Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

‘Ukatili na ajali husababisha matatizo ya afya ya akili!

Af6869f4d11a18aba7e9ff738ab7bea7 ‘Ukatili na ajali husababisha matatizo ya afya ya akili!

Mon, 8 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

TAASISI ya Kuelimisha Umma kuhusu Magonjwa yasiyo ya Kuambukiza (TOANCD), imesema ajali za barabarani na ukatili wa kijinsia ni miongoni mwa mambo yanayochochea uwepo wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza yakiwamo yanayohusu afya ya akili.

TOANCD imesema waandishi wa habari, taasisi za elimu na jamii kwa jumla waunganishe nguvu na serikali kukabili mambo hayo ili kulinda afya na uhai wa Watanzania, kuepusha mateso na ulemavu kwa waathirika na kuokoa fedha zinazotumika kutibu waathirika wa magonjwa hayo yakiwamo majeraha na matatizo ya afya ya akili kutokana na msongo wa mawazo.

Mwenyekiti wa TOANCD, Leon Bahati na Makamu Mwenyekiti wa TOANCD, Exumper Kachenje, walisema hayo mwishoni mwa wiki baada ya mkutano wa taasisi hiyo uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Afya cha Muhimbili (Muhas), Dar es Salaam.

Wakirejea taarifa, hotuba na machapisho mbalimbali ya wataalamu wa afya, walisema foleni za magari, ajali za barabarani na ukatili wa kijinsia ni miongoni mwa mambo yanayochochea ongezeko la magonjwa yasiyo ya kuambukiza ukiwamo wa shinikizo la damu, matatizo ya afya ya akili na majeraha.

“Watalaamu wanasema wazi mambo haya yanahatarisha maisha na kuchochea umaskini katika familia kutokana na kutumia fedha nyingi za zikiwamo za serikali kwa matibabu na shughuli za mazishi,” alisema Bahati.

Kachenje yeye alisema ukatili wa kijinsia ukiwamo unaotokana na ugomvi katika familia husababisha matatizo yakiwamo majeraha, ulemavu na msongo wa mawazo kwa watoto, wanawake na wanaume wanaoathirika.

Kwa nyakati tofauti, viongozi hao wa TOANCD walisema wataalamu mbalimbali wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza wanataja sababu nyingine za magonjwa hayo kuwa ni ulaji usiozingatia lishe bora, ukosefu wa mazoezi ya mwili na matumizi ya vitu kama sigara na vilevi vikali kupindukia.

Katika mkutano huo, Ofisa Muuguzi Mwelimishaji kuhusu magonjwa yasiyo ya kuambukiza kutoka Chama cha Kisukari Tanzania (TDA), Elizabeth Licoco, alisema watu wanaofanya kazi za kukaa kwa muda mrefu, nao wanapaswa kuhakikisha kila baada ya dakika 45 hadi saa moja wanasimama na kutembea japo kwa dakika mbili ili kuepusha damu kuganda na kupata madhara katika mgongo.

Meneja wa Miradi wa Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyoambukiza (TANCD), Happy Nchimbi, aliwatambulisha kwa wanachama wa TOANCD, wataalamu wengine ambao ni wadau katika mapambano dhidi ya magonjwa hayo walioungana nao.

Waliotambulishwa ni Meneja wa Mpango wa Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza wa TDA, Dk Rachel Nunge na Meneja wa Mradi wa TDA, Dk Renatus Fabiano. Happy alisema: “Mwaka huu katika maadhimisho ya Wiki ya Magonjwa yasiyo ya Kuambukiza yatakayofanyika Arusha, TOANCD itatoa tuzo kwa vyombo vya habari na waandishi waliofanya vizuri katika kuripoti habari za magonjwa hayo hivyo wajitokeze kushiriki mashindano hayo na hata ya Afrika Mashariki

Chanzo: www.habarileo.co.tz