Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Utagunduaje mtoto amezaliwa na mguu kifundo?

80926 PIC+CCBRT Utagunduaje mtoto amezaliwa na mguu kifundo?

Mon, 21 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wataalamu wa mifupa nchini Tanzania wameonya kinamama wengi wamekuwa wakiwafikisha watoto waliozaliwa na tatizo la mguu kifundo (clubfoot) katika vituo vya afya kwa kuchelewa hivyo matibabu yake kuwa magumu.

Tatizo hilo limesababisha wengi wao kushindwa kupokea matibabu sahihi na kupona kwa haraka, kwa kuwa mifupa inapokomaa huchukua muda mrefu kupona na mtoto huhitaji upasuaji wa mara kwa mara kumrudisha katika hali ya kawaida.

Akizungumza na Mwananchi, Daktari wa mifupa kutoka CCBRT, Zainab Ilonga amesema wakunga na manesi wanapaswa kuwa wa kwanza kugundua tatizo hilo na mama pia.

Amesema kawaida mtoto mwenye tatizo hilo miguu huangalia chini au ndani, wakati mwingine mguu unakuwa mfupi au imetazama chini na inaangaliana, kwa kuangalia tu ni rahisi sana kugundua mtoto ana tatizo.

“Lazima tuanze matibabu akiwa na wiki mbili tangu kuzaliwa anapozidi kuchelewa mifupa inakomaa, misuli pia kwa kuwa sisi tunaanza kufunga POP ili kunyoosha mifupa akija mkubwa anaweza kuanza kuhitaji upasuaji mkubwa lakini akifika mapema tunamfunga POP na kufanya upasuaji mdogo tu kisha baada ya hapo tunaanza kumvalisha viatu,” amesema.

Dk Ilonga amesema huchukua miezi miwili mpaka mitatu mtoto huanza kuvaa viatu na atavivaa mpaka anafikisha miaka mitano miguu inakuwa imenyooka.

Pia Soma

Advertisement

Amesema tatizo la miguu vifundo duniani kati ya watoto 750 hadi 1000 mmoja huzaliwa nalo, “Hapa CCBRT kwa mwaka sisi walau tunaona watoto wapya wasiopungua 400 walioletwa kwa ajili ya matibabu.”

Hata hivyo, matibabu ya uhakika kwa watoto hawa yanahitajika. Mkurugenzi Mtendaji wa Tigo, Simon Karikari amesema wameamua kutoa kiasi cha Sh110 milioni kwa hospitali ya CCBRT ili kuweza kusaidia watoto wenye uhitaji wa matibabu hayo.

“Upatikanaji wa huduma za afya kwa wagonjwa wenye tatizo la mguu kifundo hasa watoto imekuwa ni changamoto kubwa hivyo tatizo hili linatakiwa kupewa kipaumbele, tunaamini msaada huu utaongeza ushiriki wa jamii na utayari wa wadau katika kuhakikisha matibabu ya uhakika ili kutoa fursa na wao kushiriki shughuli za maendeleo,” amesema Karikari.

Mtendaji Mkuu wa CCBRT, Brenda Msangi amesema kampuni hiyo ni sehemu ya maendeleo ya hospitali hiyo ikiwa ni pamoja na kuboresha maisha ya wagonjwa hasa watoto.

“Tigo imeonyesha mfano wa kazi ya sekta binafsi katika kutoa suluhisho kwa matatizo yanayozikumba jamii zetu, kwa miaka kadhaa tumefanikiwa kutatua changamoto ya matibabu ya ugonjwa huu kuhakikisha wanapatiwa huduma endelevu pamoja na ufuatiliaji wa mara kwa mara.”

“Kupitia wao tumeweza kuja na mfumo wa kuwakumbusha wateja wao kwa njia ya sms juu ya ufuatiliaji wa matibabu kwa wagonjwa ili kuhakikisha wanamaliza matibabu kikamilifu.”

Brenda amesema tangu waanze kutoa huduma hiyo, zaidi ya watoto 1,500 wameshanufaika na njia ya matibbau ya Ponseti (bila upasuaji) na kutibu mguu kifundo.

Tafiti

“Tatizo la mguu kifundo hapa Tanzania bado tafiti hazijafanyika nyingi sana siwezi nikazungumzia hilo labda baada ya utafiti zaidi kufanyika, watafiti bado hawajaweza kugundua chanzo ni nini lakini kuna visababishi mama fulani akapata mtoto mwenye tatizo hili kuliko mama mwingine labda kama kwenye familia kuna tatizo ni la kurithi.

“Lakini pia wanataja mimba za pacha pia ni rahisi watoto kutoka katika hali hii lakini pia linatokana na maradhi mengine kama mgongo wazi mara nyingi na wao wanakumbana na hili tatizo, lakini pia walio na mtindio wa ubongo pia linahusiana na mguu vifundo.” Amesema Dk Ilonga.

Chanzo: mwananchi.co.tz