Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Unafahamu Kundi lako la Damu na Umuhimu wake?

Blood Group Dating.png Unafahamu Kundi lako la Damu na Umuhimu wake?

Tue, 7 Jul 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Je unalifahamu kundi lako la damu? Ni moja ya maswali mengi sana ambayo wengi wetu tunajiuliza. Wengi wetu huenda mbele zaidi kutaka kuju, je, kwa kundi ulilonalo unaweza kumpa damu mwenye kundi gani. Basi leo tujaribu kudadavua maswali haya pamoja na mengine mengi

Katika sayansi ya makundi ya damu, kwanza tutaanza na mifumo ya ugunduzi wa makundi ya damu. Mpaka Julai 2019, tafiti zinaonesha kuna takribani mifumo 39 ya damu. Nikukumbushe tu kuna mfumo wa ugunduzi wa kundi la damu na kuna kundi la damu; hivi ni vitu viwili tofauti.

Mfumo wa ugunduzi wa makundi ya damu ni njia tofauti ambazo wanasayansi walibaini zinaweza kutumika kugundua kundi la damu la mtu. Kwa mfano kuna MNS, Rh, KELL, LEWIS na ABO. ABO ndiyo mfumo unaotumika sana. Ndiyo mfumo unaotupatia makundi ya damu kama vile A, B, AB na O.

Mfumo wa ABO umeonesha usahihi wa hali ya juu kutokana na namna unavyofanya kazi. Ni mfumo unaohusisha moja kwa moja urithi wa sifa za chembechembe nyekundu za damu kutoka kwa mzazi kwenda kwa mtoto.

Unapofika hospitali na kuonana nasi wataalamu wa maabara tunakuchukua sampuli (damu) kisha tunaichakata na dawa maalumu kuangalia una kundi gani. Kwakweli hapa kwenye kuchomana sindano huwa mnatusumbua sana lakini kipimo hiki hakichukui muda mrefu kupata majibu. Kama nilivyoeleza mwanzo, mfumo huu wa ABO (ambao ndio hutumika) unatupatia makundi ya damu aina nne A, B, AB na O. Baada ya hapa tunatumia mfumo mwingine wa Rh (Rhesus) kujua kama wewe ni A+ au A-

Hii + au – isikuchanganye sana, si ya UKIMWI au magonjwa mengine ya zinaa. Kuna mzee mmoja niliwahi kumwambia ana kundi O+ kidogo azimie. Hii chanya au hasi kama inavyojieleza tu kwa tafsiri yake ni kutokuwepo (hasi) au kuwepo (chanya) kwa kitu tunaita ‘rhesus factor’.

Ikiwa ipo utaambiwa chanya na kama haipo utaambiwa hasi. Katika Makala zijazo, nitaangazia kuelezea zaidi na kwa kina, isipokuwa kwa leo niwaelekeze kwa undani zaidi kundi A, B, AB na O ambapo ukiongeza na mfumo wa Rh tunapata makundi A+, A-, B+, B-, AB+, AB-, 0+ na O-

Kuambiwa una kundi A, B, AB au O inatokana na uwepo wa aina ya seli katika uso wa chembechembe zako nyekundu za damu. Ikiwa una kundi A, maana yake una seli A, kama B maana yake una seli B hivyo hivyo kwa makundi mengine. Ndiyo maana A huwezi kumpa mwenye B na B hivyo hivyo.

Kundi A-: Ni kundi la damu ambalo mtu huyu anakuwa na aina ya seli A kwenye chembechembe zake nyekundu za damu.

Kundi A+: Ukibainika una kundi hili basi ujue kuna watu aina 4 wanaoweza kukupatia damu. A+, A-, O+ na O- na unaweza kutoa kwa A+ na AB+.

Najua unajiuliza kwamba mbona nimesema kundi A anampa wa kundi A lakini hapa nimeongelea kundi AB?

AB ana seli zote A na B hivyo yeye kuchangia mwenye A haiwezekani kwani atampa na B ambayo itakuwa hatari kwake lakini kupokea kutoka kwa A inawezekana maana AB ana A ndani yake.

Kundi A: Unaweza kupokea damu kutoka kwa A- na O- kwasababu ukiwa hasi inamaanisha huna rhesus factor hivyo mwenye Chanya (yeye anakuwa na rhesus factor) akikuamishia damu inakuletea matatizo. A- anaweza kumpatia mwenye A-, A+, AB- na AB+.

Umejiuliza tena inakuaje anampa mwenye Chanya? iko hivi mwenye hasi ina maana hana rhesus factor hivyo damu yake haiwezi kuteta shida kwa mwenye rhesus factor.

Kundi B: Mwenye kundi B ina maana ana aina ya seli B kwenye chembechembe nyekundi za damu.

B+: unapokea kutoka kwa B+, B-, O- na O+ na unaweza kutoa kwa B+ na AB+ pekee.

