Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Upasuaji moyo JKCI kila siku

34155 Pic+upasuaji Tanzania Web Photo

Tue, 1 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imefanikiwa kupata daktari bingwa mzawa aliyebobea katika upasuaji wa kuziba matundu ya moyo kwa watoto.

Daktari huyo atashirikiana na daktari bingwa wa masuala hayo kutoka China na kuanzia Januari mwakani taasisi hiyo itaanza kutoa huduma hiyo, ambapo awali ilitoa kwa makundi kupitia kambi za madaktari kutoka nje ya nchi kutokana na kukosekana kwa wataalamu wa fani hiyo nchini.

Akizungumza na Mwananchi jana, Mkurugenzi wa Idara ya Magonjwa ya Moyo wa JKCI, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo, Dk Peter Kisenge alisema kutokana na kujijengea uwezo wa ndani sasa wataweza kufanya upasuaji huo kila siku.

“Tumepata daktari mmoja kutoka nje ya nchi ambaye atakuwapo hapa kwa miaka miwili atashirikiana na daktari aliyehitimu mafunzo ya uzibaji matundu ya moyo kwa watoto, Dk Godfrey Mbawala na sasa tutatoa huduma hii bila kusubiri wataalamu kutoka nje,” alisema.

Dk Kisenge alisema kila mwaka Tanzania watoto 13,000 wanazaliwa wakiwa na matatizo ya moyo, lakini ni 4,500 pekee wanaofanikiwa kufika taasisi hiyo kwa matibabu.

Alisema uwezo wa ndani kuimarika umechangiwa na msaada wa Serikali ya China, kwani bila hivyo JKCI isingefika ilipo sasa ambapo imekua tegemeo la Afrika Mashariki na Kati kwa matibabu ya kibingwa ya moyo.

“China imekuwa msaada mkubwa kwa JKCI kwa ujenzi wa jengo la hospitali hii baada ya Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete katika utawala wake kupewa msaada wa vifaa na mafunzo.”

“Karibu Sh16.4 bilioni zilitolewa na China kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hii pamoja na vifaa mwaka 2005 baada ya Rais Kikwete kupeleka wazo kwamba tunahitaji kuwa na taasisi ya kutibu moyo,” alisema.

Dk Kisenge alisema awali upasuaji wa moyo ulifanyika katika taasisi ya Mifupa Moi na walifanya kwa watu wachache kutokana na ufinyu wa nafasi na uhaba wa wataalamu.

Kwa upande wake, Daktari wa Usingizi kutoka China, Win Chengwei alisema amefurahi kufanya kazi na madaktari wa Tanzania na pia kuwa sehemu ya kusaidia kuokoa maisha ya wananchi kupitia huduma ya dawa ya usingizi anayotoa katika upasuaji na pia mafunzo kwa madaktari wengine.



Chanzo: mwananchi.co.tz