Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uzito uliozidi husababishwa na nini?

Obesity Uzito Mnene Uzito uliozidi husababishwa na nini?

Mon, 1 Aug 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Mbali na jitihada za kupunguza tatizo la udumavu na utapialo, kuna ongezeko la uzito uliokithiri na viribatumbo.

Viwango vya utapiamlo, ikiwamo uzito uliozidi kwa wanawake wenye umri wa kuzaa vimeongezeka.

Takwimu zinaonyesha tatizo la uzito uliokithiri kwa wanawake walio katika umri wa kuzaa limeongezeka kutoka asilimia 29.7 mwaka 2014 hadi asilimia 31.7 mwaka 2018 (TNNS, 2018).

Mikoa ya Dar es Salaam, Kilimanjaro, Arusha, Mbeya na Unguja Mjini Magharibi inaongoza kwa tatizo hilo.

Uzito wa mwili hutegemea kiasi na aina ya chakula unachokula pamoja na shughuli unazofanya.

Mara nyingi tatizo hilo hutokana na kula kwa wingi kuliko mahitaji ya mwili na kutofanya mazoezi.

Mahitaji ya chakula mwilini hutegemea umri, hali ya kifiziolojia ulionayo (kama una ujauzito au unanyonyesha), kazi na mtindo wako wa maisha.

Endapo kiasi cha chakula unachokula kinatoa nishati-lishe kuliko mahitaji ya mwili, ziada hii huhifadhiwa mwilini kama mafuta, hivyo kuongezeka kwa uzito wa mwili.

Unaweza kupata madhara?

Uzito uliozidi na kiribatumbo vina uhusiano na magonjwa yasiyoambukizwa.

Pia, unachangia kwa kiwango kikubwa kupata magonjwa sugu yasiyoambukizwa kama kisukari, magonjwa ya moyo, shinikizo kubwa la damu na hata saratani.

Uzito uliozidi na viribatumbo vinachangia kuzuia mwili kutumia sukari kwa ufanisi na husababisha kuongezeka kwa mafuta mwilini ambayo hujikusanya kwenye mishipa ya damu na kufanya damu isipite kwa urahisi, hivyo kusababisha msukumo mkubwa wa damu.

Wakati mwingine hali hii husababisha damu isifike kwa kiasi cha kutosha katika viungo kama moyo, ubongo na misuli.

Hali hiyo husababisha moyo kushindwa kufanya kazi kabisa (heart failure) au moyo kukosa damu ya kutosha (ischemic heart disease).

Utumie mbinu gani kuepuka?

Mbinu za kutumia ili kuepuka uzito uliozidi na kiribatumbo ni kuwa makini na ulaji kwa kuangalia kiasi, ubora na idadi ya milo kwa siku.

Kula mlo kamili kwa kuzingatia vyakula vya aina mbalimbali, hasa mbogamboga na matunda na chagua asusa zisizo na kalori nyingi. Unaweza pia kubadilisha njia za kupika zinazotumia mafuta mengi kwa kuoka, kuchemsha, kupika kwa mvuke au kuchoma. Pia, epuka matumizi ya vyakula vinavyotoa nishati-lishe kwa wingi kama vile vilivyopikwa kwa kutumbukizwa kwenye mafuta.

Epuka vyakula vyenye mafuta na sukari nyingi, badala yake kula matunda na mbogamboga kwenye kila mlo.

Kuwa makini unapokula nje ya nyumbani kwa kuchagua vyakula vyenye nishati-lishe kidogo.

Ni vyema unapopunguza uzito usikae bila kula kwa muda mrefu, bali badilisha utaratibu wa kula na aina au kiasi cha chakula.

Pia, kuwa na desturi ya kufanya mazoezi ya mwili ili kuuwezesha mwili kutumia nishati lishe iliyozidi mwilini na kuzuia isihifadhiwe mwilini na kusababisha unene.

Kuwa na desturi ya kutembea badala ya kupanda gari hata pale penye umbali mfupi; panda ngazi badala ya kutumia lifti, fanya shughuli za nyumbani na shiriki katika michezo.

Ukifanya mazoezi na kusikia njaa, kula mbogamboga na matunda.

Mazoezi yaanze kwa taratibu; kwa muda mfupi na jinsi mwili unavyozoea, kasi, ugumu na muda wa mazoezi uongezeke.

Ni rahisi kuongezeka uzito lakini ni vigumu kuupunguza.

Inatakiwa kuwa na nidhamu katika kutekeleza mikakati uliojiwekea. Ni lazima kuwa na subira; inachukua muda na inawezekana.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz