Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vifo vya wazazi vilivyozua majanga kwa watoto

25017 Yatima+pic TanzaniaWeb

Fri, 2 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Pamoja na magumu yote aliyoyapitia bado anaamini siku moja atakuwa mfanyabishara mkubwa zaidi ya Dk Reginald Mengi au Said Salim Bakhresa.

Hii ni ndoto ya Kelly Sadock (33) mama wa watoto watatu mkazi wa Kunduchi jijini Dar es Salaam, anayefanya biashara ya kuuza maji, soda na juisi barabarani.

Kelly ni yatima aliyepitia magumu mengi yanayoumiza moyo wake kila akiyakumbuka, lakini maisha yake bado ni fundisho thabiti kwa wote waliokata tamaa au wale ambao wanapita katika kipindi kigumu.

Reginald Mengi ambaye leo ni mfanyabiashara mkubwa Tanzania na miongoni mwa mabilionea wa Afrika ambaye Kelly anatamani kuwa zaidi yake, ameandika kitabu alichokipa jina la “I Can, I Must I Will”.

Kitabu hiki kinaeleza historia ya maisha ya nguli huyu wa biashara, namna alivyotoka katika familia maskini huku akisema kwamba nia na uthubutu ni moja ya ajenda iliyomfikisha alipo sasa.

“Naimani nitafika na nitakuwa zaidi ya Mengi na Bakhresa,” anasema Kelly.

Kelly ametoka wapi?

Haikuwa rahisi kusimulia magumu aliyowahi kupitia pale mwandishi wa makala hii alipomwomba kufanya hivyo. Alilia na kushindwa kuzungumza ipasavyo.

Kelly na wadogo zake wanne, Ramadhan, Mariam, Bakari na Herman walizaliwa katika Kijiji cha Kalege mkoani Kigoma, kutoka familia ya Magala Mpambile.

Furaha ya familia hiyo ilisambaratishwa na kifo cha wazazi wao waliofariki miaka 25 iliyopita.

“Alianza kufa baba ambaye ndiye alikuwa tegemeo letu sote, baada ya miezi mitatu akafariki dunia mama na kutuacha yatima…” anasema Kelly huku machozi yakimlenga machoni mwake.

“Tuliishi katika mazingira magumu kijiji kwetu Kalege, kula kwetu kulikuwa kwa kubahatisha na wakati mwingine tulilala na kushinda na njaa,” anasema.

Kelly anasema kwamba hakuna ndugu aliyewajali wala kuwasaidia zaidi ya mjomba wao Simon Ibrahimu ambaye kwa sasa naye ni marehemu.

“Baada ya mama kufariki mjomba alituchukua akawa anatulea. Ni kama tulikuwa na bahati mbaya maana baada ya mwaka mmoja mjomba naye alikufa,” anasema.

Anameza mate na kuvuta kamasi zilizokuwa zikichuruzika kwenye pua zake kwa sababu ya kulia na kusema; “Baada ya mjomba kufa hakukuwa na ndugu mwingine wa kutusaidia, tuliishi maisha yasiyo na uangalizi wala usalama”.

“Mimi ndiyo nilikuwa mkubwa, niligeuka kuwa mama na baba wa wadogo zangu, tuliona bila kujishughulisha hatutaweza kula wala kwenda shule.

“Tulianza kulima vibarua katika mashamba ya watu ili tupate fedha za kununua chakula, nguo na kwenda shule, kumbuka sote tulikuwa bado wadogo,” anasema Kelly.

Kelly na wadogo zake ni mfano tu, lakini kwa mujibu wa takwimu zilizochapishwa na Mwananchi Data mwaka 2016 kwa hisani ya Takwimu za msingi za mwaka 2016 zinaonyesha Tanzania ina jumla ya watoto yatima 731,536 sawa na wastani wa asilimia 8.5 ambao hawapati huduma muhimu ikiwamo elimu na malezi bora.

“Tulijitahidi kufanya vibarua ila kuna wakati tulidhulumiwa na kulipwa fedha kidogo licha ya kufanya kazi kubwa, kadri tulivyozidi kukua ndivyo maisha yalivyozidi kuwa magumu,” anasema.

