Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uongozi wa kiwanda wakaidi maagizo

14471 Pic+kiwanda TanzaniaWeb

Wed, 29 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Afya za wakazi wa eneo la External Makuburi wilayani Ubungo zipo hatarini kutokana na majitaka yanayotiririka kwenye makazi yao kutoka kiwandani.

Majitaka hayo yanatoka kiwanda cha nguo cha Tanzania Tooku Garments Company Ltd kilichomo ndani ya eneo la Mamlaka ya Uwekezaji (EPZA), kupitia nyufa zilizopo ukutani na kuingia kwenye mto unaopita makazi ya watu.

Uongozi wa kiwanda hicho haukupatikana kuzungumzia malalamiko hayo licha ya mwandishi wa habari hizi kufika kiwandani mara nne. Walinzi walimweleza kuwa uongozi haupo tayari kuonana na waandishi wa habari.

Mkurugenzi mtendaji wa EPZA, Joseph Simbakalia alipotafutwa kuzungumzia suala hilo alisema mamlaka hiyo ni mpangishaji tu wa kiwanda hicho, hivyo suala la mazingira waulizwe Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Nemc). Hata hivyo, Nemc ilisema ilishachunguza suala hilo baada ya kupata malalamiko ya wananchi na maagizo iliyoyatoa yalitekelezwa.

Malalamiko ya wananchi

Mkazi wa External Makuburi, Pascal Ilanga alisema uchafuzi wa mazingira ulianza mwaka 2014 na walifikisha malalamiko kwa mamlaka kadhaa za Serikali.

“Majitaka hutiririka na kuingia kwenye mkondo wa maji ya asili uliokuwapo tangu zamani. Shughuli zinazofanywa kiwandani husababisha harufu mbaya inayokera puani na kifuani kiasi cha kutovumilika,” alisema Ilanga.

Uchunguzi wa Nemc

Taarifa ya uchunguzi ya Nemc ya Aprili 11, 2016 ambayo Mwananchi limeiona inaonyesha licha ya uzalishaji kusimama wakati ikishughulikia malalamiko ya wananchi, kulikuwa na uchafuzi wa mazingira.

“Wakati wa ukaguzi shughuli za uzalishaji zilikuwa zimesimama, maji machafu ya mvua yalikuwa yakitiririka kuelekea eneo la makazi. Pia, kulikuwa na harufu mbaya isiyovumilika,” inasema barua ya Nemc iliyosainiwa na Alfred Msokwa kwa niaba ya mkurugenzi mkuu.

Nemc ilitoa wiki tatu kwa kiwanda hicho kufanya marekebisho ambayo mratibu wa mazingira wa Nemc, Jaffar Chimgege akizungumza na Mwananchi hivi karibuni alisema yalifanyika.

Kilichofanywa na manispaa

Kuhusu malalamiko ya wananchi, Manispaa ya Ubungo imesema ilituma wataalamu wakiwa na uongozi wa EPZA kufanya uchunguzi Septemba 7, 2017.

Katika barua ambayo Mwananchi limeiona, manispaa inasema majitaka yanayoingia kwenye makazi ya watu yana kemikali za sumu. Katika barua hiyo ya Septemba 13, 2017 ilitoa siku 21 kwa kiwanda kufanya marekebisho.

“Hakuna mifumo madhubuti ya kudhibiti hewa chafu katika sehemu ya kiwanda inayotokana na matumizi ya kupulizia kemikali ya potassium permanganate isiende kwa jamii,” inasema barua hiyo iliyosainiwa na aliyekuwa mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo, Kawa Kafuru.

“Kuna feni maalumu (extracting fans) zimewekwa kwa ajili ya kuondosha hewa chafu na nyuzi laini za pamba kutoka chumba cha PP spray na zimeelekezwa upande jamii iliko na kuna hewa chafu yenye harufu mbaya isiyovumilika,” inasema barua hiyo.

Naye kaimu mkurugenzi mtendaji wa Manispaa ya Ubungo, Merick Luvinga akizungumzia suala hilo alisema kiwanda kilipewa notisi kuanzia Septemba 11, 2017 hadi Oktoba 6, 2017 na baadaye walifungua kesi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Sokoine Drive (Mahakama ya Jiji).

“Kiwanda kilishtakiwa kwa makosa matatu; kwanza kutiririsha majitaka kwenye makazi ya watu; pili kupiga kelele na tatu kutoa moshi. Wakati kesi ikiendelea wakarekebisha makosa mawili ya kelele na moshi,” alisema.

Kuhusu majitaka, alisema kiwanda kilitengeneza mtambo wa kuyasafisha na wakaguzi wa manispaa waliukagua.

“Changamoto iliyopo wanawasha mtambo ule kwa nyakati chache, si muda wote. Wakiona mtu ametembelea ndiyo wanauwasha, akiondoka wanauzima. Wanasema una gharama kubwa kuuendesha,” alisema.

Luvinga alisema manispaa inapanga kufanya ziara kuona utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa kwa kiwanda hicho.

Chanzo: mwananchi.co.tz