Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Upimaji wa hiari unavyosaidia  walioambukizwa VVU au TB 

Df16cb2a5fd9e40c8573b17eb2b6d720 Upimaji wa hiari unavyosaidia  walioambukizwa VVU au TB 

Mon, 5 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

“NILISHINDWA kuelewa nina aina gani ya kirusi cha ukimwi kilichonifanya nisijiweze aslani licha ya kutumia dawa za kufubaza kwa ufasaha kabisa. Wakati wenzangu niliomeza nao dawa wakinawiri na kuendelea na shughuli zao kama kawaida ikiwemo kilimo, mimi nilikonda na kuwa mtu wa kitandani muda wote,” anasema Neema Nestory aliyekua akisumbuliwa na ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB) huku pia akiishi na Virusi vya Ukimwi (VVU) kwa wakati mmoja.

Neema ni miongoni mwa wanaoishi na VVU zaidi ya miaka 10 sasa, wanaopata dawa za kufubaza virusi (ARV) katika Hospitali ya Wilaya ya Magu mkoani Mwanza.

Mwanamke huyu anasema hakutambua mapema kwamba alikua na magonjwa yote mawili, hadi ulipoanzishwa mradi wa ‘Boresha’, unaotekelezwa na Shirika lisilo la Kiserikali la AGPAHI (Ariel Glaser Pediatric Aids Health Care Initiative) kwa kushirikiana na serikali ya Tanzania kupitia Wizaya ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Pamoja na mambo mengine, mradi huo wa miaka mitano (2016-2021) umekua ukihimiza upimaji afya kwa hiari ili wanaogundulika na maambukizi waanze matibabu mapema na hivyo kutengeneza taifa lenye rasilimali watu iliyo imara.

“Watoa huduma (waliojengewa uwezo) wa Shirika hilo walinishauri kupima TB, na kukutwa nikiwa na maabukizi ambayo kumbe ndiyo yalikuwa yakinidhoofisha. Nilianza dawa mara moja na ndani ya muda mfupi nilirudia hali yangu ya kawaida na kufanana na wenzangu. Sasa natumia ARV tu na afya yangu ni njema, nashiriki shughuli za kilimo muda wote,”anasema.

Anasema alilazimika kumaliza dozi ya miezi sita kwa sababu tu ya kutimiza masharti ya wataalamu wa afya, lakini kimsingi alijihisi kupona ndani ya muda mfupi baada ya kuanza dawa.

Mradi wa Boresha umekuwa ukiwapatia mafunzo ya ushauri watoa huduma wa hospitali hiyo na baadhi ya wanaoishi na VVU pamoja na TB ili wawaelimishe wanajamii wengine juu ya umuhimu wa kupima afya kwa hiari na kupata matibabu stahiki kwa wakati.

Kutokana na kunufaika, Neema sasa ni mmoja wa watu wanaoshirikiana na watoa huduma katika kumshawishi kila anayefika hospitalini hapo kutembelea kitengo cha huduma na matibabu (CTC) kwa upimaji wa hiari, hata kama ana sababu nyingine tofauti iliyomleta hospitalini hapo.

AGPAHI pia humwezesha kila aliyepatiwa mafunzo kuwafuatilia wote wanaotumia dawa na kuhakikisha wanahudhuria kliniki ipasavyo.

Utaratibu huo wa kumfuata kila mgonjwa nyumbani kwake huwavutia wananchi wengi kupima afya kwa hiari na kuanza matibabu mapema kwa wanaogundulika na maambukizi.

“Nawashauri kujitokeza hata kama mtu haoni dalili. Binafsi sikuonesha dalili za wazi sana bali niliishia kukonda tu na kukosa nguvu. Hali hiyo ilinitesa ikizingatiwa niliambukizwa maradhi haya kikatili kwani marehemu muwe wangu hakunifahamisha mapema kwamba alikua na VVU,” anasema.

Mkuu wa Kitengo cha TB na Ukoma katika Hospitali hiyo, Mussa Itembe anasema mojawapo ya mafanikio ya mradi wa Boresha si tu uwepo wa dawa muda wote bali dawa ambazo hazina maudhi wala athari ya aina yoyote kwa mtumiaji.

Anasema Shirika la AGPAHI limekua msaada mkubwa, hasa inapotokea hospitali imeishiwa dawa kutokana na ongezeko la wagonjwa wanaotokana na upimaji wa hiari.

Shirika hilo hufanya mawasiliano ya haraka na vituo vingine vya afya vyenye dawa za kutosha na kuazima kiasi cha dawa hizo pamoja na kugharamia usafiri wa kuzileta Hospitali ya Magu ili asitokee mgonjwa wa kukosa huduma.

Anasema mara nyingi wagonjwa wa VVU hupewa dawa kinga inayojulikana kitaalamu kama ‘Isoniazid’ ili wasiambukizwe TB kwani magonjwa yote mawili yanapokutana humdhoofisha zaidi mgonjwa kutokana na mwili kushindwa kuyabeba yote kwa mpigo.

“Maana ya kutumia ARV ni kulinda kinga za mwili kwa anayeishi na VVU. Akiambukizwa na TB ni hatari kwani ina kasi ya kushusha kinga, hali inayoomdhoofisha zaidi mgonjwa na inaweza kusababisha kifo cha haraka. Lakini hata wanaopimwa na kugundulika tayari wana TB, dawa zipo na wanatibika haraka wakifuata masharti ya wataalamu wa afya,” anasema.

HabariLeo pia ilitembelea Hospitali ya Wilaya Misungwi, lengo likiwa ni kutafuta maoni ya wananchi ambayo wangeyatoa katika maadhimisho ya Siku ya Kifua Kikuu duniani, Machi 24, endapo usingetokea msiba wa Rais John Magufuli uliosababisha maadhimisho hayo kufutwa.

Mradi wa Boresha unatekelezwa pia katika hospitali hiyo huku watoa huduma wakijivunia ongezeko la wananchi wanaojitokeza kupima afya kwa hiari.

Mratibu wa wa masuala ya Ukimwi wa Wilaya ya Misungwi, Regina David, anasema kujitokeza kwa wingi watu kupima afya si tu kunasaidia mgonjwa kupata matibabu kwa wakati, bali pia kudhibiti maambukizi mapya katika jamii.

“Na katika CTC yetu tunatoa mafunzo ya namna ya mgonjwa anapaswa kujikinga na kuwakinga wengine. Tuna mazingira mazuri kwa kweli ikiwemo hili hema lililotolewa na AGPAHI. Linampa uhuru wa kujieleza kwani huingia mtoa huduma mmoja na mgonjwa mmoja. Tukiwa wahudumu wengi mgonjwa hukosa amani hata kama wote ametuzoea,” anasema.

Mratibu huyo anasema kutokana na utaratibu wa kupima kwa hiari, kuanzia Septemba hadi Desemba mwaka jana kituo (CTC) kilipokea wagonjwa wapya takribani 50, na tayari wengine wapatao idadi hiyo hiyo wamefika pia katika kituo hicho kuanzia Januari hadi Machi.

Mtumiaji wa matibabu ya TB kupitia kituo hicho, Mariam Joseph, anayetarajia kumaliza dozi yake mwezi huu, anatoa wito kwa wananchi kupima afya zao kama njia mojawapo ya kupunguza maambukizi mapya katika jamii.

Akizungumzi hali ilivyokuwa kabla ya mradi wa Boresha, daktari katika kitengo cha watu wenye VVU na TB, Sumbuo Kullaya anasema wagonjwa wengi walikua wakijitokeza wakiwa tayari katika hatua mbaya na hivyo kuyafanya matibabu kuwa magumu.

Anashukuru kuanzishwa kwa mradi wa Boresha ambao pia ulisababisha a kuundwa kwa Klabu (Ariel Club) inayowakutanisha watoto wanoishi na virusi vya ukimwi, wenye umri kati ya miaka tisa hadi 18 na kuwapatia elimu jinsi ya kuzuia maambuki mapya kwa wao wenyewe na wengine katika jamii.

Shirika la AGPAHI limekua likiwawezesha vijana hao kwa nauli na chakula wanapokuwa kituoni hapo na pia kuwawezesha kwa mambo mengine, hali ambayo imekua ikivutia vijana wengi kujitokeza na kupima afya zao, hivyo kujiunga na klabu hiyo kwa wale wanaogundulika na maambukizi.

Watoto chini ya miaka tisa wanaoishi na VVU pia wamekua wakipelekwa na wazazi au walezi wao hospitalini hapo ambapo, pamoja na mambo mengine, huhudhuria semina ya jinsi ya kuishi na watoto hao katika hali ya upendo bila unyanyapaa.

“Utaratibu huu ulianza mwaka 2017 na sasa tuna takribani vijana 90 na watoto (chini ya miaka tisa) 45. Huwa tunatembelea pia kitengo cha mama na mtoto, wakiwemo wajawazito ili kuwahimiza kupima na kujua hali ya afya zao lakini vilevile kuwaelimisha juu ya kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto,” anasema.

Chanzo: www.habarileo.co.tz