B-: unaweza kupokea kutoka kwa B- na O- pekee na kutoa kwa B-, B+, AB+ na AB-.

Kundi AB: Hapa ina maana una seli zote A na B kwenye chembechembe nyekundu za damu.

AB+: Huyu kwa lugha ya kitaalamu tunamuita universal receipient, maana yake anapokea kutoka kwa makundi yote ya damu ila anampatia AB+ pekee.

AB-: unaweza kupokea kutoka kwa AB-, A-, B- na O- na unaweza kutoa kwa AB+ na AB- pekee.

Kundi O: Mwenye kundi O maana yake ni 0 (zero) yani hana seli zozote kati ya A na B kwenye chembechembe nyekundu za damu yake.

O-: Kitaalamu tunamuita universal donor yani anaweza kumpatia mtu mwenye kundi lolote la damu. Hawa watu ni adimu sana. Kama wewe ni mmoja wapo, Tambua tu huku hospitali tunakuhitaji sana.

O+: Kundi hili ni wengi sana. Hapa ndio wengi tunakutana. Ni kundi lenye asilimia kubwa sana ya watu. Mtu huyu anaweza kupokea kutoka kwa O- na O+ na anaweza kutoa kwa A+, B+, AB+ na O+

Ukifuatilia vizuri nimeongelea zaidi seli A, B, AB na O, hizi si seli ikiwa unafikiria seli nyeupe au nyekundu, hizi kwa kitaalamu zinaitwa ‘antigen’.

Kuna faida nyingi za kulijua kundi lako la damu hata wakati wa ndoa au wakati wa ujauzito.

Twende kwenye swali letu la pili. Nini kinapelekea mimba kuharibika au kupata mtoto mmoja pekee wa kwanza ikiwa baba ana kundi la damu Chanya (+) yani A+, B+, AB+ au O+ na mama hasi (-) yani A-, B-, AB- au O-. Umewahi kujiuliza hili swali?

Kwanza kabisa, kila mtu ana kundi moja la damu kati ya haya makundi manane (A+, A-, B+,B-, AB+, AB-, O+ au O-), kundi ambalo mtoto hulipata baada ya mchanganyo wa vinasaba kutoka kwa wazazi wake. Kabla ya ujauzito, wengi tumekuwa hatufatilii makundi yetu ya damu pasipo kujua ni kitu muhimu sana kwa wote iwe mwanaume au mwanamke.

Kwa baba mtarajiwa na mama mtarajiwa, ikitokea mama ni Rh hasi (-) na baba Chanya (+) harafu huyu mama akapata mimba na mtoto akarithi Rh+ kutoka kwa baba kwa mimba ya kwanza hii huwa sio shida kwasababu damu ya mtoto haiingiliani na damu ya mama.

Shida huwa wakati wa kujifungua kwasababu kuna uwezekano wa damu ya mama kuingiliana na damu ya mtoto. Muingiliano huu ukitokea, mfumo wa damu wa mama kwakua hauna Rh (Rhesus) kwasababu tumesema mama ni hasi (-) basi hizi Rh kutoka kwa mtoto zitaonekana kama vitu vigeni ikimaanisha (foreign bodies).

Miili yetu ilivyoumbwa ikitokea kuna mgeni mpya ameingia kwenye mfumo wa damu hutambulika kama adui hivyo mwili hutengeneza kinga dhidi yake (antibodies) ili kupambana na mgeni huyo. Kwa mimba ya kwanza haina shida kwani mpaka damu zinaingiliana na mwili unatengeneza kinga dhidi ya Rh zilizotoka kwa mtoto tayari mama huyu anakuwa amejifungua. Kumbuka tu huyu mtoto wa kwanza hiyo Rh+ katoa kwa baba kwasababu mama ni Rh-.

Mimba ya pili ikiwa mtoto huyu hatarithi Rh kutoka kwa baba mambo yatakuwa shwari lakini kama akirithi Rh kutoka kwa baba huku tayari mwilini kwa mama tayari Rh zimetambulika kama adui basi ndipo shida huanzia kwasababu kinga za mama zitapenya kwenda kwa mtoto kupambana na adui na kwa sababu huyu adui (Rhesus) anakaa katika chembechembe nyekundu za damu (red blood cell) askari hawa watafanya uharibifu mkubwa wa chembechembe hizi kwa kuzivunja vunja na kusababisha ugonjwa ambao kwa kitaalamu huitwa hemolytic au Rh disease of the newborn.

Afya ya mama haitodhurika ila mtoto anaweza kupoteza maisha. Ndiyo sababu unashauriwa kuhudhuria kliniki au kumuona mtaalamu wa afya kwa ajili ya ushauri wa kitaalamu kwani inaweza kuepukika. Kuna sindano unaweza kuchomwa wiki ya 28 au masaa 72 kabla ya kujifungua.

Imeandikwa na;

Festo Donald Ngadaya

Mtaalamu wa Vipimo Maabara.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live