Anasema wakati akiwa mdogo alipenda kuwa mpelelezi mashuhuri endapo anagebahatika kusoma, lakini ndoto hiyo haikuweza kutimia. Nilipenda sana na hata sasa napenda kuwa mpelelezi mashuhuri, pengine wazazi wangu wangekuwepo huenda leo ningekuwa naitwa mpelelezi,” anasema.

Mdogo wake abakwa

“Siku ambayo inaniumiza na sitakaa niisahau ni siku ambayo mdogo wangu wa kike alibakwa wakati akitoka kufanya biashara stesheni kuuza maharage usiku,” anasema huku akigugumia neno stesheni kwa uchungu.

“Ni siku ambayo huwa inanikumbusha swali la kwa nini wazazi wangu walikufa tena kwa kufuatana,” alilia na kufunika uso wake kwa khanga aliyokuwa amejitanda mabegani mwake wakati wote alipokuwa akizungumza.

Kelly anasema mdogo wake ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka 13, alibakwa lakini kwa sasa tayari ameolewa.

“Alikuwa bado mdogo na alikuwa amemaliza darasa la saba akisubiria matokeo, hivyo alikuwa akifanya biashara ili apate fedha ya kumsaidia kwenda shule endapo angefaulu,” anasema.

“Mdogo wangu alikuwa anapenda kusoma kama dada yake na alikuwa na uwezo mkubwa darasani, baada ya kubakwa alipata mimba hivyo hakuwa na namna nyingine alilazimika kuolewa,” anasema Kelly.

Kelly anasema siku chache baadaye matokeo ya darasa la saba yalitoka na mdogo wake alikuwa amefaulu lakini hakuweza kwenda shule kwa sababu mbili; kwanza alikuwa mjamzito, pili hakuwa na fedha za kwenda shule.

Wadogo zake wakimbilia Dar, wafanya kazi ya kupiga debe

“Baada ya mdogo wangu kuolewa, nilibaki na wadogo zangu wa kiume watatu. Tukaendeleza gurudumu la maisha kijijini. Tuliendelea kufanya vibarua na biashara ndogondogo.

“Siku moja tukiwa tunakula jioni, wadogo zangu waliniaga na kuniambia wanakwenda mjini Dar es Salaam kutafuta maisha kwani wamechoshwa na maisha ya kijijini.

“Sikuwa na namna ya kuwazuia zaidi niliwauliza wakienda huko wataenda kuishi wapi, watakula wapi na watalala wapi? Jibu walilonijibu ni kwamba hiyo ni siri yao,” anasema.

“Alitangulia Ramadhani na alipofika alikuwa akilala stesheni kwa kipindi cha mwezi mmoja, baada ya hapo wadogo zangu wawili walimfuata kaka yao,” anasema Kelly.

Kelly anasema alibaki peke yake kijini, hivyo akaamua kutafuta mwanaume. “Niliolewa na Sadock Elia nikiwa na miaka 15 baada ya kuona nimebaki peke yangu na maisha kuzidi kuwa magumu,” anasema.

Anasema akiwa ndani ya ndoa na Elia alibahatika kuzaa naye watoto watatu lakini kwa bahati mbaya mwanaume huyo alimkimbia na kumwacha na watoto hao kijijini.

Anasema mume wake alikuwa akidaiwa fedha, hivyo alikimbia deni na kutokomea kusikojulikana bila hata kumuaga. “Hivi ninavyozungumza sijui mume wangu yuko wapi, ni mzima au amekufa,” anasema. Shida ikabaki pale pale, nilikosa mwelekeo, nikiwaangalia wanangu moyo uliniuma na kujiuliza nitawalisha nini?,” anasema.

“…Nikaona nife na wanangu nikawatafuta wadogo zangu nikawaeleza yaliyonikuta na hali yangu ya sasa,” anasema. Anasema anachoshukuru Mungu yeye na ndugu zake wanapendana na kuthaminiana, inapotokea mwenzao amepata shida husaidiana haraka iwezekanavyo.

