Dar es Salaam. Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amepiga marufuku hospitali za Serikali kutumia majibu ya vipimo vya nje katika matibabu ya wagonjwa.
Waziri Ummy amesema kuwa daktari wa hospitali ya serikali atatumia majibu ya vipimo vya nje pale itakapothibitika kuwa kipimo hicho hakipo kwenye hospitali husika.
Akizungumza leo Februari 24, 2020 alipotembelea Hospitali ya Rufaa ya Temeke, Ummy amesema kuna mchezo wa madaktari kuwataka wagonjwa kwenda kufanya vipimo nje ya hospitali.
Amesema kwa kiasi kikubwa vituo hivyo vinavyoelekezwa vinamilikiwa na madaktari hao na wanafanya hivyo kwa maslahi yao binafsi.
“Ukiangalia nje ya hospitali kumejaa vituo vya kufanyia vipimo, sasa nasema marufuku majibu hayo kutumika kwenye hospitali zetu labda mashine husika isiwepo,”
Ummy pia amewatahadharisha wataalam wanaoharibu kwa makusudi vipimo vya ndani ya hospitali ili wawaelekeze wagonjwa kwenye vituo vyao.
Pia Soma
- Kabendera atiwa hatiani kwa mashtaka mawili
- Jaji Kenya matatani akidaiwa kushirikiana na mtuhumiwa wa mauaji
- Serikali ya Tanzania yamuondolea Kabendera shtaka moja
Kwa upande wake mganga mfawidhi wa Hospitali ya Temeke, Meshack Shemwela amesema hospitali hiyo imejitosheleza kwa vipimo vyote na hivi karibuni watafunga mashine mpya nne za Ultra Sound.