na unyanyasaji wa kijinsia.

Wadau hao ni pamoja na wazee, viongozi wa dini, vijiji, kata, serikali za mitaa, wanasheria na taasisi zisizo za kiserikali.

Anasema wameichagua wilaya ya Kisarawe kwa sababu ni miongoni mwa wilaya zilizochaguliwa tangu mwaka 2012 kwa lengo la kupunguza vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wanawake, watoto wa kike na kufanya kazi na wanakamati ili kuviibua na kuvitolea suluhisho.

Akizungumzia ukatili wa kijinsia, Eda anasema sababu kuu inayochangia kuongezeka kwa vitendo hivyo ni malezi duni.

“Ni mjumuiko wa mambo mengi, lakini kwa upande wa Tamwa, katika hii miaka tuliyofanyia kazi suala hili, tumeona kuna shida kwenye malezi. Watoto wanazagaa mitaani hawana usimamizi na uangalizi thabiti, hivyo kusababisha wakumbane na mambo ya ubakaji na ulawiti,” anasema.

Anasema wanawake kwa upande wao wananyanyasika kwa sababu ya hali duni ya uchumi.

“Inapotokea mwanamke anamtegemea mume wake kwa vitu vidogo kama nyanya na chumvi, tangu siku ya kwanza hadi ya mwisho, migogoro na malumbano hutokea kwa sababu ni mtu mmoja anayetegemewa katika kuleta kipato kwenye nyumba,” anasema.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Masaki wilayani humo, Janiu Mussa anasema vigodoro ni chanzo cha watoto hasa wa kike kubakwa na kupata mimba.

“Wanakwenda kwenye vigodoro na kucheza ngoma zao tena kwa mitindo ya ajabu,” anasema.

Wadau hao wanasema wakati kigodoro kikiendelea, mengi yanatendeka ikiwemo unywaji pombe, uvutaji bangi, lugha za matusi na uchezaji unaohamasisha vitendo vya ngono.

Anasema wanapokuwa kwenye vigodoro wanawake wanakuwa katika hatari ya kubakwa na wanaume walevi, wao wenyewe kunywa pombe, kulewa na kurubunika kiurahisi.

Mussa anashauri iwepo sheria ya kuzuia kijana mwenye umri wa chini ya miaka 18 kuhudhuria ngoma hizo.

“Ikiwezekana, ukimuona mtoto kwenye kigodoro, hata kama siyo wako unatakiwa kumfukuza,” anasema.

Pamoja na vigodoro, lakini madereva bodaboda nao wanatajwa kuwarubuni wanafunzi wa kike wanaotumia usafiri huo kwenda shule.

Ofisa Upelelezi wa Polisi Wilaya ya Kisarawe, Robert Elias, anasema madereva wa bodaboda wanachangia kuwarubuni wanafunzi.

“Shule zipo mbali, kutokana na jiografia ya mji wa Kisarawe na hakuna magari ya abiria, hivyo wanafunzi wanalazimika kupanda bodaboda, huko ndiko wanakorubuniwa,” anasema.

Kwa upande wake, Ali Komwa, Kiongozi wa Jumuiya ya Kiislamu Kisarawe, anasema wanataka waumini kujitokeza na kueleza kuhusu matukio ya unyanyasaji na sio ule wa kupigwa pekee bali hata kunyimwa chakula na kutukanwa.

Anasema ukatili kwa kiasi kikubwa wilayani humo ni kwa watoto, ingawa pia wanawake nao hufanyiwa matukio yasiyofaa, udhalilishaji mbele ya jamii.

“Wanawake wanapigwa na waume au wenzi wao, siyo hivyo tu bali wengine hunyimwa hata chakula na kutukanwa, huo pia ni unyanyasaji,” anasema.

Anasema taasisi hiyo huketi pamoja na viongozi wa dini zingine na kujadili changamoto za kimaadili zinazotokea katika jamii na kuzitafutia ufumbuzi.

“Tunachotaka ni watu waseme, sio waziwazi tu lakini hata kwa siri waeleze yanayowasibu ili yafanyiwe kazi,” anasema.

Mkuu wa Upelelezi Elias, anasema matukio ya ubakaji na ulawiti ni mengi. Kwa mfano, waliobakwa na kulawitiwa wilayani humo kwa mwaka 2016/17 ni 157.

“Watoto wa jinsia zote wanabakwa. Tunapokea baadhi ya kesi mtoto wa kike amebakwa na kulawitiwa. Vivyo hivyo kwa watoto wa kiume nao wanalawitiwa,” anasema.

Anasema matukio hayo yanachagizwa zaidi na mila na desturi kwa mfano ngoma na unyago, vigodoro na mazingira ya malezi duni kwa watoto.

“Kwa mfano mtoto analelewa na mama pekee, baba hajulikani aliko wala haeleweki,” anasema.

Anasema pia kuna changamoto katika kusimamia kesi kama hizo, ambapo inapofikia hatua ya kutoa ushahidi mahakamani baadhi ya wazazi wanashindwa kujitokeza.

“Mzazi akishaona mtoto amepewa mimba, anakwenda kuripoti polisi lakini kinapokuja kipindi cha kesi hajitokezi. Mbaya zaidi wapo wanaofikia kusema binti yake na kijana walikutana siku moja tu, hivyo hawamfahamu,” anasema.

Ameitaka Tamwa kuelimisha zaidi kuhusu mzigo wa familia unaotokana na mimba za utotoni na madhara yake kwa jamii.

Akizungumza Agosti 25, mwaka huu wakati akigawa madawati kwa Shule ya Msingi, Mwanzage, Tanga, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema anakerwa na tabia ya watoto wa kike kukesha kwenye vigogoro kwa kuwa inamjengea mazingira hatarishi.

Chanzo: mwananchi.co.tz