Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Umuhimu wa tiba asili kukabili magonjwa ya mlipuko

86076770c24da0327bee5bbdb197be3c Umuhimu wa tiba asili kukabili magonjwa ya mlipuko

Fri, 5 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

TIBA Asili imekuwepo tangu kuumbwa kwa mwanadamu na tangu hapo imekuwa ikiboreshwa katika kukabiliana na magonjwa mbalimbali yakiwemo ya mlipuko.

Historia ya tiba asili inaonesha kuwa, tangu kale, wahenga walitumia miti shamba na majani ya mti mbalimbali kwa ajili ya tiba ingawa walifanya hivyo bila kuwa na uhakika wa utafiti wa kisayansi bali msukumo wa kiimani na kiutamaduni.

Maeneo mengi nchini walichemsha magome ya miti na kuwapa watoto walipougua au watoto wachanga ili kuwakinga na maradhi mbalimbali.

Baadhi ya miti iliyotumika kwa tiba ni muarobaini uliotumiwa na wazee miaka ya zamani na hadi sasa baadhi wanatumia kama tiba ya malaria na magonjwa mengine mengi ingawa hakuna utafiti bayana unaodhihirisha hilo.

Akizungumza na HabariLEO hivi karibuni Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Dawa Asili Muhimbili (Muhas), Dk Joseph Otieno, anazungumzia mti wa muarobaini na kusema una mafuta tete, ila usalama wake haufahamiki duniani.

Dk Otieno anasema kwamba wataalamu wa afya duniani kote hawaridhii mti huo kutumika kama tiba asili kwa sababu una aina fulani ya alikaloidi yenye madhara kwenye miili ya binadamu.

Hata hivyo katika jamii ya Kitanzania, matumizi ya dawa za asili zisizozingatia utafiti au utaratibu wa tiba ulio rasmi zimeelezwa na wataalamu wa afya kuleta changamoto kubwa katika matibabu ingawa sasa Serikali kwa kushirikiana na wadau wa tiba hiyo, wameitambua kama tiba rasmi na hatua zimechukuliwa.

Magonjwa ya milipuko ni moja kati ya magonjwa yanayoangamiza jamii kwa haraka zaidi ikiwa hayatadhibitiwa kikamilifu. Hivi sasa nguvu ya tiba asili inaonekana na kutia moyo zaidi katika eneo la tiba hasa baada ya dunia kukumbwa na ugonjwa hatari wa Covid-19.

Ugonjwa huo uliibuka ghafla mwishoni mwa Desemba mwaka 2019, nchini China ukisababishwa na virusi vya corona na kuenea kote ulimwenguni.

Hapa nchini Serikali kwa kushirikiana na wadau wa afya imeweka nguvu kubwa kudhibiti ugonjwa huo wa mlipuko na imehamasisha na kutoa miongozo ya matumizi ya tiba asili jambo lililofanya Watanzania wengi kugeukia tiba hiyo inayoonesha matumaini ya kupambana na Covid-19.

Mkurugenzi wa Utafiti wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Dk Paul Kazyoba, anasema magonjwa mengi ya mlipuko yanasababishwa na virusi na husambaa kwa haraka na kwa muda mfupi tofauti na magonjwa ya mlipuko yanayosababishwa na bakteria.

Kutokana na ukweli huu, Dk Kazyoba anasema tiba asili inaweza kuwa njia sahihi katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko kwa sababu asilimia 98 ya mimea duniani haishambuliwi na virusi.

"Mimea inazalisha kemikali nyingi sana tofauti tofauti, kemikali hizi ni muhimu katika tiba asili, kwa hiyo tiba asili ni fursa kubwa katika kupambana na magonjwa ya mlipuko," anasema Dk Kazyoba.

Anasema Tanzania ina mimea mingi inayotumika kwa ajili ya tiba asili na kinachotakiwa ni kwa wataalamu wa tiba asili kuongeza bidii katika kuitambua.

"Tukiwekeza kwenye tiba asili na utafiti, tutaweza kupambana na magonjwa ya mlipuko, utafiti wa dawa siyo wa kukurupuka, unahitaji uwekezaji, naamini ndani ya miezi 24 ijayo, muonekano wa tiba asili utakuwa bora sana," anasisitiza Dk Kazyoba.

Katika kuonesha umuhimu wa utafiti, anasema NIMR wanafikiria kuendelea kuifanyia utafiti zaidi dawa yao ya NIMRCAF kwa sababu kwa NIMR utafiti ni hazina kubwa.

Anasisitiza kuwa Watanzania wanatakiwa kuthamini vitu vyao ikiwemo tiba asili kwa kuwa matatizo ni mwalimu kama ilivyokuwa wakati wa mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19 mwaka jana ambapo watu wengi waligeukia tiba asili.

"Pia wataalamu wa tiba asili waliosajiliwa na Baraza la Tiba Asili wanatakiwa kuzingatia utoaji wa huduma badala ya kufikiria kufanya biashara zaidi," anasema Dk Kazyoba.

Katibu Mkuu Tiba Asili, Bonaventura Mwalongo, anasema kuwa miti zaidi ya 12,000 imegunduliwa katika kukabiliana na magonjwa mbalimbali yakiwemo ya mlipuko.

Mwalongo anasema kwa mfano jijini Dar es Salaam mimea dawa zaidi ya 2,000 inatumika kwa matibabu mbalimbali.

“Mwaka 1979, mataifa yaliyoendelea yalikuja Afrika na kuchukua tani 28,000 za mimea dawa, lakini pia mwaka 1980, Japan ilikuja kuchukua tani 22,000 za mimea dawa, kwa hiyo tunaishukuru sana Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuweka msukumo mpya kwenye matumizi ya tiba asili, kinachotakiwa ni kwa taasisi za tiba asili kuunganisha nguvu,” anasema Mwalongo.

Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Profesa Yunus Mgaya, anasema kuna umuhimu mkubwa wa kuinua hadhi ya muonekano na kukubalika kwa tiba asili.

Profesa Mgaya anasema japo Watanzania wengi wameshaona umuhimu wa tiba asili, lakini kwenye eneo la namna zinavyofungashwa na kuhifadhiwa bado ni changamoto kubwa.

"Dawa isipofungashwa vizuri halafu ikutane na jua, joto na mambo mengine, thamani yake inapungua, pia dawa ambazo ziko kwenye kimiminika zinavutia vimelea hatari vya magonjwa kama vile fangasi, vifungashio vizuri vinaongeza ubora wa dawa," anasema Profesa Mgaya.

Anasema NIMR kupitia kituo chake cha utafiti cha Mabibo Dar es Salaam, itaanza kutengeneza dawa kwenye mfumo wa vidonge badala ya vimiminika.

Profesa Mgaya anasema dawa za tiba asili kwenye nchi za China, Korea na India ziko kwenye ubora wa juu na vifungashio vyake pia vina ubora wa juu.

Anasema asilimia 93 ya dawa zonazotumika hapa nchini zinaagizwa kutoka nje, hivyo tiba asili ikiimarishwa na kuboreshwa itasaidia kuokoa fedha nyingi ambazo zinatumika kuagiza dawa kutoka nje ya nchi

Chanzo: habarileo.co.tz