DAKTARI bingwa wa magonjwa ya moyo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dar es Salaam, Dk Yona Gandye ametaja mambo kadhaa yanayosababisha moyo kutanuka ikiwamo uvutaji sigara na unywaji pombe uliokithiri.
Ametaja sababu nyingine kuwa ni magonjwa hatarishi ukiwamo sukari, shinikizo la juu la damu, uzito mkubwa, urithi kutoka kwa wazazi na maambukizi yanayotokana na virusi au bakteria au fangasi.
Aliyasema hayo wakati akizungumzia mafanikio ya kambi ya siku mbili ya wataalamu wa JKCI kutibu magonjwa ya moyo jijini Dar es Salaam.
Alisema wakati wa kambi hiyo, wagonjwa wanne waliwekewa kifaa cha kuusadia moyo kufanya kazi vizuri kijulikanacho kitaalamu kwa jina la Cardiac Resynchronization Therapy Device – CRT-D.