Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ummy: Wanawake nyonyesheni watoto

6ff23e4f8369242d0cc3498cba6a97be Ummy: Wanawake nyonyesheni watoto

Mon, 3 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu( pichani) amesema asilimia 97 ya watoto wenye umri wa chini ya miaka miwili wananyonya maziwa ya mama.

Hata hivyo alisema pamoja na mafanikio hayo jamii ina wajibu wa kuwawezesha wazazi, hususani wanawake waweze kunyonyesha watoto wao maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya mwanzo baada ya kujifungua.

Waziri Ummy amesema hayo wilayani hapa katika kuadhimisha Wiki ya Unyonyeshaji Duniani ambapo kwa mwaka huu kitaifa yamefanyika mwishoni mwa wiki wilayani Muheza mkoani Tanga.

Maadhimisho hayo mwaka huu yalikuwa na kauli mbiu ya ‘Tuwawezeshe wanawake kunyonyesha watoto kwa afya bora na ulinzi wa mazingira’.

Alisema idadi ya watoto wanaoanzishiwa kunyonyeshwa maziwa ya mama kwa wakati sahihi katika kipindi kisichozidi saa moja baada ya kuzaliwa ni asilimia 53 na idadi ya watoto wanaonyonyeshwa maziwa ya mama pekee bila kupewa maji, vinywaji na vyakula vingine katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo baada ya kuzaliwa ni asilimia 58.

Vilevile amefafanua kuwa idadi ya watoto wanaoanzishiwa vyakula vya nyongeza kwa wakati sahihi katika umri wa miezi 6 hadi 8 ni asilimia 87 na idadi ya watoto wenye umri wa miezi 6 hadi miezi 23 wanaolishwa chakula kinachokidhi vigezo vya ubora kilishe ni asilimia 35.

“Vigezo hivyo ni idadi sahihi ya milo anayopewa mtoto kwa siku kulingana na umri wake, mlo uwe na mchanganyiko wa vyakula kutoka kwenye makundi yasiyopungua manne ya vyakula,”alisema.

Alifafanua ulishaji usio sahihi kwa mtoto unaochangiwa na mama kuelemewa na majukumu mengi ya kazi, hivyo kukosa muda wa kutosha wa kumtunza mtoto ni sababu kubwa ya utapiamlo kwa watoto.

“Watoto wanapotimiza miezi sita waanzishiwe vyakula vya nyongeza vyenye ubora kilishe huku wakiendelea kunyonyeshwa hadi watakapotimiza umri wa miaka miwili,”alisema.

Akizungumzia kauli mbiu ya Wiki ya Unyonyeshaji Duniani mwaka huu, alisema inalenga kukumbusha jamii kutambua mchango wa unyonyeshaji katika utunzaji wa mazingira ya dunia na ikolojia yake na kulinda afya ya binadamu ambapo inahimiza jamii kuboresha kasi ya unyonyeshaji na kupunguza kiwango cha matumizi ya maziwa na vyakula mbadala vya watoto wadogo.

Chanzo: habarileo.co.tz