Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Utoaji mimba hutesa hata watoto walionusurika

2cec9147ec17e739c1d462905f186e98 Utoaji mimba hutesa hata watoto walionusurika

Mon, 7 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

JULAI 20, 2020, niliandika makala katika gazeti hili iliyoitwa ‘Laana nne Kwa mwanamke Anayetoa Mimba.’ Kwa kutumia vyanzo mbalimbali likiwamo shirika moja la kimataifa linalotetea uhai la Human Life International (HLI), katika makala haya nitazungumzia namna laana ya utoaji mimba inavyowatesa watoto walionusurika.

Nitaanza kwa kurejea kisa kimoja kilichochapishwa na HLI. Hiki ni kisa cha Bernadetta Thompson wa Uingereza ambaye baada ya kuharibika mimba yake ya kwanza, na kumuua mtoto wake wa kwanza (ambaye sasa angekuwa wa pili), alikabiliwa na matatizo mbalimbali yakiwemo ya kisaikolojia.

Haya ni pamoja na kushindwa kumshika mtoto mchanga, kuwa na mwelekeo ya kujiua, kujichukia mwenyewe na kumchukia kila mtu, kujihisi kuukosa umama wa kweli na kujihisi kutaka kumdhuru mtu mwingine.

Tatizo lingine la kisaikilojia kama tulivyoona katika makala ya Julai 20, mwaka huu, ni pamoja na kujihisi kupotelewa na kitu fulani, kujihisi mkosaji, kuwa na fikra kali na hata kusikia vilio vya watoto wachanga na ndoto za vitoto vilivyojipanga katika mistari vikiwa vimefungwa minyororo.

Chapisho hilo la HLI mtandaoni linasema baada ya mikasa hiyo miwili, Bernadetta alibahatika kujifungua mtoto na kumwita jina lake Benjamin.

“Akiwa bado mtoto na katika hatua zake za kukua, Benjamin alikwa anaota ndoto za kuweweseka kuwa alikuwa anafukuzwa na mama yake aliyekuwa ameshika kisu akitaka kumuua,” linasema chapisho.

Linaongeza: “Ndoto hizi za Benjamin ziliisha pale mama yake alipomfahamisha kuwa, alikuwa ametoa mimba, yaani alimuua kaka yake.”

Kisa hiki kinabainisha kuwa, damu ya mtoto anayeuawa katika tendo la utoaji mimba, hulia katika nafsi za watoto walio hai ambao wamezaliwa na mama huyo.

Kabla hatujaenda mbali, ni vyema kujua watoto walionusurika ni akina nani hawa na kama sisi wenyewe tunaweza kuwa miongoni mwa watoto walionusurika kuuawa na mama au baba zao kupitia utoaji mimba.

Kimsingi, watoto walionusurika ni pamoja na wale waliozaliwa baada ya jaribio la kutoa mimba (kimwili) kushindikana; waliozaliwa baada ya wazazi wao kutishia kuwaua (kwa maneno), waliozaliwa kabla au baada ya mwenzao wa mama mmoja kuuawa, waliozaliwa katika mazingira ambapo wenzao wengi wanauawa na wale wanaozaliwa katika nchi ambazo zimetunga, zimepitisha na zinatumia sheria ya kutoa mimba.

Uchunguzi HLI unaonesha kuwa, watoto hawa hawajafanya kosa linalostahili adhabu, bali ‘laana’ hii inamhusu mama aliyeua watoto wake kwa njia ya utoaji mimba.

Katika mazingira haya, atharui za utoaji mimba zinakuwa na matokeo mabaya kwa watoto wanaozaliwa na mama huyu.

Imebainika kuwa watoto wengi walionusurika hawaoni thamani ya kuishi na pia, hawaoni thamani ya uhai wao au watu wengine.

Jiulize ni mara ngapi umewahi kumsikia mtoto au hata mtu mzima akimwambia mwenzake: “Nitakuua.”

Hapo ndipo watu hujiuliza kuwa, kauli hizi zina maana gani na wengine huchunguza kutaka kujua kitu kilichosababisha hasira ya kiwango hiki cha mtu kutamka au kutishia kumuua mwingine.

“Hata siku hizi tunashuhudia vitendo hivi katika matukio ya yutanasia (mauaji ya huruma), ambapo mtu, kutokana ama na ugonjwa au umri kuwa mkubwa, anamwomba daktari au mtu mwingine amuue ili kumwondolea mateso aliyo nayo,” linasema HLI.

Linaongeza: “Pengine daktari baada ya kumhudumia mgonjwa kwa muda mrefu pasipo matumaini ya kumponyesha, anakengeuka na kushauri mgonjwa wake aombe kifo kama tiba kwa ugonjwa wake…”

Hapa lazima ifahamike kuwa katika hali ya kawaida, watoto hao huishi na hofu ya kuuawa wakati wowote, hivyo wanashindwa kufanya mipango ya maisha ya baadaye. Mfano wa kisa cha Benjamin aliyekuwa anaota anakimbizwa na mama yake aliyetaka kumuua, unahusika sawia na kuthibitisha kuwa, katika hali ya namna hiyo, ni vigumu mtu kuweka mipango ya maisha kwa kuwa hofu ya kifo humtawala katika maisha.

Niliwahi kusoma makala moja iliyoandikwa na Joseph Sabinus ikiuliza: “Kwa nini Watu Hulia Msibani?” Sambamba na vyanzo vingine, ilibainika kuwa msibani watu hulia kwa sababu mbalimbali.

