Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Upungufu wa damu kwa watoto hupunguza uwezo wa kujifunza

68455 Mtoto+pic

Sun, 28 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Unajua madhara ya upungufu wa damu kwa mtoto huathiri uwezo wake wa kufahamu na kujifunza katika ukuaji wake? Damu ni sehemu muhimu ya mwili wa binadamu na ina mkusanyiko wa chembechembe nyekundu zinazotengenezwa na virutubishi vinavyopatikana kwenye chakula.

Virutubishi hivyo ni madini ya chuma, vitamini na folic acid, na vitamini B12.

Hata hivyo, mtu akikosa virutubishi hivyo, husababisha mwili kushindwa kutengeneza chembe chembe nyekundu na hatimaye hupata upungufu wa damu.

Dk Rehema Mzimbiri ambaye ni Ofisa Lishe Mtafiti kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania ( TFNC), anasema upungufu wa damu kwa mtoto huleta madhara ya kiafya na kuathiri ukuaji wake.

Dk Mzimbiri anataja madhara ya upungufu wa damu kwa watoto kuwa ni kupungua kwa kinga mwili na kupata maradhi ya mara kwa mara. “Vilevile husababisha mtoto kuwa dhaifu, mchovu na mwenye kukosa nguvu na kupungua uwezo wake wa kufahamu na kujifunza” anasema Dk Mzimbiri.

Mtaalamu huyo anasema tatizo la upungufu wa damu lisipochukuliwa hatua stahiki huweza kusababisha kifo.

Pia Soma

“ Hivyo, jamii ina wajibu wa kukabiliana na upungufu wa damu kwa watoto na hata watu wazima ili waweze kuwa na afya nzuri,” anasema.

Dalili za upungufu wa damu

Dk Mzimbiri anasema ili kuzuia tatizo la upungufu wa damu ni muhimu kuzijua dalili na kukabiliana nazo.

Anazitaja dalili za upungufu wa damu kuwa ni kujisikia dhaifu, kuchoka na kukosa nguvu na kizunguzungu.

“Dalili nyingine ni mapigo ya moyo kuongezeka, weupe usio wa kawaida kwenye macho, midomo, ulimi, viganja, kucha na hata katika ngozi, ni miongoni mwa dalili za upungufu wa damu,” anasema mtaalamu huyo wa lishe.

Pia, watoto na wajawazito wenye tabia ya kutamani kula udongo ni miongoni mwa dalili za upungufu wa damu.

Anasema dalili nyingine ni kuvimba miguu ambayo ni hatari, hivyo mtu atakapoona dalili hizo ni vyema kwenda hospitali kwa ajili ya kupata matibabu.

Hatua za kuzuia upungufu wa damu kwa mtoto

Dk Mzimbiri anasema inashauriwa baada ya mtoto kuzaliwa aanze kunyonyeshwa maziwa ya mama ndani ya saa moja ya mwanzo na kuendelea kwa miezi sita mfululizo. “Maziwa ya mama hasa yale ya mwanzo yenye rangi ya njano yanavirutubishi vyote muhimu kwa ajili ya afya ya mtoto, hivyo ni vizuri wazazi wakanyonyesha watoto wao,” anasema.

Mary Kibona ni Ofisa Mtafiti Lishe kutoka TFNC, anasema maziwa ya mama ni chakula na kinywaji pekee kinachotosheleza mahitaji ya mtoto tangu anapozaliwa hadi anapotimiza umri wa miezi sita.

“Kutokana na umuhimu wa unyonyeshaji, ndiyo maana nchi mbalimbali duniani ikiwamo Tanzania huadhimisha wiki ya unyonyeshaji wa maziwa ya mama kila ifikapo Agosti mosi hadi Agosti 7, lengo ni kutoa fursa maalumu kwa watu wote kubadilisha taarifa, ujuzi, mambo mema na kukumbushana umuhimu wa kulinda na kuendeleza unyonyeshaji wa maziwa mama kama njia bora zaidi ya kujenga afya ya mtoto kimwili na kiakili,” anasema.

Hata hivyo, Takwimu za Afya na Demografia Tanzania (TDHS 2015/16) zinaonyesha kuwa asilimia 98 ya wanawake nchini hunyonyesha watoto.

“Hii ina maanisha kuwa unyonyeshaji watoto maziwa ya mama ni njia kuu inayotumika kuwalisha watoto wetu,” anasema Kibona.

Pia, anasema pamoja na kiwango hicho kizuri cha unyonyeshaji, bado kuna tatizo la wanawake wengi kutonyonyesha kwa kufuata taratibu sahihi za unyonyeshaji, kama sheria zinavyotaka.

Dorisce Katana, Ofisa Lishe Mtafiti kutoka TFNC anabainisha kuwa licha ya kiwango hicho, wanawake wachache ndiyo wananyonyesha kwa ufanisi.

“ Licha ya takwimu hizo kuonyesha kiwango kizuri cha unyonyeshaji, ni asilimia 59 tu ya watoto wenye umri chini ya miezi sita wananyonyeshwa maziwa ya mama pekee, wengine wananyonyeshwa pamoja na kupewa kinywaji au chakula kingine tofauti na maziwa ya mama,” anasema Katana.

Hatua sahihi za unyonyeshaji

Neema Joshua, Ofisa Mtafiti Lishe kutoka TFNC anashauri kuwa baada ya kujifungua, mama anatakiwa kugusana na mtoto wake ngozi kwa ngozi, tendo hilo husaidia maziwa kutoka mapema.

“ Pia, kitendo cha mama kugusana na mtoto wake huongeza uhusiano kati ya mama na mtoto na humpa mtoto joto,” anasema Joshua.

Pia, anasema maziwa ya njano humsaidia mtoto kutoa kinyesi cha mwanzo chenye rangi ya kijani au nyeusi na humuepusha kuumwa tumbo na kupata ugonjwa wa manjano.

Joshua anasema mtoto aendelee kunyonyeshwa mara kwa mara na wala asipangiwe muda wa kunyonya bali anyonye kila anapohitaji.

Mtaalamu huyo anafafanua kuwa wakati wa kunyonya mtoto awekwe kwenye titi moja kwa muda wa kutosha kabla hajahamishwa kwenye titi lingine ili aweze kupata maziwa yote yanayotoka mwanzoni na yale yanayotoka mwishoni na kumuwezesha kushiba.

“Maziwa yanayotoka mwanzoni wakati wa kunyonyesha hukata kiu ya mtoto kwa kuwa yana maji mengi na yale yanayotoka baadaye huwa mazito; yana sukari na mafuta mengi ambayo humshibisha mtoto,” anasema Joshua.

Pia, anasema mtoto haruhusiwi kupewa chakula chochote hata maji isipokuwa kama italazimika kumpa dawa kwa ushauri wa mtaalamu wa afya.

“ Ni muhimu kutompatia mtoto maji au vinywaji vingine mpaka atimize umri wa miezi sita kwa kuwa maziwa ya mama yana virutubishi vyote muhimu na maji ya kutosha kukata kiu ya mtoto hata wakati wa joto kali,” anasema Joshua.

Chanzo: mwananchi.co.tz