Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vifo vya mapema magonjwa yasiyoambukiza vyabainika

Fri, 21 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Imeelezwa vifo vya kati ya miaka 30-39 vitokanavyo na magonjwa yasiyo ya kuambukiza vinazidi kuongezeka ambapo tafiti zinaonyesha ni watu milioni 15 kati ya watu milioni 41 wanaofariki kila mwaka.

Magonjwa haya yametajwa kukua zaidi ambapo hivi sasa kati ya vifo milioni 41, asilimia 71 ya vifo vyote hutokana na magonjwa yasiyoambukiza.

Mratibu Programu ya Usalama Barabarani kutoka Shirika la Afya Duniani, Merry Kessi amesema robo tatu ya vifo hivyo sawa na watu milioni 32, wanatokea katika nchi zenye uchumi wa chini ya kati.

Kessi ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Desemba 21, 2018 walio katika mradi wa usalama barabarani unaosimamiwa na Wizara ya Mambo ya Ndani, Kikosi cha Usalama Barabarani, Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO).

“Watu milioni 41 wanafariki kila mwaka duniani na vifo milioni 15 vitokanavyo na magonjwa yasiyoambukiza vinatokea mapema. WHO imebaini watu wenye umri wa miaka 30 na 69 kati yao asilimia 85 wanakufa vifo vya mapema kutoka nchi zenye uchumi wa chini na kati,” amesema Kessi.

Amesema vifo hivyo vinachangiwa na magonjwa ya moyo kwa kiwango kikubwa cha watu milioni 17.9, saratani milioni 9.0, mfumo wa upumuaji milioni 3.9 na kisukari watu milioni 1.6.

“Makundi haya manne ya magonjwa yanashambuliwa na kusababisha vifo vya mapema kwa zaidi ya asilimia 80 ya wanaougua,” amesema.

Naye Ofisa Mawasiliano kutoka kitengo cha Elimu ya Afya kwa Umma, Said Makora amesema wizara ina mkakati wa kupambana na magonjwa haya lakini bado kuna maeneo yanahitajika maboresho zaidi.

“Tumbaku ni tatizo. Bado kuna changamoto hasa majumbani asilimia kubwa ya wanaoathirika na matumizi hayo ni wanawake na watoto ambao wanapokea moshi huo kutoka kwa wavutaji na wao ndiyo waathirika wakubwa,” amesema Makora.

Nchini Tanzania magonjwa yasiyoambukiza yanashambulia mijini watu 108 kati ya 100,000 ikilinganishwa na vijijini ambako watu 95 kati ya 100,000 kwa mujibu wa tafiti za mwaka 2010.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz