Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Upimaji wa saratani karibu na wananchi utaboresha afya, kuokoa fedha za matibabu

10596 Upimaji+pic

Tue, 3 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kugundua dalili za awali za saratani ni njia bora ya kutibu ugonjwa huo kwa kuwa kuna baadhi ya dalili ambazo huonekana moja kwa moja ingawa idadi kubwa ya wanawake na wanaume huwa wanashindwa kuzitambua.

Watu wengi hasa waishio vijijini ni waathirika wakubwa wa ugonjwa huo kutokana na kukosekana kwa huduma za uchunguzi zilizo karibu nao, jambo linalofanya wagundulike wakiwa katika hatua za juu.

Takwimu zinaonyesha asilimia 80 ya wagonjwa wa saratani nchini hugunduliwa wakiwa katika hatua ya tatu na nne, jambo ambalo linaweka ugumu kwao wa kupona pindi waanzapo matibabu.

Mkurugenzi mtendaji wa Hospitali ya Saratani Ocean Road, Dk Julius Mwaisalage alinukuliwa akisema miongoni mwa sababu zinazochangia kuongezeka kwa wagonjwa wa saratani ni mtindo wa maisha.

Wengi hawafanyi mazoezi, unywaji wa pombe kupita kiasi, uvutaji wa sigara na ulaji mbaya wa vyakula.

Kupitia Mwananchi Jukwaa la Fikra lililoandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kwa ajili ya kujadili kuhusiana na maradhi yasiyoambukiza, alishauri ni vema nguvu nyingi zikawekezwa katika kukinga maradhi hayo kuliko kuyatibu.

Mwaisalage anasema upatikanaji wa huduma za uchunguzi wa saratani unatakiwa kusogezwa katika makazi ya watu kusudi kuhakikisha wananchi wanakuwa na uwezo wa kuzifikia huduma hizo.

“Licha ya kuwa sasa kuna vituo 600 vinavyoweza kubaini saratani ya mlango wa kizazi na matiti ambazo zinaongoza hapa nchini kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa, lakini bado vinatakiwa kuongezeka zaidi kwa sababu nchi ni kubwa,” anasema Mwaisalage.

Anasema mpaka sasa saratani ya mlango wa kizazi na matiti inachukua karibu asilimia 50 ya wagonjwa wote kwa mujibu wa takwimu kutoka taasisi ya saratani Ocean Road.

“Wagonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi hivi sasa ni asilimia 32.8 huku wagonjwa wa saratani ya matiti ni asilimia 12.9,” anasema Dk Mwaiselage.

Anasema licha ya kuwa Serikali imeongeza bajeti ya dawa kutoka Sh700 milioni miaka miwili iliyopita hadi Sh7 bilioni mwaka huu, bado kuna mgawanyo usio sawa kati ya maeneo ya mijini na vijijini.

“Mgawanyo usio sawa unatokana na ufikikaji katika baadhi ya maeneo, lakini pia upande wa tiba, sehemu nyingine kuna vifaa vinavyoweza kutumika, lakini mashine zinaharibika kila mara, hii pia ni changamoto,” anasema.

“Ni vyema kuhakikisha kuwa huduma ya uchunguzi kwa dalili za awali za ugonjwa wa saratani, uchunguzi na tiba zinapatikana karibu na makazi ya watu ili kupunguza wimbi la wagonjwa wengi walio katika hatua za mwisho,” anasema Dk Mwaiselage.

Mkurugenzi Mkuu wa Nimr, Profesa Yunus Mgaya anasema ni lazima watu wabadilishe mfumo wa maisha ili kujiepusha na maradhi ya saratani wanayoweza kuyapata baadaye na kulazimika kutumia fedha nyingi kuyatibu.

“Vingine havihitaji hela kubadili, tumewahi kupewa elimu mara kadhaa kuwa kuweka chakula cha moto katika vitu vya plastiki au mifuko tunaweza kupata saratani, kwanini tuendelee kutumia njia hizo na sio kubadilika,” alihoji Profesa Mgaya.

Alisema elimu inatakiwa kuwafikia watu wa sehemu nyingi ili kuhakikisha kuwa hakuna anayeachwa nyuma.

Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania (Mewata), Dk Faraja Chiwanga anasema kama wataalamu ni vyema kuangalia maeneo yenye uhitaji mkubwa kwa kufanya uchunguzi ili kujua mahitaji ya watu kabla ya kuwapatia elimu.

“Tuangalie ni eneo gani lina uhitaji sana ili kujiaminisha kuwa kile tunachokitoa kinawafikia watu sahihi, hakipotei bure, inaweza kusaidia katika kuwabadilisha watu na tukafanikiwa kugundua wagonjwa wengi walio katika hatua za awali,” anasema Dk Chiwanga.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu akichangia hoja katika mjadala huo, anasema miongoni mwa mikakati ambayo Serikali imeweka ni kupambana na maradhi yasiyoambukiza kwa sababu afya ndiyo mtaji wa uchumi.

“Ndiyo maana tuliamua kuanza kutoa chanjo kwa wasichana walio na umri wa miaka 14 ili kuhakikisha kuwa tunawalinda kama taifa la kesho na nipende kuwahakikishia kuwa, chanjo hiyo haina madhara kama inavyotangazwa,” anasema Ummy.

Anasema kabla ya chanjo hiyo kuanza kutumika, imethibitishwa ubora na Shirika la Afya Duniani (WHO), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na mkemia mkuu wa Serikali.

Anasema jitihada zinazofanywa na Serikali ni pamoja na kusogeza huduma za uchunguzi wa saratani karibu na makazi ya watu na kutenga siku maalumu kwa ajili ya kuhamasisha na kutoa elimu.

“Tutahakikisha walau kila kituo cha afya ngazi ya pili kinakuwa na huduma ya kupima na kuchunguza saratani ya mlango wa kizazi na matiti na tunazidi kupanua huduma za matibabu ili kupunguza mzigo wa wagonjwa katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road kwa kuwafanya watibiwe katika Hospitali ya Bugando, KCMC, na Hospitali ya Kanda ya Mbeya,” anasema Ummy.

“Tunaamini kuwa endapo vituo hivi vitaanza kutoa huduma za uchunguzi, idadi ya wagonjwa itaongezeka zaidi kuliko wale 50,000 wanaogunduliwa hivi sasa kila mwaka.”

Anasema pia katika kuhakikisha wanapambana na maradhi hayo, wizara imeanzisha kada rasmi ya watoa huduma wa ngazi ya jamii kwa kuwaweka wawili kila kijiji ambao watakuwa na kazi ya kuibua masuala ya chanjo, lishe, mazoezi.

“Shirika la Global Fund wametufadhili wahudumu wa afya 600 na Iris aid pia wametufadhili wahudumu wa afya 200 hivyo, tunaanza kidogo kidogo na baadaye tutahakikisha kuwa tunafika katika vijiji vyote,” anasema Ummy.

Ummy anasema Serikali inapoteza fedha nyingi kuwahudumia wagonjwa wanaofika hospitalini wakiwa katika hatua ya tatu na ya nne kutokana na uwezekano wao wa kupona kuwa mdogo.

“Kwa sababu tunajua kuwa ni ngumu kwa watu hawa kupona hivyo kinachofanyika ni kama kuwapunguzia maumicu makali wanayoweza kuwapata.”

Chanzo: mwananchi.co.tz