Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ushauri wa USAID kwa serikali ya Tanzania kuhusu Afya

8fbdb63fca424cbbced6bae5baa753dd.png USAID yaishauri Tanzania afya

Wed, 25 Aug 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SHIRIKA la Kimataifa la Maendeleo la Marekani (USAID) limeishauri Tanzania kuanzisha mfumo madhubuti wa kuratibu sekta ya afya ili kutumia vizuri rasilimali na kupata matokeo chanya.

Mkurugenzi wa Afya wa USAID, Anathy Thambinayagam alitoa ushauri huo jana katika mkutano wa mwaka wa afya.

USAID imekuwa ikiisaidia Tanzania kufikisha elimu ya afya kwa wananchi kupitia mradi wake wa Tulonge Afya unaopitia Health Promotion Digital Platform (HPDP).

Alisema kuanzishwa kwa mfumo wa mawasiliano wa masuala ya afya kutaleta uhakika katika utekelezaji wa sera ya afya na kupata matokeo chanya.

“Mustakabali wa afya ni kutumia taarifa vizuri ili zisaidie kufanya maamuzi kwa taasisi na kwa watu binafsi; tunafurahia kuwa sehemu ya hili maana imesaidia kuboresha sekta ya afya na tunategemea kuendelea kufanya kazi pamoja ili kuboresha maisha ya wananchi wa Tanzania,” alisema.

Mradi wa Tulonge Afya unasaidia kuboresha mabadiliko ya tabia na masuala ya kijamii ambapo vikundi vya kuleta mabadiliko hayo vimeanzishwa katika mikoa 12 nchini.

Alisema mradi wa Tulonge Afya ulioanzishwa mwaka 2017 umetoa elimu juu ya Virusi vya Ukimwi, afya ya uzazi, afya ya mama na mtoto, malaria na kifua kikuu.

Alisema kutokana na dunia kukumbwa na ugonjwa wa Covid-19, USAID kupitia mradi wa Tulonge Afya imekuwa ikitoa elimu kuhusu kujikinga dhidi ya ugonjwa huo.

“Tumekuwa tunasaidia mawasiliano katika kuongeza mahitaji ya chanjo ya Covid-19 kwa kutoa elimu kwa wananchi na kuachana na upotofu wa taarifa kuhusu chanjo hiyo,” alisema.

Chanzo: www.habarileo.co.tz