Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Vyuo vya afya mbioni kuja na mtalaa mmoja

Wed, 20 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Vyuo vikuu vitatu vimeanza kukusanya maoni ya wadau kwa ajili ya kuandaa mtalaa linganifu wa mafunzo katika elimu ya watoa huduma za afya nchini (THET).

Vyuo hivyo ni Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas) Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba cha Bugando (Cuhas) na Chuo Kikuu Kishiriki cha Tiba cha Kilimanjaro (KCMC).

Akizungumza mara baada ya kuzindua mradi wa miaka mitano utakaohusisha ukusanyaji maoni ya kuandaa mtalaa, Profesa Ephata Kaaya aliyewahi kuwa makamu mkuu wa Muhas alisema kwa miaka mingi vyuo vya afya vimekuwa vikitumia mitalaa tofauti tofauti jambo ambalo hutofautisha uwezo wa wahitimu.

“Wiki hii tutakuwa na mkutano na wadau kukusanya maoni yao na tutakuwa tunakaa na wataalamu mara kwa mara ili kupata maoni yao ya jinsi ya kuboresha utoaji wa huduma za afya wenye ubora, ikiwamo wahitimu wenyewe waeleze wapi kuna kitu kimeungua kweli elimu yao na wanataka kiongezwe, ” alisema Profesa Kaaya.

Alisema mradi huo wa miaka mitano gharama yake ni dola 600,000 kwa mwaka ambapo kwa miaka mitano utagharimu dola milioni tatu lengo lake ni kuanzisha mtalaa linganifu utakaowafanya wahitimu kutoka katika vyuo vyote vya afya nchini kuwa na uelewa, weledi na ujuzi unaolingana.

Kwa upande wake, Dk Doreen Mloka mkurugenzi wa mafunzo endelevu na weledi kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili alisema hapo awali hakukuwa na mwongozo wa elimu ya afya itoleweje kutokana Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) hivyo kila chuo kilikuwa kinafundisha kivyake.

“Kuanzia kesho tutakutana na wadau 60 wakiwamo waajiri ambako wanafunzi wa masuala ya afya wakihitimu wanakwenda kuajiriwa ili kujua kuna upungufu upi wanaouona, lakini na wahitimu wetu pia nao waeleze katika mafunzo yao wanataka nini kiongezwe baada ya hapo tutajadili tulichokipata na kuandaa mitalaa” alisema Dk Mloka.



Chanzo: mwananchi.co.tz