Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Daktari bingwa anayerekebisha jinsia, kutenganisha watoto pacha

Video Archive
Mon, 7 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Si maarufu sana, lakini ni kiungo muhimu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH). Ni Dk Zaituni Bokhary.

Dk Zaituni, mkuu wa kitengo cha upasuaji watoto, ni daktari bingwa aliyeshiriki kutenganisha pacha walioungana kwa miaka tofauti.

Lakini sifa ambayo haijasemwa kwa sauti kubwa ni ile ya kusaidia watoto wanaozaliwa na jinsi tata (ya kike na kiume); anawarekebisha upasuaji wa njia ya matundu (laparoscopic) na kuiachia jinsi ambayo ina uwezo zaidi ndani ya mwili wa mtoto.

Dk Zaituni, ambaye kikazi anajulikana kama Dk Tuni, ndiye aliyeshiriki na hata kufanikisha upasuaji wa kutenganisha pacha walioungana takribani mara nne, wakiwemo wa hivi karibuni waliofanyiwa upasuaji nchini Saudi Arabia.

Katika miaka minne ya udaktari bingwa katika upasuaji, amefanikiwa kutibu watoto wenye matatizo kama kushusha kokwa (korodani) za watoto wa kiume ambazo husalia tumboni wakati wa uumbaji, kuwawekea njia ya haja kubwa na hata uke kwa wale wanaozaliwa bila viungo hivyo muhimu.

“Nimezaa nina watoto watatu, nikiwa kazini kila mtoto ninayemfanyia upasuaji huwa nahisi ni mwanangu,” anasema Dk Zaituni katika mahojiano maalumu na Mwananchi.

Pia Soma

Advertisement
“Ninajikuta nafanya kazi kwa uadilifu na hata ikitokea kitu kikaenda tofauti, huwa natoa hata machozi. Napenda nikimfanyia upasuaji mtoto siku ya pili awe amepata fahamu, najisikia fahari sana.”

Bingwa huyo anayesimamia upasuaji kwa watoto 10 mpaka 12 kwa siku, anasema kazi yake kubwa ni kurekebisha viungo vya watoto.

“Kuna watoto hawana njia za haja kubwa unamuwekea njia yake. Wapo wanaozaliwa na utumbo mkubwa ambao zile seli zinazosaidia mtoto kupata choo zinakuwa hafifu, hivyo anakuwa na tumbo kubwa na hapati choo, hawa ninawafanyia wakiwa na kuanzia siku mbili tatu tangu wamezaliwa na oparesheni yake ni kubwa,” anasema.

“Kwa mfano leo (Septemba 30) nilikuwa nafanya upasuaji kwa mtoto wa kiume mrija wa haja ndogo haukuwa kwenye uume ulikuwa chini, hivyo nausogeza uje katikati ili ajisaidie kama watoto wengine hapa tunatengeneza uume.

“Tunafanya upasuaji huo wa kuunganisha mirija iliyofunga katika sehemu mbalimbali. Huu tunafanya kwa njia ya matundu madogo pia au kitaalamu laparascopic na ni upasuaji ambao tunaufanya tangu mwaka 2018 nchini Tanzania ni Muhimbili pekee tunafanya matundu kwa watoto.”

Wapo wanaozaliwa na tumbo ambalo halina mawasiliano au muunganiko na mdomo, anasema Dk Zaituni, kwa kuwa sehemu ya koo inakuwa imeziba.

“Mara nyingi watoto hawa hushindwa kunyonya kwa kuwa hakuna kinachopita kuingia tumboni, hao hufanyiwa upasuaji kuunganisha koo na tumbo baada ya kuzaliwa,” anasema.

Pia alizungumzia watoto wanaozaliwa na jinsia mbili.

“Haijulikani kama ni wasichana au wavulana na tunafanya kwa kutumia upasuaji huu. Kamera inanisaidia kujua kama ana mfuko wa uzazi au ni mwanaume ninaona na hapo pia tunakuwa tulishafanya vipimo awali tunaelewa homoni zipi ni nyingi zaidi,” anasema.

Dk Zaituni anashauri wazazi wanaoona watoto wao katika maumbile yanayotia shaka, kuwawahisha hospitali ili warekebishwe.

Alisema tangu wameanza upasuaji huo, watoto 57 wamerekebishwa kwa mafanikio makubwa na hawakulazimika kufungua tumbo.

Alisema mafanikio hayo yametokana na uwekezaji uliofanywa kuanzia mwaka 2017 uliowezesha kupata vyumba viwili vya upasuaji katika jengo la watoto na kuongeza idadi ya watoto wanaohudumiwa kutoka watatu mpaka 10-12 kwa siku.

Kutenganisha watoto pacha

Lakini daktari huyo anajulikana zaidi kutokana na kutenganisha pacha walioungana. Alishiriki kwa mara ya kwanza upasuaji huo mwaka 2012 nchini India alikowapeleka pacha wa Kyela mkoani Mbeya, Elikana na Eliudi.

“Hawa waliungana sehemu ya tumbo, nyonga na walikuwa wanatumia viungo mbalimbali pamoja, kesi yao ilikuwa ngumu,” anakumbuka.

“Nikiwa daktari wa upasuaji ninayehitaji kujifunza, nilisafiri nao mpaka China Pediatric Hospital.”

Alisema baada ya kuonekana wangeweza kutenganishwa, upasuaji ulifanyika na walipandikizwa nyama ili kufunika matumbo yote mawili.

Alisema alirudi kuendelea na masomo yake Cairo, Misri baada ya vipimo na wakati wa upasuaji aliitwa na kushirikiana na jopo la madaktari tisa.

Dk Zaituni alisema pacha wengine, Meryness na Anissia, walitokea Kagera, Misenyi Mabare mwaka 2018 ambao waliungana sehemu ya kifua, tumbo, nyonga na viungo vya ndani kwa asilimia kubwa kibofu cha mkojo.

Walisafirishwa kwenda Saudi Arabia kwa kugharimiwa na mfalme wa nchi hiyo. Walikuwa na umri wa chini ya siku 24 tulikaa nao na walikaa nao kwa miezi sita wakati wakikusanya taarifa.

Upasuaji huo ulishirikisha madaktari wa mifupa, ini, figo, moyo, maambukizi, plastic surgery na viungo.

Alisema baada ya wote kuwachunguza walifanya kikao cha madaktari na yeye alitoa taarifa ya hatua walizopitia tangu kuzaliwa.

“Walikuwa na miguu mitatu na ule wa tatu ulikuwa haufanyi kazi, lakini tulifanya kazi kubwa nzuri,” anasema na kuongeza kuwa kila mmoja alipata mguu mmoja.

Alisema upasuaji ulifanyika Desemba 23 mwaka jana na ulichukua saa 14 ukishirikisha madaktari zaidi ya 15 wakiwemo wenyeji wengine kutoka nje ya Saudi Arabia.

Dk Zaituni anasema japokuwa mmoja alifariki dunia baada ya kurudi nchini salama, pacha anayeishi atakwenda Saudia miaka minne baadaye ili kuwekewa mguu bandia.

Itaendelea kesho

Chanzo: mwananchi.co.tz