Wengine hulia kwa kuwa marehemu alikuwa tegemeo katika familia ama ni mume, mke, ndugu, jirani au rafiki. Wengine hulia kwa kuwa walikuwa wanamdai marehemu na wengine hulia kwa kuwa mhusika amefariki dunia kabla hawajatimiza mipango au uhadi Fulani.

Wapo pia ambao hulia wanapokumbuka kuwa ipo siku nao watakufa na kuwa katika hali aliyopo marehemu sasa lakini wapo ambao hulia kwa kuwa msimba huwakumbusha vipenzi vyao waliokwisha tangulia mbele za haki.

HLI inasema: “Lakini kwa mtu aliyenusurika kifo kutokana na utoaji mimba uliofanywa na mama yake, kilio chake kinaweza kuwa kinatokana na sababu kwamba, yeye anajiweka kama ndiye aliyekufa. Hii ndiyo hofu ya kifo.”

Atharo nyingine ni madai kwamba, watoto hao mara nyingi wanashindwa kuwaamini na kuwathamini wazazi wao.

Kwa kawaida, watoto huwaheshimu na kuwathamini wazazi wao kutokana na silika ya kimahusiano kidamu, imani na mila zetu.

Kwa mujibu wa Mandiko Matakatifu, Amri ya Nne ya Mungu, inawaamuru watoto kuwapenda na kuwaheshimu baba na mama ili wapate miaka mingi na heri duniani. Hapo, upendo na heshima kwa wazazi unapata matunda yake katika tuzo. Jamii haitegemei kuwaona au kuwasikia watoto wakiwadharau au kuwatukana wazazi wao.

“Vitendo vya utoaji mimba vimezua laana kwa watoto ambao sasa huwatukana wazazi, kutishia kuwaua (au hata kuwaua), kuwatelekeza na hata kuwapiga wazazi wao. Moyo wa ukatili wa mama umehamia kwa mtoto ambaye nayo anaudhihirisha kwa kumgeukia huyo mama mwovu,” inasema HLI.

Kwamba, katika matendo kama hayo, mara nyingi jamii imeelekeza lawama kwa watoto wanaopachikwa tuhuma mbalimbali. Hapa, ni vyema kutafakari upya tuhuma hizo.

Kimsingi, mtoto aliyenusurika hawezi kumthamini mama yake kwani anajihisi kuwa mama yake ni mkatili na muuaji, hata kama hajaambiwa kuwa kaka zake au dada zake waliuawa kwa kazi ya akili na mikono ya mama yake.

‘Laana’ hizo zinaonekana hata siku hizi katika maeneo na matukio mbalimbali yakiwamo yanayoshuhudiwa ya baadhi yawatoto kuwashikia silaha mama zao na kutaka kuwaua au wengine kuwaua kabisa. Hata hivyo, siyo kwamba wazazi (mama) wote wanaokumbana na mikasa hii walijihusisha na ukatili wa mauaji kwa utoaji mimba.

Uchunguzi pia unabaini kuwa, mara nyingi watoto walionusurika kuuawa kupitia utoaji mimba, wanakuwa wanyonge na wenye hasira kali.

Biblia takatifu inasema katika uumbaji wake, Mungu alimuumba kila binadamu akiwa mwenye furaha, amani, upendo na tunu nyinginezo.

Hata hivyo, katika hali ya utoaji mimba, mama anafuta hizo tunu njema za Mungu na kupandikiza kwa watoto wanaozaliwa kabla au baada ya mwenzao kuuawa tunu hasi za unyonge na hasira kali kwa sasabu mwenzao ameuawa. Huu ni unyonge wa kila mfiwa na hasira hizo ni kwa sababu kifo hicho kimesababishwa na ukatili wa mama.

Kwa hiyo uzao unajenga hasira siyo kwa mama huyo tu, bali kwa kila mwanamke. Hata watu wasiohusika watamwona mtoto huyo kuwa mwenye hasira zinazoelekezwa kwa kila mmoja.

Kwa mujibu wa watalaamu mbalimbali wa masuala ya elimu na saikolojia, walimu wanapobaini kuwapo kwa watoto wa aina hiyo, wafanye jitihada za makusudi na kipekee kuwasaidia, badala ya kuwaadhibu au kuwaacha maana uhusiano baina ya mwalimu na watoto hao huathiri maendeleo yao kielimu.

Wataalamu wengine wamebaini laana kadhaa kwa watoto walionusurika zikiwamo za watoto hao kuwa na chuki kwa mama; kukosa upendo kwake na hata mama yake anaweza kujihisi vibaya.

Kwamba mara nyingi imebainika kuwa, mtoto huyo hamwamini mama, anajitenga na kukimbilia kwa baba yake (kama yupo). Muda mwingi anakuwa karibu na baba kuliko mama yake na kubwa zaidi, anajenga chuki kwa jinsi ya kike na kutowathamini wanawake.

Katika hali hiyo, jamii inahitaji washauri nasaha kuwasaidia watoto hao kuwarudishia ubinadamu waliopoteza; inahitaji mashirika ya hiari ili kuwahudumia kwa upendo na kuwarejeshea malezi yaliyopotea kutoka kwa wazazi wao.

Serikali iwe na mikakati zaidi kuwasaidia watoto hao na hasahasa, iongeze juhudi zaidi kudhibiti utoaji mimba.

Mwandishi wa Makala haya ni Mkurugenzi wa Shirika la Kutetea Uhai (PROLIFE) Tanzania. Anapatikana kwa 0713609641.

Chanzo: habarileo.co.tz