Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ukosefu wa elimu unavyochangia ongezeko la wagonjwa wa saratani

Dr Sarah Dkt.Sarah Maongezi, Mratibu wa Mpango huo

Wed, 30 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Vyombo vya habari vimetakiwa kuwa mstari wa mbele kutoa elimu ya kutambua na kuchukua tahadhari dhidi ya saratani ili kuisaidia jamii kuepuka madhara ya ugonjwa huo ikiwemo vifo.

Hatua hiyo ni baada ya mikoa ya Kanda ya Ziwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa wanaoripotiwa kuugua ugonjwa huo ambapo wengi wao hufika hospitali wakiwa katika hatua za mwisho.

Akizungumza kwenye semina ya siku moja kwa waandishi wa habari jijini Mwanza iliyoandaliwa na Taasisi ya Agha Khan kwa ufadhili wa shirika la Maendelwo la Ufaransa (AFD), Meneja Ubia, Uwezeshaji na Mawasiliano wa mradi mtambuka wa saratani (TCCP), Dk Sarah Maongezi amesema uelewa mdogo juu ya tatizo hilo ni moja ya sababu zinazochangia wagonjwa kufika kituoni tatizo likiwa hatua za mwisho.

Dk Sarah amesema kupitia mradi wa TCCP wamekuja na mkakati wa kutoa elimu kupitia vyombo vya habari, warsha za viongozi mbalimbali ili kukabiliana na tatizo hilo.

"Miongoni mwa changamoto kubwa ni pamoja na wagonjwa wengi kufika hospitalini wakiwa katika hatua za mwisho, hivyo katika kukabiliana na hii ipo haja ya jamii kupewa elimu ya kutambua viashiria vya ugonjwa huo," amesema Dk Sarah.

Changamoto nyingine ni kukosekana kwa taarifa sahihi kuhusu ugonjwa huo kwa jamii.Amesema kupitia mradi huo wanatarajia kuwafikia watu milioni 1.7 wakiwemo waandishi wa habari ambao watasaidia kutoa taarifa na elimu juu ya ugonjwa huo.

"Wagonjwa wengi wanafika hospitalini wakiwa kwenye hatua ya tatu na ya nne na sababu kubwa ni uelewa mdogo, hivyo waandishi wa habari kupitia kalamu zenu mnaweza kusaidia kuelimisha jamii,” amesema.Katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, Tanzania imeshuhudia ongezeko kubwa la wagonjwa wa saratani unaochangangiwa na mtindo wa maisha usiozingatia lishe bora na kutokufanya mazoezi.

Takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Tafiti za Saratani (IARC) za 2018, zinaonyesha kuwepo kwa wagonjwa wapya 42,060 kwa mwaka na takribani wagonjwa 28,610 sawa na asilimia 68 hufariki kutokana na ugonjwa huo nchini Tanzania.

Pia katika kila watu 100,000, watu 76 hugundulika kuwa na ugonjwa wa saratani.

Akizungumzia suala la Mashine za kupmia ugonjwa huo, Dk Sarah amesema, mashine hizo huuzwa ghali ambapo kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) mashine moja inatakiwa kuhudumia wagonjwa milioni 1 na kueleza kuwa nchini zipo mashine saba ambazo hazijitoshelezi.

Daktari Bingwa wa upasuaji Hospitali ya Rufaa ya Dk Athanas Ngambakubi amesema kwa mwaka 2020 inakadiriwa watu milioni 1.1 walipata saratani duniani.

Amesema watu 711,429 walifariki kwa saratani Afrika wakati huo Tanzania watu 40,464 walipata saratani kati yao 26,945 walifariki kutokana na saratani.

“Na kwa hapa Tanzania saratani inayoongoza ni ya mlango wa kizazi ikifuatiwa na matiti kwa upande wa wanawake na kwa wa wanaume ni tezi dume," amesema Dk Ngambakubi.

Awali akifungua mafunzo hayo, daktari bingwa wa magonjwa ya saratani hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando Dk Beda Likonda amesema ipo mihimili minne ambayo ikitendewa haki jamii itafikiwa na kuleta matokeo chanya ikiwemo takwimu, elimu, tiba na tiba shufaa.

"Pia serikali ihakikishe tiba zinapatikana kuanzia katika hatua mbalimbali za vituo vya tiba kama vile vituo vya afya, zahanati, hospitali za mikoa na wilaya ili huduma ziwafikie wananchi kwa wingi, " amesema Dk Likonda.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live