Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Utafiti: Asilimia 38 wenye VVU wana shinikizo la damu

HIV TEST.jpeg Utafiti: Asilimia 38 wenye VVU wana shinikizo la damu

Mon, 29 May 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

ASILIMIA 38 ya watu wenye maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) wamebainika kuwa na ugonjwa wa shinikizo la damu, hali inayowaweka hatarini kupata magonjwa yasiyoambukiza huku asilimia 10 kati yao wakionekana na mafuta yaliyozidi mwilini.

Asilimia hiyo ni kati ya watu 722 waliofanyiwa utafiti na Kituo cha Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu nchini (NIMR) Kanda ya Mbeya ambapo kati yao, 650 wamebainika kuwa na maambukizi na 122 hawana maambukizi.

Mtafiti Mkuu Mwenza wa Utafiti wa kundi la watu wa Afrika AFRICOS ambaye pia ni Mtafiti Mwandamizi wa NIMR Kanda ya Mbeya, Dk Lucas Maganga alitoa taarifa hiyo mwishoni mwa wiki alipozungumza na watumishi kutoka Ubalozi wa Marekani na Shirika la HJFMRI na waandishi wa habari nchini.

Taarifa ya Dk Maganga ni sehemu ya utekelezaji wa afua za kupambana na Ukimwi katika kuadhimisha miaka 20 ya mapambano dhidi ya maambukizi ya VVU kupitia mfuko wa dharura wa Rais wa Marekani wa kupambana na Ukimwi PEPFAR na washirika wake, WRAIR-DOD na HJFMRI mkoani Mbeya.

Alifafanua kuwa katika jitihada za mapambano dhidi ya VVU, NIMR kupitia Utafiti wa kundi la watu wa Afrika AFRICOS ambao unafanya kazi na nchi nne za Afrika ikiwamo Tanzania, Afrika Kusini, Nigeria na Kenya umesaidia kuboresha huduma za matibabu kama vile upatikanaji wa dawa za kufubaza makali ya Virusi vya Ukimwi.

Mtafiti wa VVU kutoka NIMR Kanda ya Mbeya na Mratibu wa AFRICOS, Dk Reginald Gervas alisema kuwa utafiti huo ni wa kwanza kuwahusisha watu wa Afrika na kwamba utasaidia matibabu rafiki kwa wananchi.

“Utafiti wa AFRICOS ambao unasaidia utafiti wa Ukimwi umesaidia kuboresha sera ya matibabu, kupunguza usugu wa dawa, pamoja na ushauri wa upatikanaji wa huduma za pamoja za Ukimwi na magonjwa yasiyoambukizwa,” alisema Dk Gervas.

Meneja wa Kituo cha Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu nchini NIMR Mikoa ya Nyanda za juu Kusini, Dk Nyanda Ntinginya alisema wameendelea kufanya utafiti na kuratibu utafiti wa AFRICOS pamoja na maabara inayotembea ili kuwapatia wananchi tiba sahihi ya maambukizi ya VVU.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live