Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Unywaji maziwa watumishi wa umma wazinduliwa

Bf0502ee94d4a6e5b72c00dc48795fe2 Unywaji maziwa watumishi wa umma wazinduliwa

Thu, 15 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Serikali imezindua mpango wa unywaji maziwa kwa watumishi wa umma ili kuhamasisha unywaji wa maziwa yanayozalishwa ndani ya nchi na kuongeza kipato cha wafugaji.

Akizindua mpango huo jijini Dodoma juzi, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki alisema utekelezwaji wa mpango huo utasaidia kutatua changamoto ya soko la maziwa na kuleta tija kwa wafugaji.

Alisema lita za maziwa zinazozalishwa na wafugaji nchini ni bilioni 3, lakini maziwa yanayochakatwa kwa mwaka ni milioni 74.3 na hivyo, kufanya maziwa mengi kupotea kwa kukosa soko la uhakika jambo ambalo si jema.

"Leo tunazindua awamu ya kwanza ya unywaji wa maziwa katika ofisi za serikali na kwa awamu hii ya kwanza, tumeanza na wizara kumi (10), lakini kutakuwa na awamu nyingine za uzinduzi zitakazohusisha wizara, taasisi na mashirika ya umma,” alisema Ndaki.

Alisema kuwa uzinduzi huo unakwenda sambamba na ugawaji wa majokofu ya kutunzia maziwa kwa wizara hizo huku akiwaomba viongozi katika wizara, watumishi na wananchi kwa jumla, kuunga mkono mpango huo.

Aliongeza kuwa unywaji wa maziwa katika ofisi za umma utainua kwa kiwango kikubwa soko la maziwa yanayozalishwa nchini na kuepuka unywaji wa maziwa kutoka nje ya nchi, na hivyo kukuza pato la wafugaji pia itachochea upatikanaji wa ajira.

Ndaki alisema litakuwa jambo la ajabu kuona Ofisi ya Serikali inaagiza maziwa yanayotengenezwa kutoka nje ya nchi, wakati Serikali imezindua mpango mahususi unaohamasisha unywaji wa maziwa yanayozalishwa nchini.

Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania, Dk George Msalya, alisema ana imani kuwa kama ofisi zote za Serikali zenye watumishi takribani laki tano, zitaunga mkono unywaji huo wa maziwa itakua fursa nzuri kukuza soko la maziwa ya ndani nchini.

Wizara zilizohusishwa katika uzinduzi wa awamu ya kwanza ya unywaji wa maziwa, kwa uratibu wa Bodi ya Maziwa, ni pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Viwanda na Biashara, Tamisemi, Wizara ya Mambo ya Ndani na Wizara ya Elimu.

Chanzo: www.habarileo.co.tz