Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Upungufu wa damu salama ni wa kudumu, daktari aeleza sababu

56154 Pic+damu

Tue, 7 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Msimamizi mkuu wa kitengo cha damu salama Mkoa wa Dodoma, Dk Leah Kitundya amesema tatizo la upungufu wa damu salama halitaisha kwa kuwa damu huisha muda wa matumizi yake siku 35 tangu kutolewa kwa mchangiaji.

Dk Kitundya ametoa kauli hiyo leo Jumanne Mei 7, 2019 jijini Dodoma akizungumza na Mwananchi Digital kuhusu upungufu wa damu salama mkoani Dodoma.

Amesema kwa siku Mkoa wa Dodoma unahitaji chupa 50 za damu salama lakini hata wasipotokea watu wa kuwaongezea damu hiyo, hulazimika kuiharibu siku ya 36 tangu mchangiaji aitoe.

“Tatizo la upungufu wa damu salama halitaisha hata siku moja kwa sababu damu tunayoichukua kwa wachangiaji inadumu kwa siku 35 tu siku ya 36 tunaiharibu kwa sababu inakuwa haifai tena kwa matumizi ya binadamu kwa hiyo unaona ni kwa jinsi gani tatizo hili haliwezi kuisha,” amesema Dk Kitundya.

Hata hivyo, ametoa wito kwa wakazi wa Mkoa wa Dodoma kujitokeza kwa wingi kuchangia damu kwa kuwa inahitajika kwa wingi kwa ajili ya kunusuru maisha ya watu.

Amesema wachangiaji wakubwa wa damu katika kitengo cha damu salama Mkoa wa Dodoma ni wanafunzi wa sekondari, taasisi za kidini na wanajeshi huku wanawake wakiwa nyuma kuchangia damu na wakati wao ndio wahitaji wakubwa.

Ameongeza kuwa ni wajibu wa kila Mtanzania mwenye afya njema kuchangia damu ili kuokoa maisha ya watu wengine, kwa kuwa kila siku kuna watu wanahitaji damu salama ili kuokoa maisha yao.



Chanzo: mwananchi.co.tz