Kigoma. Serikali ya Tanzania kupitia Ofisi ya waziri Mkuu Sera, Utaratibu na Bunge na wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inaendesha shughuli ya utayari wa kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola nchini humo.
Akizungumza leo Jumatatu Agosti 5, 2019 na wadau wa afya mjini Kigoma, Mkurugenzi msaidizi utafiti na mipango idara ya menejimenti na maafa ofisi ya waziri Mkuu, Bashilu Taratibu amesema shughuli hiyo itafanyika kwa siku tano katika halmashauri tano za mkoa huo.
"Kwa awamu ya kwanza shughuli hii inafanyika kwa mikoa miwili wa Kagera ambapo tayari tumeshamaliza na sasa tupo mkoani Kigoma katika halmashauri ya Uvinza, Buhigwe, Manispaa ya Kigoma ujiji, halmshauri ya wilaya ya Kigoma na Kasulu," amesema Taratibu.
Amesema shughuli hiyo imejikita katika kuwafanyia majaribio wadau hao wa afya ambao tayari walishapata mafunzo lengo ni kuona jinsi watakavyokabiliana na mgonjwa wa Ebola akiingia nchini.
Awali, akifungua shughuli hiyo kwa niaba ya Katibu tawala mkoa Rashidi Mchatta, katibu tawala msaidizi, Daniel Machunda amesema nchi za jirani ya Demokrasia ya Congo (DRC), bado inakabiliwa na ugonjwa wa ebola tangu Agosti 2018.
Amesema mpaka kufika Julai 31, 2019, wagonjwa 2,973 wamepata ugonjwa huo huku vifo vikiwa 1,823 ikiwa ni asilimia 68 ya idadi ya watu waliopata ugonjwa huo.
Pia Soma
- Ulega atangaza fursa mazao ya bahari Tanzania
- Wafungwa, mahabusu kuanza kupimwa TB
- Mbunge hamasa ya uwekezaji wa Uingereza ziarani nchini