Idadi ya watu wanaofariki kutokana na magonjwa ya Ukimwi, kifua kikuu na malaria kwa kipindi imepungua cha miaka mitatu kutokana na maboresho yalifanyika katika sekta ya afya nchini.
Takwimu zilizotolewa na Serikali zinaonyesha kuwa maambukizi ya Ukimwi mwaka 2021 yaliua watu 25,000 na mwaka 2023 idadi hiyo ilipungua hadi vifo 22,000.
Kwa upande wa malaria ambayo mwaka 2021 iliua watu 1,882, kwa mwaka 2023 iliua watu 1,540 wakati kifua kikuu kikiua watu 18,100 mwaka 2023 ikilinganishwa na vifo 26,800 mwaka 2021.
Takwimu hizo zilitolewa jana Dar es Salaam na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu wakati akieleza namna Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa miaka mitatu 2021-2023 ilivyofanikiwa kupunguza vifo vitokanavyo na magonjwa hayo pamoja na maboresho yaliyofanyika kwenye sekta hiyo.
Ummy alisema magonjwa hayo yameendelea kudhibitiwa nchini na watu wenye maambukizi ya Ukimwi wameendelea kupata dawa za kufubaza makali ya ugonjwa huo.
“Kwa upande wa malaria tumeendelea kutoa huduma za kupima pamoja na upatikanaji wa dawa za ugonjwa huo,” alisema.
“Tutaendelea kutumia mikakati mbalimbali ya kudhibiti malaria kwa sababu kutokana na mabadiliko ya tabianchi na mafuriko, dawa zinatengeneza usugu mwilini,” aliongeza.
Katika hatua nyingine, Waziri Ummy alitahadharisha jamii juu ya ongezeko la magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambapo tathmini inaonyesha kufikia 2030 nchi za Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara zitakuwa zimekumbwa na magonjwa hayo kwa asilimia 70.
“Tukiendelea na mwenendo huu tutafika pabaya. Mfano ugonjwa sugu wa figo takwimu zinaonyesha asilimia tatu hadi 13 ya Watanzania wana tatizo hilo, ugonjwa huu kwa asilimia kubwa unatokana na shinikizo la juu la damu pamoja na kisukari,” alisema
Alisema watu wanaosafisha damu ni 5,000 hadi 5,500 kati yao 2,700 wanatumia kadi za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na watu 800 wanajilipia fedha taslimu.
“Takwimu zetu zinaonyesha tuna watu 2,000 wanaotaka kusafisha damu wakiwa na tatizo sugu la figo hawamudu gharama, hii ni changamoto, tunajitahidi, ndio maana kwenye Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote tumeweka mfuko wa kugharamia wasio na uwezo na magonjwa sugu,” alisema.
Ummy alisema kama watu hawatabadilika hata fedha zinazotengwa hazitatosheleza.
Alisema Serikali itaendelea kutoa elimu kwa watu kuzingatia lishe bora na kuachana na tabia bwete yaani kutofanya mazoezi, ili kuepuka magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Alisema mgogoro uliopo baina ya NHIF na watoa huduma za afya binafsi unachangiwa na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambayo yanaugharimu mfuko huo fedha nyingi.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Upasuaji Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), Dk Anthony Assey alisema ajali ni kundi la magonjwa yasiyo ya kuambukiza zinayosababisha idadi kubwa ya watu ndani ya taasisi hiyo.
“Watu wengi wanaofikishwa kwetu matatizo yao yanatokana na ajali za bodaboda, kuanguka kwenye majengo marefu na kubeba mizigo kwenye masoko, hivyo ni muhimu watu wachukue tahadhari,” alisisitiza.
Wakati huohuo, Waziri Ummy alitaja mikakati ya wizara hiyo kwa mwaka mmoja na nusu uliobaki kwa kipindi cha Samia, kuwa ni kuimarisha mfumo wa rufaa na Tehama.
“Tunataka hospitali za rufaa za mikoa kutumia Tehama na kutoa huduma bora, salama na zenye ufanisi,” alisisitiza.
Kuhusu eneo la miundombinu, Waziri huyo alisema ndani ya miaka mitatu ya Rais Samia kumefanyika uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya kutolea huduma za afya ambapo vituo vya kutolea huduma vimeongezeka kutoka 8,549 mwaka 2021 hadi kufikia 9,610 Machi 2024.
Mafanikio mengine aliyoyataja chini ya miaka mitatu ya Rais Samia ni huduma za kipimo cha CT Scan kupatikana kwenye hospitali 27 kati ya 28 za mikoa nchini.