Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Umuhimu wa kupanua wigo huduma uzazi wa mpango

B52d6f0c25345fc798689c1d5cde7bd1.png Umuhimu wa kupanua wigo huduma uzazi wa mpango

Mon, 27 Dec 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Regina (si jina lake halisi), ni msichana aliyeletwa na shangazi yake Dar es Salaam akitokea Musoma ili kumsaidia kazi za ndani lakini kwa sasa analea mtoto baada ya kupata mimba ambayo hakuipanga.

“Nilitaka kumpeleka Veta (chuo cha ufundi). Wakati ninahangaika, nikaja kugundua kwamba Regina ana mimba. Nimegundua hilo anakaribia kujifungua kwa sababu alinificha. Sasa mume wangu amechachamaa, anataka tumrudishe nyumbani lakini nikiangalia hali ya kwao ninajua anakwenda kuteseka na mtoto,” anasema shangazi yake Regina.

Regina anasema alipoanza urafiki na mvulana aliyempa ujauzito ambaye hata hivyo amemkana, walikuwa wakitumia mpira wa kiume lakini kuna siku yule mvulana alikataa kutumia na siku hiyo anaamini ndiyo aliyopata mimba.

Msichana huyo mdogo ambaye anakiri kwamba hakudhamiria abadani kubeba ujauzito, anasema alikuwa na habari kuhusu huduma za uzazi wa mpango lakini mazingira yake yalimnyima nafasi ya kwenda kliniki kutafuta huduma hiyo.

Wapo wanawake wengi (pamoja na wanaume) ambao wanajikuta wakijamiiana na wenzi wao kutokana na matamanio ya mwili, lakini hawako tayari kuzaa. Hii si kwa wale walio nje ya ndoa pekee kama Regina bali hata walioko kwenye ndoa.

Inaelezwa kwamba wanawake wengi (si wote), kuanzia mijini hadi vijijini wangehitaji kupata huduma za uzazi wa mpango lakini

tatizo limekuwa ni urahisi wa upatikanaji wake.

Dk Cuthbert Maendaenda, Mkurugenzi wa Asasi ya Kiraia ya Tanzania Men as Equal Partners in Development (TMEPiD), anasema kimsingi, watu hujamiiana kwa sababu mbili; hitaji la ujinsi wao (recreation) na ya pili ni kupata uzazi.

“Kama ilivyo kwamba ni haki kila mtu kuchagua mwenza wake, ni haki pia ya kila mtu kuamua kuzaa au kutozaa na ni upi muda sahihi kwake kuzaa. Lakini haki hii itapatikana vizuri zaidi endapo huduma za uzazi wa mpango zitapanuka ili kila mtu azipate kwa urahisi na kwa njia endelevu,” anasema.

Akizungumza katika semina kwa waandishi wa habari juu ya umuhimu wa kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za uzazi wa mpango, Dk Maendaenda anasema tatizo lililopo kwa sasa ni njia za uzazi wa mpango, ukiondoa kondomu, kupatikana kliniki pekee na hivyo kuwawia watu wengine ugumu wa kuzipata kwa urahisi.

“Ndio maana tunahimiza sasa kama nchi tujielekeze kwenye mbinu jumuishi za masoko ya bidhaa za afya uzazi ili kuwa suluhisho la kuongeza ufanisi katika huduma za uzazi wa mpango Tanzania,” anasema Dk Maendaenda katika semina hiyo iliyoandaliwa na

TIMEPiD na kudhaminiwa na Shrika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA).

Mbinu jumuishi za soko ni zipi?

Dk Maendaenda anasema katika soko la bidhaa za afya, mbinu jumuishi za masoko (Total Market Approach TMA) ni mfumo unaoweza kutumika kwa kuweka mikakati ya kuongeza upatikanaji wa bidhaa muhimu za afya kwa namna endelevu.

Anasema matumizi ya mbinu jumuishi za masoko pamoja na tathmini za ufanisi wake hapa nchini zimefanyika tangu mwaka 2010 kupitia miradi ya wadau na kwamba changamoto iko kwenye utekelezaji na uenezaji wa mfumo huu katika ngazi za mikoa na halmashauri.

Anasema wakati huduma za umma zitolewazo bure na zinazofidiwa haziwezi kuondolewa, namna nyingine za kugharamia huduma zinapaswa kutumika ili kuwezesha watu wote wanaohitaji huduma za uzazi wa mpango kuzipata kwa urahisi kila wanapozihitaji.

“Miaka ya nyuma, hata kondomu kama njia ya kupanga uzazi, zilikuwa zinapatikana kliniki pekee, lakini kwa sasa zinapatikana kwenye maduka ya dawa. Tunataka hata huduma nyingine za uzazi wa mpango zipatikane kwenye maduka kama ya dawa mtu akienda

na kasha anaonesha kwamba huwa ninatumia dawa kama hii, anapewa.

“Kitakachotakiwa ni wahudumu wa maduka kupata elimu ya hizi huduma za uzazi wa mpango na kama ipo inayohitaji utaalamu kama vipandikizi, mhusika ananunua kwenye duka la dawa, anaelekezwa kwa wataalamu,” anasema Dk Maendaenda.

