Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Umuhimu wa tohara kwa wanaume kujilinda na VVU

Bc27a3cc7eac0da1d78856036251ce74 Umuhimu wa tohara kwa wanaume kujilinda na VVU

Mon, 7 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

UELEWA mdogo sambamba na kukosa ujasiri wa kufanya maamuzi vinatajwa kuwa sehemu ya vikwazo vinavyokwamisha jitihada mbalimbali zinazofanywa na wadau wa afya nchini za kufikia malengo ya tohara kwa wanaume kuwa na mchango mkubwa kwenye mapambano dhidi ya maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi.

Tohara inatajwa kuwa sehemu ya mbinu zinazopaswa kupewa kipaumbele kwenye mapambano ya kudhibiti maambukizi ya VVU ikitajwa kuwa na uwezo wa asilimia 60 wa kuzuia maambukizi.

Serikali na wadau wamekuwa wakipambana kuhakikisha hili linafanyika ndani ya jamii.

Wanaume mbalimbali wanaojitokeza kufanyiwa tohara kwenye kampeni maalumu inayoendeshwa na Shirika la Watereed Tanzania inayokwenda sambamba na maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia inalenga kutoa huduma hiyo katika kata zote za wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya.

Lengo la kampeni hiyo ni kuwasogezea karibu wanaume elimu juu ya umuhimu wa tohara sambamba na kuwapa huduma kwa ukaribu badala ya kutembea umbali mrefu.

Wakizungumza na mwandishi wa makala haya, baadhi ya wanaume wakiwemo wenye umri mkubwa waliopata huduma ya tohara walisema awali hawakuwa na elimu lakini sasa wametambua umuhimu lakini wengine wakasema bado kuna woga ndani ya jamii.

Wapo pia wanaosema upo uoga uliojengeka ndani ya jamii unaosababishwa na mtu kuona aibu kwa kuonekana kuwa alichelewa kupata huduma hiyo. Na wengine wanahofia huenda wanaweza kupoteza mwelekeo wa ndoa zao walizodumu nazo kwa muda mrefu pale watakapoonekana wamechukua uamuzi wa kufanya tohara wakati awali hawakufanya hivyo.

Method Chaula mwenye umri wa miaka 58, mkazi katika kitongoji cha Magea katika mji mdogo wa Rujewa wilayani hapa anasema: “Nimejisikia kuja kufanyiwa tohara baada ya kuona inasaidia kwa kiasi kikubwa kuepusha watu na maambukizi ya magonjwa mengi ikiwemo VVU, kaswende na magonjwa mengine mengi.

“Baada ya kuona hivyo vitu sipendezwi navyo nimeamua kuja kufanya tohara mimi mwenyewe kwa ridhaa yangu. Nawashauri wenzangu ambao hawajafanyiwa tohara waje wafanye wasiendelee kufanya tendo la ndoa bila tohara.”

Chaula anaongeza: “Umri si tatizo mbona mie nimeamua kuja mimi mwenyewe pamoja na umri mkubwa nilio nao. Unaweza ukaona nina miaka 58 lakini nimeamua kuanzia leo hii kuwa msafi kwa kukubali kufanyiwa tohara. Kama bado nahitaji kufanya tendo la ndoa nimeona pia ni muhimu nikajiweka kwenye tendo hilo kwa usalama zaidi hata kama nilichelewa.”

Ibrahimu Mwandulifwa, mkazi wa kijiji cha Igawa wilayani Mbarali mwnye umri 38 na mume wa mke mmoja, anasema amefikia uamuzi wa kufanyiwa tohara baada ya kupata elimu na kutambua kuwa alikuwa akifanya tendo la ndoa katika mazingira yasiyo salama kwake kutokana na kutotahiriwa.

“Humo ndani kwa kweli nimepokelewa vizuri na nimepokea maelezo na maelekezo nikayaona yako sawa. Sintoishia hapa nitawashauri na wengine waje wapate huduma hii. Wapo rafiki zangu niliokuwa nao ambao mpaka sasa na wao hawajatahiriwa. Kuhusu suala la kupima nimemwambia nilipima mwezi wa tano wakanambia hilo nisiwe na tatizo nalo tena,” anasema.

Mtoa huduma ya tohara kupitia kampeni maalumu iliyoambatana na Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia, Anna Jackson, anasema kwa asilimia 60 maambukizi ya VVU yanapunguzwa kwa kufanya tohara kwa mwanaume.

“Tuko hapa kwa ajili ya kuelimisha jamii kupima VVU pamoja na kufanyiwa tohara. Walio tayari kufanyiwa tohara tunawafanyia hapa. Ni kuanzia walio na umri wa miaka 15 mpaka mzee kikongwe. Na tumeona watu wana mwitikio mkubwa na tunaendelea kuwafanyia hapahapa kwenye gari maalumu.”

“Uwepo wa ngozi ya mbele katika uume unachangia kwa kiasi kikubwa mtu kupata maambukizi kwa kuwa licha ya urahisi wake wa kuchubuka pia ni rahisi kutunza wadudu na uchafu tofauti na mwingine aliyetahiriwa,” anafafanua.

Dk Anna anasema toka walipoanza kampeni hiyo Novemba 23 mwaka huu mpaka Desemba mosi siku ya kilele cha maadhimisho ya siku ya ukimwi duniani, mwitikio wa watu kujitokeza kupima VVU na kufanyiwa tohara ulikuwa ni mkubwa. Anasema hadi siku hiyo zaidi ya watu 100 walikuwa wamefanyiwa tohara.

Anasema mwitikio haukuishia kwa vijana pekee, kwa kuwa mpango ulilenga kuwafikia kuanzia vijana wenye umri wa miaka 15 hadi wazee vikongwe.

“Wazee wenye umri wa miaka hamsini, sitini mpaka sabini wanakuja. Mwitikio wao ni mkubwa mpaka sasa tuna zaidi ya watu 100 ambao wameshafanyiwa na tunaendelea kama mlivyojionea wengine wako humo ndani wakipewa ushauri na wengine wanasubiri huduma. Katika huduma hii tulilenga wilaya yote ya Mbarali lakini tuna makundi mawili; moja lilianzia kata ya Madibira, sisi tulianzia kata ya Ilongo,” anasema.

Watereed Tanzania chini ya Shirika mama la HJFMRI ni miongoni mwa mashirika makubwa yanayofanya shughuli zake katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo mkoani Mbeya kuhusiana na Ukimwi.

Mkurugenzi wa Idara ya jamii, Hija Wazee, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Shirika hilo anasema wamekuwa wakishirikiana na serikali katika mapambano dhidi ya maambukizi mapya ya VVU katika nyanja mbalimbali ikiwemo Mpango wa Tohara.

“Nia ya Watereed Tanzania ni kusaidiana na Serikali. Tunafanya miradi mbalimbali ikiwemo wa kinga ambao uko kwenye idara yangu moja kwa moja. Tunatakiwa tupunguze maambukizi ya virusi vya ukimwi. Tunataka tufikie asilimia 95 tatu,” anasema.

Anafafanua kwamba 95 ya kwanza inahusu watu wote kupima kujua afya zao, 95 ya pili ni wale ambao wamepimwa na kukutwa wana maambukizi wanatakiwa waunganishwe kwenye huduma za tiba na wale waliokwishafika kwenye huduma za tiba, asilimia 95 miongoni mwao wawe wanajua ni jinsi gani virusi vyao vimefubazwa.

Chanzo: habarileo.co.tz