Tanga.Waziri wa Afya Maendeleo ya jamii Jinsia wazee na watoto,Ummy Mwalimu amesema anakerwa na mtindo wa baadhi ya wanafunzi wa shule za Sekondari Jijini hapa kuhudhuria ngoma za vigodoro na wengine kuvuta
bangi badala ya kujikita kwenye masomo.
Amewataka kutumia muda wao katika masomo kwa kuwa ndiyo msingi wa maisha yao na mambo ya vigodoro pamoja na kuvuta bangi wawaachie ambao wako nje ya masomo.
Waziri Ummy ameyasema hayo leo Agosti 25 wakati akikabidhi madawati 45 yenye thamani ya Sh 5.7 milioni kwa shule ya Sekondari Toledo iliyopo kata ya Mwanzange Jijini Tanga.
“Inanitia simanzi sana kusikia mwanafunzi anakwenda kukesha kwenye vigodoro badala ya kujisomea..niwaambieni tu kwamba kwa mtindo huo alama za ziro kwenye mitihani ya kitaifa zitazidi kuongezeka huku wenzenu wa maeneo mengine wakifika mbali kwa sababu ya juhudi ya
masomo”amesema Ummy.
Amesema katika kuhakikisha ufaulu wa wanafunzi wa jijini Tanga unaongezeka ameanzisha tuzo maalumu itakayoshindaniwa na wanafunzi wa kidato cha pili watakaofaulu mitihani itakayotungwa kwa ajili ya
kuwapima viwango vyao.
Amesema tuzo hizo zitakazojulikana kwa jina la “Ummy Mwalimu Award” zitatolewa katika maeneo matatu ambayo ni kwa mwanafunzi atakayeongoza masomo yote katika mashindano hayo, ya pili itahusisha wasichana peke yao na ya tatu ni kwa walimu ambao watatoa mwanafunzi
atayaeongoza mitihani hiyo.