Ni kwa msingi huo, anasema ni wakati mwafaka sasa kuhusisha sekta ya kibiashara katika upatikanaji wa huduma za uzazi wa mpango kwani “ni mbinu iliyothibitishwa kuongeza matumizi yake katika makundi ya jamii yenye viwango tofauti vya kiuchumi.”

Anasema kuruhusu sekta ya biashara kuhudumia jamii wanaoweza kumudu gharama zake, huboresha upatikanaji wa huduma na kunufaisha serikali na wadau wa maendeleo kupitia mchango wa rasilimali za sekta hiyo.

Sayana Press

Dk Maendaenda anasema kwa sasa kuna sindano inayoweza kumkinga mwanamke kupata ujauzito kwa kipindi cha miezi mitatu na ambayo anajichoma mwenyewe kwenye paja inayoitwa Sayana Press.

Anasema nchi 11 Afrika ikiwemo Rwanda na Malawi zimeruhusu matumizi ya sindano hii kwa maana ya kupatikana kila mahala na

inasaidia kupunguza mimba zisizotarajiwa ambazo kwa takwimu zilizopo ni zaidi ya asilimia 30 ya mimba zote zinazotungwa nchini kwa mwaka.

“Hii Sayana Press ni sawa na Depo-Provera, tofauti ni kwamba Depo inachomwa kwenye makalio au bega na mtaalamu, lakini hii ni dozi kamili ambayo mtu anajichoma chini ya ngozi kwenye paja au chini ya tumbo,” anasema.

Kwa nini uzazi wa mpango?

Akizungumza kwenye semina hiyo ya waandishi wa habari, Meneja wa Utetezi wa Shirika la Tanzania Communication and Development Centre (TCDC), James Mlali anasema huduma ya uzazi wa mpango zina umuhimu katika kuboresha afya ya mama, mtoto na kuleta maendeleo kwa familia na jamii kwa ujumla.

“Tafiti za ulimwengu mzima zinaonesha kwamba matumizi ya uzazi wa mpango yakifanyika vyema vifo vya akina mama vinavyotokana na uzazi hupungua kwa asilimia 44 na vifo vya watoto kwa asilimia 35,” anasema.

Anasema watu wengi wanapokuwa hawazingatii uzazi wa mpango, kunasababisha uwepo wa wategemezi wengi kwa maana ya idadi ya watoto kuanzia mwaka 0-24 na kisha wazee na hivyo kuathiri maendeleo na kila siku.

Kwa hali ya sasa, anasema kila mtafuta mkate wa kila siku, ana wastani wa wategemezi tisa!

Anasema nchi ya Malaysia, kwa mfano ilikuwa karibu sawa na Tanzania kwenye pato la taifa miaka ya 1960 ikiwa na pato la taifa la Dola za Marekani 299 huku Tanzania ikiwa Dola 319.

Lakini mwaka 2010 pato la Malaysia lilikuwa limefikia Dola 8,754 wakati la Tanzania likiwa dola 514.

Anasema takwimu zinaonesha kwamba miaka ya 1960 wastani wa kuzaa kwa kila mwanamke (fertility Rate) ilikuwa watoto sita kwa Malaysia na Tanzania watoto saba, lakini mwaka 2010 takwimu zilionesha kwamba Malaysia walikuwa na wastani wa kila mwanamke kuzaa watoto wawili huku Tanzania ikiwa na watoto 5.4 (sawa na watoto sita).

Uzazi wa mpango una madhara kiafya?

Mlali anasema kumekuwa na maneno mengi mitaani yasiyo ya kweli kuhusu huduma za uzazi wa mpango za kisasa kuwa na madhara.

“Mimi na Dk Maendaenda sote tuna vitambi. Siku moja nilikwenda kwenye semina moja nikasikia wengine wanasema Oh! Hizi dawa zinaleta kitambi kwa mwanamke, sasa nikawauliza, mimi na Maendaenda (wanaume) tumetumia dawa gani?”

Anasema kama zilivyo dawa zingine zikiwemo chanjo, matumizi ya dawa za uzazi wa mpango zinaweza kumletea mtu matatizo madogo (side effects), na kwamba tatizo likiwa kubwa, mhusika anawaona wataalamu wanamaliza tatizo mara moja.

Anasema wakati kwa takwimu za mwaka jana watumiaji wa huduma za uzazi wa mpango nchini ni asilimia 41, nchi za wenzetu ni zaidi ya asilimia 80 na husikii habari za madhara.

Dini zinakataa uzazi wa mpango?

Mlali anasema kwa mujibu wa vitabu vilivyo na ‘fatwa’ zilizotolewa na mashehe kuhusu suala la uzazi wa mpango, hakuna dini inayozuia uzazi wa mpango, isipokuwa kuna dini zinataka matumizi ya njia za asili.

“Kwa upande wa dini ya Kiislamu kinachokatazwa ni kufunga uzazi kabisa na si kufanya uzazi wa mpango,” anasema.

Chanzo: www.habarileo.co.tz