Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Unicef kuwasaidia watoto waliofanyiwa ukatili wa kijinsia

17897 Pic+unicef TanzaniaWeb

Wed, 19 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbeya. Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani (Unicef) limeanza kuzisaidia halmashauri za wilaya, miji na majiji kutekeleza mpango wa kuwatunza watoto waliofanyiwa ukatili wa kijinsia na wanaokumbana na sheria kinzani kupitia familia za kuaminika.

Familia za kuaminika ni zile zilizojitolea kuwalea watoto hao  badala ya  vituo vya kulea watoto wanaoishi katika mazingira magumu au shule za kurekebisha tabia wakati mchakato mwingine wa  kisheria au matibabu ukiendelea.

Tayari Wilaya ya Mbeya inazo familia 16 zinazotoa huduma kwa watoto waliofanyiwa ukatili ambao walipaswa kupelekwa kwenye vituo hivyo au shule za kurekebisha tabia.

Akizungumza baada ya kutembelea baadhi ya familia, mtaalamu wa masuala ya ulinzi wa mtoto, Mbelwa Gabagambi alisema matunzo kwenye familia yanasaidia kurejesha upendo na kumuondoa mtoto kwenye msongo wa mawazo.

"Unicef tuliona mfumo huu wa ulinzi wa mtoto ni mzuri kwa hivyo tunasaidiana na Serikali kuutekeleza. Kwa wilaya zilizo jaribu umesaidia kuokoa watoto wengi," alisema.

 Ofisa Ustawi wa Jamii, Wilaya ya Mbeya, Liluan Kilongumtwa alisema watoto 22 wameshasaidiwa kupitia familia za kuaminika.

"Tulitangaza kwenye jamii na familia zilizoona zinaweza kuwasaidia watoto ziliomba. Tulipitia michakato yote ikiwamo mafunzo na hivi tunavyoongea, wapo watoto wanalelewa na familia hizi," alisema.

Alisema kikawaida mtoto hapaswi kuishi zaidi ya miezi sita kwenye familia ya kuaminika.

"Hizi familia zimekuwa msaada mkubwa kwa watoto wetu hasa waliokuwa wamefanyiwa ukatili wa kijinsia," alisema.

Chanzo: mwananchi.co.tz