Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

‘Umaskini unachochea ukatili kwa kijinsia’

Df54f2e5c83a8b61d76dffac054179ab ‘Umaskini unachochea ukatili kwa kijinsia’

Tue, 6 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

UMASIKINI umetajwa kuwa ni miongoni mwa visababishi vya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia vikiwamo vitendo vya ubakaji, ndoa na mimba za mapema kwa watoto.

Nyingi miongoni mwa kesi hizo huishia kufutwa mahakamani huku watendaji wa vijiji na kata waliofanikisha kuibuliwa kwa kesi hizo wakinyooshewa vidole na kejeli kuiwa wanaingilia mambo yasiyowahusu.

Hayo yalibainika hivi karibuni wakati wa mkutano wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (Mtakuwwa) ulioandaliwa na shirika lisilokuwa la kiserikali la Women Wake Up (Wowap) na kushirikisha Kamati ya Ulinzi wa Wanawake na Watoto ngazi za kata na vijiji katika kata za Buigiri, Manchali, Chilonwa na Msanga.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Mwegamile, Nassoro Shaban, alisema jamii imekuwa ikiibua matukio, lakini mashauri hayo yamekuwa hayafiki mwisho mzuri kutokana na kukosekana kwa ushahidi wa kutosha.

Alisema mashauri hayo yanapofika kwenye ofisi za mtendaji kijiji au kata na watendaji wanapochukua hatua ya kufikisha kesi hizo mahakamani, wengine huchukuliwa kama ni watu wanaoingilia mambo yasiyowahusu jambo ambalo si kweli.

“Tunajitahidi tuwezavyo kuhakikisha haki inatendeka ikiwemo kwenda kutoa ushahidi mahakamani, unang’ang’ania mtu, lakini mwisho wa siku anaachiwa huru na mahakama,” alisema.

Alisema baadhi ya wazazi wamekuwa na tabia ya kumalizana wao kwa wao ili kupoteza ushahidi hasa pale tukio linapofanywa na ndugu wa karibu au jirani na kupewa fedha au mifugo ili kesi usiendelee na hii yote, inachangiwa na umaskini.

“Katika kijiji changu mwanafunzi alipata ujauzito, mama wa binti anauza pombe za kienyeji kwa hivyo, alikuwa hamfuatilii binti yake, kijana aliyempa mwanafunzi ujauzito akakamatwa kesi ikaenda mahakamani, ikasikilizwa, kijana akashinda kesi yuko mtaani, kijana mwenyewe tunakaa karibu pale vyumba vyetu vinatazamana, pata picha hapo tunatazamanaje ?” akahoji.

Ofisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Chamwino, Lucas Kaombwe, alisema Mtakuwwa ulianzishwa mwaka 2017 na unatakiwa kufanyiwa tathimini ifikapo 2022.

Alisema kila halmashauri ina mpango wa kutokomeza ukatili wa kijinsia. Kaombwe alisema Kamati ya Ulinzi wa Wanawake na Watoto katika ngazi ya Halmashauri itaratibu shughuli zinazohusu mpango na kuboresha utoaji wa huduma kwa makundi yaliyo katika mazingira hatarishi.

Alisema kazi kubwa za kamati ni kuratibu shughuli zinazohusu mpango wa kuboresha utoaji wa huduma kwa makundi yaliyo katika mazingira hatarishi. Ilibainika katika mkutano huo kuwa, vikwazo vingine katika vita dhidi ya ukatili huo wa kijinsia dhidi ya watoto hasa ubakaji na usababishi wa mimba kwa wanafunzi na watoto ni jamii kutojitokeza kutoa ushahidi na wasichana wanaopata ujauzito kusita kuwataja wahusika.

Mratibu wa Mafunzo kutoka Wowap, Nasra Suleiman, alisema lengo la mafunzo hayo ni kuziwezesha kamati na kuzijengea uwezo na maarifa katika ngazi ya kata na vijiji.

“Tunafanya kazi ya utetezi wa haki za mtoto, kimsingi kamati zinaundwa na serikali katika mpango wa kutekeleza ukatili kwa watoto kuhakikisha unaondoshwa,” alisema.

Chanzo: www.habarileo.co.tz