“Wadogo zangu wa kiume wakaniambia dada badala ya kuendelea kuteseka kijijini njoo Dar. Si kwamba wadogo zangu walikuwa na maisha mazuri. Hapana,” anasema.

Anasema wadogo zake walikuwa wakifanya kazi ya kupiga debe na kuchunga mifugo kwa mtu na walipanga chumba kimoja tu. Nilikwenda mjini kwa wadogo zangu nikiwa na watoto wangu, niliishi nao katika chumba hicho kimoja,” anasema.

Wadogo zangu walinipa fedha ya mtaji Sh5,000 nikaanza kuuza maji ya kandoro kwa kutembeza barabarani, fedha niliyoipata ndiyo niliyonunua mahitaji ya watoto wangu na kuwasomesha,” anasema.

Anasema pamoja na yote bado fedha aliyopata haikufua dafu mbele ya wingi wa shida zake, hivyo ilifika wakati akashindwa hata kuwalipia karo watoto wake kwani kipindi hicho elimu ya msingi ilikuwa ni ya kuchangia.

Akutana na wazungu

“Siku moja nilikuwa nimekaa barabarani nikisubiri wateja. Kama Mungu, walipita wazungu fulani ambao waliguswa na maisha ya watoto wangu na kuamua kuwasaidia kwenda shule,” anasema.

“Siku hiyo nilikuwa na wanangu, kwa sababu ya kukosa karo walikuwa hawaendi shule hivyo nilikuwa nazunguka nao mtaani kuuza maji,” anasema.

Anasema wazungu hao walipowaona watoto wake waliguswa na kuwasogelea kwa sababu walikuwa wamedhoofu kutokana na lishe duni wakawauliza walipo wazazi.

“Wazungu walikuja na kuniuliza kwa nini watoto hawaendi shule? Niliwaeleza hali halisi wakaguswa na kusema wanashirika lao jina nimelisahau kidogo wanasomesha watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu,” anasema.

“Nilikubali wakaniahidi watakuja nyumbani. Baada ya siku chache, walikuja na kuguswa zaidi na mazingira tunayoishi hivyo waliamua kujitolea kuwasomesha wanangu katika shule moja iliyopo Tegeta (jina tunalo).

Kelly anaeleza pamoja na kupata msaada wa kusomeshewa watoto wake hakubweteka kwani wazungu walijitolea kuwasomesha tu majukumu mengine bado walimuomba afanye mwenyewe. “Niliendelea na kazi yangu ya kuuza maji huku nikimshukuru Mungu kwa kuwaleta wazungu hao,” anasema.

Anasema siku chache baadaye akiwa barabarani akiuza maji alipita mratibu wa kutambua kaya maskini kata ya Kunduchi anayeshughulika na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), Bahati Masebu.

Kelly anasema mratibu huyo alimuandikisha kwenye mpango huo na mara ya kwanza akapewa Sh46,000. “Nilibaki nikishangaa maana kushika fedha hiyo kwa wakati mmoja lilikuwa jambo geni kwangu nilikuwa nikisikia tu nilichofanya nilichukua hiyo fedha na kununua unga wa mahindi kilo 25 na maharage kilo 10 nikaweka ndani,” anasema.

Anasema alifanya hivyo kwa sababu hawakuwa na chakula, awamu ya pili ya mpango huo alipokea Sh46,000 tena, ambazo alikwenda kununua deli la kuhifadhia vinywaji baridi na kuongezea mtaji wake kwa kununua maji ya chupa, soda na juisi. “Niliongeza thamani ya biashara yangu ya maji, badala ya kuuza kandoro pekee nilianza kuuza maji ya chupa, juisi na soda, kwa sasa najipanga nikipata tena fedha niongeze mtaji wangu,“ anasema.

Anasema lengo lake ni kumiliki mgahawa mkubwa wa kiwango cha kimataifa ambao utakuwa ukitoa huduma za chakula cha aina mabalimbali na vinywaji.

Chanzo: mwananchi.co.tz