Papai ni tunda lenye radha nzuri mdomoni, lakini ni chanzo kizuri cha asidi ya foliki ambayo huimarisha mfumo wa fahamu, hasa watoto, pindi mimba inapotungwa.
Kama ulikuwa hujui, jifunze sasa, papai ni tunda lililo na vitamini C kwa wingi pamoja na vitamini A.
Ofisa Mtafiti Mwandamizi wa Sayansi na Chakula, kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe( TFNC), Francis Modaha amesema vitamini C iliyopo katika papai, huimarisha kuta za mishipa ya damu, fizi na huondoa viini haribifu mwilini.
Amesema vitamini A iliyopo kwa wingi katika papai, huimarisha kinga mwili, uoni, ngozi, ukuaji mzuri wa mtoto na maendeleo mazuri kwa watoto wadogo.
Papai pia, lina vitamini B1, 2, 5, E na K na kwamba uwepo wa vitamini K husaidia ufyonzaji wa madini ya chokaa mwilini, hivyo huchangia kuimarisha mifupa.
Modaha amesema papai husaidia umeng’enyaji wa chakula kwa sababu lina vimeng’enyo.
Mtaalamu huyo wa lishe amesema uwepo wa kimeng’enyo kwenye tunda la papai bichi hutumika mara nyingi kulainisha nyama.
Modaha amesisitiza kuwa ulaji wa papai mara kwa mara husaidia kupunguza uwezekano wa kupata maradhi ya moyo kutokana na uwepo wa vitamini na madini mbalimbali katika tunda hilo.