Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vidonda tumbo: Tabia zake, jinsi zinavyoingia na namna zinavyoondolewa

Healing Frequency Stomach Ulcer Vidonda tumbo: Tabia zake, jinsi zinavyoingia na namna zinavyoondolewa

Thu, 9 Jul 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

• Sigara, pombe, viungo… tafakari!

VIDONDA vya tumbo vina namna yake vinavyotokea kwenye ukuta wa ndani wa utumbo, wa chakula au sehemu ya mwanzo ya utumbo mwembamba ujulikanao kama ‘duodenum.’

Zipo aina kuu mbili za vidonda vya tumbo; vinavyotokea ndani ya mfuko wa tumbo, yaani ‘gastric ulcers’, pili hutokea kwenye sehemu ya mwanzoni ya utumbo mwembamba inaitwa ‘duodenal ulcers’.

CHANZO CHAKE

Katika utumbo, huwa unamwagwa tindikali kwa ajili ya kusaidia mmeng’enyo wa chakula. Kwa kawaida, tindikali huwa ni kali na isipodhibitiwa tumboni, inaweza kuleta madhara.

Mfuko wa tumbo wa binadamu una ukuta wa ndani, uliozungukwa na ute (mucus) unaosaidia kuzuia tindikali isiunguze au kuharibu sehemu hiyo.

Uzalishaji ute huo unapopungua, una kawaida ya kusababisha tindikali ama kuunguza/kuharibu sehemu ya ukuta wa tumbo, hivyo kusababisha vidonda vya tumbo.

Kupungua ute husababishwa na mambo. Kuna maambukizi ya bakteria ajulikanaye kwa jina la ‘helicobacter pylori’ (H. pylori), matumizi ya kipindi kirefu ya dawa za kundi la ‘Nsaids’ kama vile aspirini na ‘ibuprofen.'

Pia, mazingira ya kuwepo tindikali nyingi iliyopitiliza tumboni (hyperacidity) ni hali inayohusiana na urithi wa asili, msongo wa mawazo, uvutaji sigara na matumizi ya baadhi ya vyakula kama pilipili na viungo.

Lingine, linaelezwa kitaalamu ni kuwepo tabia zinazomuweka mtu katika hatari ya kupata vidonda vya tumbo, ikijumuisha uvutaji sigara, matumizi makubwa asteroids’ (kama dawa za kutibu asthma), historia ya familia kuwa na mgonjwa wa vidonda vya tumbo na matumizi ya pombe kupita kiasi.

DALILI ZAKE

Dalili za vidonda vya tumbo, hutegemea na hali ya vidonda vilivyo. Kuu inayowapata wengi ni kuhisi maumivu kama ya kuwaka moto eneo kati ya kifua na tumbo.

Kuna maumivu ambayo mara nyingi huwa makali zaidi, wakati tumbo likiwa halina chakula na inadumu kwa dakika chache au saa kadhaa.

Dalili nyingine, ni pamoja na kupungua uzito, kichefuchefu na kutapika, kushindwa kula kutokana na maumivu, kuhisi kuwa na gesi tumboni, kucheua au kupanda kwa tindikali kwenye koromeo, pamoja na kiungulia.

UGUNDUZI HOSPITALI

Kugundua vidonda na matibabu yake hospitali hutegemea dalili na hali ya vidonda vilivyo. Daktari huchunguza, kwa msada wa vipimo na anafanya mapitio ya historia ya mgonjwa na dalili au dawa alizowahi kutumia awali.

Ili kugundua uwepo wa bakteria H. Pylori’damu, kinyesi au kipimo cha mgonjwa hutumika.

Vipimo vingine vinavyoweza kutumika ni kinachoitwa ‘Barium X-ray’’ na ‘endos copy’. Hicho cha pili, mpira huingizwa tumboni mwa mgonjwa kupitia kinywa.

Kingine ‘endoscopic biopsy’ hufanyika kwa namna ya sehemu ndogo ya ukuta wa tumbo huchukuliwa na kufanyiwa vipimo.

MATIBABU

Matibabu ya maradhi hayo yanatofautiana, kulingana na chanzo halisi cha vidonda vilivyo. Sehemu kubwa, hufanyika kwa daktari kumuandikia dawa za kutumia na mara chache, upasuaji hufanyika.

