Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ummy atoa maagizo chanjo homa ya manjano

Ummy Mwalimu Uviko.jpeg Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya

Wed, 9 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri wa Afya amewaagiza viongozi wa wizara yake kutoa chanjo ya manjano kwa watu wanaosafiri nje ya nchi katika hospitali zote za rufaa za mikoa ili kurahisisha upatikanaji wake.

Hatua hiyo imekuja baada ya Wizara ya Afya ya Kenya kutangaza mlipuko wa homa ya manjano Machi 3, 2022 ambapo wagonjwa 15 waliripotiwa katika kaunti ya Isiolo na kusababisha vifo vya watu watatu.

Waziri Ummy ametoa agizo hilo leo Jumatano Machi 9, 2022 wakati akizungumzia kuhusu ugonjwa huo ambao umegundulika nchini Kenya.

“Nataka kuelekeza hospitali zote za rufaa za mikoa chanjo hii iwe inapatikana kwasababu mtu anataka kusafiri kwenda nje ya nchi yuko Shinyanga, yuko Kigoma aanze kuhangaika achome hukohuko kwasababu lazima tuzingatie ule muda wa siku 10 kabla ya mtu kusafiri,”amesema.

Ummy amewaagiza wataalamu wanaongalia afya mipakani kuangalia uwezekano wa kutoa vyeti vya chanjo ya manjano kwa njia ya eletroniki ili kukabiliana na changamoto ya kugushi vyeti hivyo.

Pia amewataka watanzania kuchukua tahadhari kwa kuhakikisha ugonjwa huu hauingii nchini na kuhakikisha kuwa usafi wa mazingira yanakuwa safi ili kuepusha mbu wanaoeneza ugonjwa huo kuzaliana.

Amesema ugonjwa huo unazuilika kwa njia ya chanjo ambayo kutokana na ushauri wa Shirika la Afya Duniani (WHO) hutolewa kwa wasafiri hasa wanaokwenda katika nchi zile ambazo zimekuwa na ugonjwa huu ili kuwazuia wasafiri hao wasipate ugonjwa na kuingiza katika nchi zao pindi wanaporejea.

Kwa upande wa ugonjwa wa Polio ambao umegundulika nchini Malawi, Meneja Mpango wa Taifa wa Chanjo katika Wizara ya Afya, Dk Florian Tinuga amesema pamoja na hatua nyingine zinazochukuliwa na Serikali wataanza utoaji wa chanjo katika mikoa minne ambayo inapakana na nchi ya Malawi.

Ameiitaja mikoa hiyo ni pamoja na Songwe, Ruvuma, Njombe na kwamba utoaji chanjo huo utakaofanyika kwa watoto wa chini ya miaka mitano utaanza Machi 24 hadi 27 mwaka huu.

Amesema wakimaliza mikoa hiyo, awamu ya pili itahusiana na katika mikoa mingine yote nchini ambapo wataanza kuchoma watoto wote wa chini ya miaka mitano kati ya Aprili hadi Juni.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live