Arusha. Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (Nimr) kwa kushirikiana na mtandao wa kujengea uwezo tafiti za afya katika nchi za Afrika Mashariki, imezindua mradi unaolenga kuibua wagonjwa wapya wa kifua kikuu (TB).
Akizungumzia mradi huo wa miaka mitatu, kaimu mkurugenzi wa kuratibu tafiti za afya Nimr, Dk Paulo Kazyoba alisema lengo ni kuboresha mfumo wa afya namna ya kugundua vimelea vya ugonjwa wa kifua kikuu nchini na kwa nchi za Afrika Mashariki.
Dk Kazyoba alisema mradi huo utaisaidia Nimr kufanya tafiti zitakazochangia kuboresha sera na utendaji katika sekta ya afya.
“Mradi huu utachangia kwa kiwango kikubwa kutupatia majibu ya namna ya kugundua haraka vimelea vya ugonjwa wa kifua kikuu,” alisema Dk Kazyoba.
Naye Profesa Sayoki Mfinanga kutoka kituo cha utafiti cha Nimr kilichopo Muhimbili, alisema mkutano huo unawahusisha watafiti wa afya kutoka nchi wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini.
Profesa Mfinanga alisema licha ya utaratibu mzuri wa kutoa tiba kwa wagonjwa wa kifua kikuu, mkakati zaidi unahitajika wa kuibua wagonjwa na kuhakikisha wanapatiwa matibabu hospitalini.
Alisema tatizo la kifua kikuu ni kubwa kwa nchi za Afrika na kwamba, jitihada zaidi zinahitajika katika kufanya tafiti za matibabu ili yawe chini ya miezi sita.
Akizungumza kwenye mkutano huo, mganga mkuu mkoa wa Arusha, Dk Timoth Onanji alisema wamefanikiwa kuibua wagonjwa wa TB kwa asilimia 74 mwaka 2016 ikiwa ni zaidi ya takwimu za Taifa ambazo ni asilimia 72.
Alisema mwaka 2017 waliibua wagonjwa kwa asilimia 75 na takwimu za Januari hadi Machi, zinaonyesha wamevuka lengo la Serikali kwa kufikia asilimia 85.
Dk Onanji alisema hilo linatokana na ufuatiliaji maeneo ya vijijini.
Takwimu zinaonyesha kati ya Januari hadi Machi wagonjwa wapya 3,180 waligundulika kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo.
Alisema changamoto kubwa ipo katika utambuzi wa watoto.