Ni muhimu kuelewa kwamba, matibu ya vidonda vya tumbo hufanyika mara tu vinapogunduliwa na iwapo kuna vidonda vya tumbo vinavyotoka damu, mgonjwa mara nyingi analazwa, kwa ajili ya matibabu zaidi na hata kuongezewa damu inapobidi.

Iwapo sababu ya vidonda vya tumbo itabainika kuwa ni bakteria (H. pylori) basi dawa ya kuangamiza bakteria ‘antibiotic’ hutumika.

Kwa vidonda vya tumbo vya kawaida, daktari hutoa dawa zinazofanya kazi ya kuzuia tumbo kuzalisha kiwango kikubwa cha tindikal.

Pia, kuna dawa nyinginezo zinazosaidia kuzuia chembehai zinazozalisha tindikali na dawa kusaidia kuweka mazingira ya tumbo vizuri kwa kupunguza ukali wake.

Dalili za vidonda zinaweza kupotea mapema, mara tu baada ya kuanza matibabu. Lakini, hata baada ya dalili kupotea mgonjwa, bado mgonjwa anapaswa kuendelea kutumia dawa alizopangiwa na daktari hadi hatua ya mwisho.

Hilo ni muhimu sana, hasa pale chanzo cha vidonda kinapokuwa ni bakteria. Inashauriwa, pia mgonjwa aliye katika matibabu asijihusishe na maumizi ya pombe, sigara, dawa na chakula kinachoamsha dalili za vidonda.

Kwa mara chache, vidonda vyenye hali ya hatari, vinachangia kufanyike tiba ya upasuaji na hiyo ni pale vidonda vinapojitokeza kila mara, havipo, vinatoa damu, vinachangia kulika kwa ukuta wa tumbo au utumbo mdogo.

Ni aina ya upasuaji unaoweza kuhusisha hatua kama: Kukiondoa kidonda chote, kuondoa nyama sehemu nyingine ya utumbo na kuziba sehemu ya kidonda na kukata mawasiliano ya fahamu ya tumbo kupunguza uzalishaji wa tindikali.

Mtu anapaswa kuelewa kwamba, kupata matibabu mapema iwezekanavyo mara tu baada ya kugundua kuwa una vidonda vya tumbo, ni jambo muhimu.

DALILI ZAKE

Kadri vidonda vinavyoachwa bila kutibiwa, ndivyo vinavyoleta madhara makubwa zaidi baadaye.

Mtu anapaswa kufika hopitalini haraka kumuona daktari, mara tu baada ya kupata mojawapo ya dalili zifuatazo: Kwanza, maumivu ya ghafla ‘yanayokata’ na hayakomi tumboni, kutoa kinyesi chenye rangi nyeusi au chenye damu au kutapika damu.

Dalili hiyo ni kiashiria kizuri kuwa kidonda kimemega sehemu ya ukuta wa tumbo au mshipa wa damu.

KUUDHIBITI UGONJWA

Ili kuzuia kusambaa kwa bakteria na kupunguza uwezekano wa kuwapata, watu wanapaswa kunawa mikono kwa sabuni kila mara, pia kuhakikisha chakula chao safi na kimepikwa vizuri.

Kuzuia vidonda vinavyosababishwa na matumizi ya dawa za kundi la ‘Nsaid’ kama aspirini. Ni busara kuepuka kwa kadri mtu anavoweza.

Kama mtu anahitaji kutumia dawa hizo, anapaswa kuhakikisha anatumia dawa kadri ilivyopendekezwa na daktari na kuepuka matumizi ya pombe, wakati anatumia dawa za kundi hilo.

Inaelezwa, kuwapo baadhi ya tabia au mitindo ya maisha inayosaidia kuzuia watu kupatwa na vidonda vya tumbo.

Tabia hizo za kuepukwa zinajumuisha ukwepaji matumizi ya pombe, sigara, msongo wa mawazo uliopitliza.

Hiyo yote inatajwa kusaidia kujenga ukuta wa tumbo katika hali ya uimara na wenye afya, hivyo kuondoa uwezekano wa kupata vidonda.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live