Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Upandikizaji figo ulivyoleta matumaini kwa watanzania

528b39c9e24870238491669ba736f8ae Upandikizaji figo ulivyoleta matumaini kwa watanzania

Mon, 15 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

“NILIANZA matibabu hapa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya kwa muda wa mwaka mmoja na nusu... Matibabu kwa kweli yalikuwa ni mazuri na madaktari walijitahidi kwa hali na mali. Kisha nikapewa rufaa kwenda Hospitali ya Benjamini Mkapa, Dodoma, nilikofanyiwa upandikizaji wa figo. Ilikuwa Novemba 4, mwaka jana.”

Hayo ni maneno ya Teofrida Mnyakiwele, mmoja wa watanzania walionufaika hatua ya utolewaji wa huduma ya upandikizaji wa gigo nchini. Historia hii anaitoa alipokutana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima.

Teofrida alikutana na Dk Gwajima wakati waziri huyo alipofanya ziara kutembelea wodi ya kliniki ya wagonjwa wa figo katika hospitali ya rufaa, kanda ya Mbeya ambapo pia alitumia safari hiyo kutoa tamko la Maadhimisho ya Siku ya Figo duniani yaliyofanyika Alhamisi iliyopita, Machi 11.

“Kwa kweli huduma ilikuwa ni nzuri. Naishukuru Serikali kwa sababu madaktari walionifanyia ile huduma ni wazawa. Mpaka hapo tunajua kwamba madaktari wetu wanao uwezo mkubwa sana… Na kama mnavyoniona mimi nimetoka salama na aliyenitolea figo kaka yangu naye yuko salama kama mnavyomwona hapa,” anasema Teofrida.

Anasema watanzania hawapaswi kuwa na mashaka juu ya huduma za upandikizaji zinazotolewa nchini kwa kuwa ushahidi unajionesha kwa waliopata huduma hiyo akiwemo yeye wako salama.

“Dk Octavian anaweza akaongea hapa. Awali nilikuwa nimedhoofu sana lakini baada ya kupata hii huduma ambayo serikali imetuletea kwa kweli naendelea vizuri na nina uwezo wa kufanya kazi zangu na aliyejitolea kunipa figo naye yuko vizuri na kazi zake anafanya kama kawaida,” anaongeza.

Anasema uamuzi wa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli ya kuweka msimamo wa matibabu ya msingi kutolewa ndani ya nchi badala ya kwenda nje kama ilivyokuwa miaka ya nyuma ndiyo uliowezesha wanyonge kuanza kupata walau tiba muhimu kwa ukaribu kutokana na uwekezaji uliofanyika kwenye sekta ya afya.

“Rais ana mchango mkubwa sana kwa kuwa amekuwa kiongozi anayesaidia sana kusimamia huduma za kijamii… Masuala ya afya, elimu na masuala mengine.

“Shukrani nyingine pia ni kwa Wizara ya Afya kwa sababu mimi nimefanyiwa upandikizaji wa figo kwa msaada wa Serikali... Kwa hiyo mpaka hapo tunaona kwamba serikali na watu waliopo katika serikali yetu wana ule moyo wa kujali wananchi. Wanajali wananchi kama mimi hapa na nimepona,” anasema.

Kaka wa Teofrida ambaye ndiye aliyejitolea kumpa dada yake figo, Fredrick Mnyakiwele anasema ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwezesha afya ya nduguye kurejea katika hali ya kawaida.

“Kulingana na jinsi dada yangu alivyokuwa anaumwa, nilikuwa nikipita hapa nikiwa na mawazo mengi na ningeweza hata kugongwa na gari pale barabarani. Lakini kwa jinsi madaktari wa hospitali ya rufaa kanda ya Mbeya walivyokuwa karibu na sisi pamoja na wauguzi wote kwa kweli walikuwa wakitufariji sana kuhusiana na suala la kumpandikizia figo mgonjwa wangu.

“Napenda kumshukuru Rais John Magufuli kwa moyo wake wa kizalendo na upendo kwa wananchi wake. Nilikuwa nikiona ni suala gumu sana kulingana na gharama ambazo zilihitajika kwa ajili ya kumpandikizia dada yangu figo na hasda kama wangelazimika kwenda India. Ni gharama kubwa ambazo kwa wananchi wenye hali ya chini hawawezi wakawa na uwezo huo,” anasema.

Anasema yeye na dada yake walikuwa wanawaza sana kuhusu kwenda India na gharama zake lakini ilivyodhihirika dada yake atapata tiba hapa nchini wakapumua.

“Nilichokuwa naogopa ni gharama… Sikuogopa uhai wangu hasa kwa kuzingatia kwamba dada yangu amesoma, ana elimu nzuri halafu mwisho wa siku anakuja kufa katika umri mdogo. Kwa kweli nilikuwa na vitu vingi sana vya kujiuliza kichwani mwangu.

“Kwa mtu mwingine atakayeniona barabarani sidhani kama anaweza kujua kwamba nimewahi kutoa figo… Ni suala la kumshukuru Mungu na Serikali yangu pia,” anasema Fredrick.

Hata hivyo, anasema katika suala hilo la figo na huduma nyingine za afya bado kuna changamoto nyingi ambazo zinatokea na bado zinahitaji kutafutiwa ufumbuzi zaidi ili kuwasaidia wananchi walio na uwezo wa chini kabisa.

