Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ummy, wamiliki vituo binafsi vya afya meza moja sintofahamu NHIF

Watanzania Tujenge Utamaduni Wa Kupima Afya   Ummy.jpeg Ummy, wamiliki vituo binafsi vya afya meza moja sintofahamu NHIF

Sat, 30 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baada ya watoa huduma kutishia iwapo utekelezaji wa kitita kipya utaanza bila hoja zao kuangaliwa, huenda wakaacha kushirikiana na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu anatarajiwa kukutana nao Januari 4, 2024.

Taarifa iliyotolewa na Meneja Uhusiano wa NHIF, Anjela Mziray leo Jumamosi, Desemba 30, 2023 imeeleza kuwa Waziri atakutana na wawakilishi wa wamiliki wa vituo vya kutolea huduma tarehe tajwa jijini Dar es Salaam.

Kufautia hilo, Mwenyekiti wa Chama cha Watoa Huduma za Afya Binafsi (Aphta), Dk Egina Makwabe ameishukuru wizara kwa kuona umuhimu wa kukaa meza moja.

“Tumekuwa tukifanya kazi na uongozi wa Wizara, Mganga Mkuu kwa kipindi chote cha sintofahamu pamoja na NHIF, hii ni ishara nzuri kama tukishirikiana tunaweza kupata suluhisho la pamoja kama nchi.

“Ni kweli tulipanga kusitisha huduma Januari Mosi siyo utani. Tuliona vituo vingeshindwa kujiendesha na kufa, sisi tutakaa na Waziri na timu yake na NHIF na tutakubaliana bei na itakuwa na masilahi kwa pande zote, sote tunahudumia Watanzania,” amesema.

Sehemu ya taarifa ya NHIF imeeleza kuwa waziri huyo atakutana na wamiliki kutoka Aphta, Kamisheni ya Huduma za Jamii ya Kikristo (CSSC) na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata).

Imeleeza kuwa mfuko unaendelea kutoa elimu na kupokea maoni kuhusu kitita kipya cha mafao chenye huduma zilizoidhinishwa kutolewa kwa wanufaika wake kupitia vituo takribani 9,000 nchini ambavyo ni vya ngazi za zahanati hadi hospitali ya Taifa, vinavyomilikiwa na umma, binafsi na madhehebu ya dini.

Amesema maboresho ya kitita kipya cha huduma kwa wanufaika wa NHIF yanaongeza wigo wa upatikanaji wa huduma katika vituo vya ngazi mbalimbali, hivyo kurahisisha upatikanaji wa huduma za msingi na za kibingwa kwa ukaribu zaidi.

Aidha amesema maboresho hayo yamewianisha kitita na miongozo ya tiba iliyopo na bei za huduma kulingana na hali ya soko na hivyo kuondoa changamoto iliyokuwepo ya wanachama kukosa baadhi ya huduma, zilikosekana kwenye kitita cha awali.

Anjela amesema wakati hatua hiyo ikiendelea, mfuko unapenda kuwatoa hofu wanachama wake kuhusu tishio la usitishwaji wa huduma katika vituo vinavyomilikiwa na sekta binafsi, ambalo limeripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari.

“Majadiliano kuhusu kitita yanaendelea na taarifa rasmi ikiwa ni pamoja na tarehe ya kuana utekelezaji itatolewa baada ya kikao tajwa kufanyika,” amesema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live