“Kwanza kabisa ni gharama kwa upande wa kliniki ya usafishaji figo. Kama unavyojua mtu kabla ya kupandikiziwa figo lazima ahudhurie kliniki kwa ajili ya kuchuja na kutoa zile sumu zilizoko mwilini. Gharama zinakuja kwenye masuala ya kuchuja kwa sababu vifaa vinavyotumika vinahitaji kuwa katika uangalizi mkubwa na kila wakati na gharama za kiufundi iwapo vitaharibika,” anasema.

Anasema gharama za kusafisha figo ni kati ya shilingi laki moja na tisini elfu hadi laki mbili na kwamba kwa wiki mgonjwa anatakiwa kuchuja figo mara tatu.

“Sisi watanzania wanyonge tunaomba kwanza serikali yetu kuendelea kupunguza gharama za kliniki ya kuchuja kama ikiwezekana. Namuamini rais kama ameweza kufanya vitu vikubwa sana katika hii nchi, anao uwezo pia wa kupunguza hizi gharama. Watu wengi wanakufa kwa kushindwa kumudu gharama za matibabu,” anasema.

Anashauri pia huduma hiyo ya upandikizaji na uchujaji wa sumu ikasogezwa katika hospitali zote za kanda ili kuwezesha wanyonge kuzipata kwa urahisi tofauti na hivi sasa wanalazimika kutumia fedha kwa ajili ya nauli na kujikimu ugenini.

Takwimu kutoka wiazara ya afya zinaonesha kuwa wagonjwa 316 wamepandikizwa figo katika hospitali mbalimbali nchini, hususani Muhimbili na Hospitali ya Benjamin Mkapa hadi kufikia Novemba mwaka jana wakiwemo 78 waliohudumiwa na madaktari wazawa nchini.

Dk Gwajima anasema Tanzania inakadiriwa kuwa na wagonjwa wa figo kati ya 4,800 na 5,200 wanaohitaji huduma ya kusafisha damu au kupandikizwa figo. Anasema kati ya hao, wagonjwa 1,000 wanapata huduma mbalimbali kwa sasa.

Anasema jumla ya wagonjwa 78 wamepandikizwa figo na madaktari wazawa ambapo katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili walipandikizwa 62 na Hospitali ya Benjamini Mkapa wagonjwa 16 na waliosalia walitibiwa nchini India.

Anabainisha kuwa mpango wa wizara ni kuhakikisha inaziwezesha hospitali zote 26 za rufaa za mikoa kuweza kutoa huduma za matibabu ya figo ikiwemo usafishaji damu ifikapo mwaka 2025.

Anasema lengo la Serikali ni kuwapunguzia zaidi gharama za matibabu wagonjwa kwa kuwasogezea huduma hizo kwenye mikoa yao kuliko kuendelea kugharamia nauli na fedha za kujikimu wakiwa ugenini wanapofuata matibabu.

“Tumeongeza huduma za kibingwa katika hospitali zetu ambapo kwa sasa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, hospitali zote za rufaa za kanda na hospitali ya rufaa ya mkoa wa Tanga ya Bombo zinatoa huduma ya usafishaji damu kama tulivyoshuhudia katika Hospitali ya Kanda ya hapa Mbeya.”

“Wagonjwa wa figo ni kati ya wagonjwa walio katika hatari kubwa ya maambukizi ya magonjwa ya mfumo wa hewa kama vile kifua kikuu na bakteria hivyo ni muhimu kuendelea kuielimisha jamii kujikinga na madhara ya magonjwa ya kuambukiza,” anasisitiza.

Anasema wanaume ndio waathirika wakubwa wa ugonjwa wa figo ikilinganishwa na wanawake, hali anayosema inachangiwa kwa kiasi kikubwa na mfumo uliojengeka kwa kundi hilo kutopendelea kupima afya zao mara kwa mara na baadaye wanajitokeza tatizo likiwa limekuwa.

Mratibu wa huduma za figo kutoka Wizara ya Afya, Dk Linda Ezekieli, anasema ni muhumu sana jamii kuzingatia ushauri wa wataalamu juu ya kujikinga na ugonjwa huo ikiwemo lishe bora, kufanya mazoezi sambamba na kuzingatia uwiano wa uzito na kimo cha mwili ili kuepuka uzito uliopitiliza.

Anawasihi pia wanaume kubadilika na kupenda kupima afya zao na kwamba ni muhimu pia kujua dalili za matatizo ya kiafya kabla ya kufikia hatua ya tiba.

Magonjwa ya figo yanaweza kuwa na dalili kadhaa zikiwemo kuvimba mwili kunakoanzia usoni, kupungua au kukosa mkojo kabisa, kukojoa mkojo wenye damu au rangi ya kahawia, kuwa na shinikizo la damu, kuchoka mwili na kupungukiwa na damu.

Dalili hizi hujitokeza baada ya figo kupata athari kubwa, hivyo inawezekana kabisa mtu kuwa na tatizo la figo bila kuwa na dalili.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa kanda ya Mbeya, Dk Godlove Mbwaji anasema hospitali hiyo imekuwa ikipokea wagonjwa mbalimbali kutoka mikoa inayoihudumiwa na kwamba wale wanaohitaji huduma ya matibabu katika ngazi za juu imekuwa ikitoa rufaa huku pia ikiendelea kuwafuatilia.

Chanzo: www.habarileo.co.tz