Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ujerumani kuipa Tanzania Sh20 bilioni kuboresha sekta ya afya

80497 Ujerumani+pic

Thu, 17 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania inatarajia kupokea Sh20 bilioni kama msaada kutoka Serikali ya Ujerumani kwa ajili ya kuboresha mifumo ya Teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) katika mfuko wa Taifa wa huduma za Afya.

Mkataba wa huo ulisainiwa jana Jumatano Oktoba 16,2019 katika ofisi za Wizara ya fedha jijini Dar es Salaam upande wa Serikali uliwakilishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dotto James na upande wa Ujerumani alikuwa ni Kaimu Balozi wa Ujerumani Jorg Herrera.

Katika hafla hiyo James aliishukuru Ujerumani na kusema msaada huo utafanikisha mpango wa Serikali wa kuwa na wanachama wengi wa huduma za bima, kuboresha namna ya kuwatambua na kuwasajili na kuboresha mifumo ya utendaji kwa ujumla.

“Serikali imedhamiria kutoa huduma za afya kwa wote na ili kufanikisha hili inakusudia kuwa na mpango mmoja wa huduma za afya (SNHIF) ambao utakuwa ni lazima kila Mtanzania kujiunga hivyo kutakuwa na uhitaji mkubwa wa uboreshaji wa Tehama,” alisema.

James alisema Serikali itaendelea kushirikiana na Ujerumani na wadau wengine muhimu ili kufikia maendeleo makuu na endelevu.

Kwa upande wake, Herrera alisema anaipongeza Serikali ya Tanzania kwa utayari wake katika miradi ya afya kwa umma hivyo Serikali ya Ujerumani inajivunia kuwa washirika wa maendeleo na nchi hii.

Pia Soma

Advertisement
“Wananchi wenye afya bora ni kiungo muhimu na msingi wa maendeleo endelevu ya nyanja zote hivyo uboreshaji wa sekta ya afya ni muhimu kwa mpango wa Serikali ya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025,” alisema Herrera.

Alisema kupitia uimarishaji wa Tehama na kuleta suluhisho la kidijitali katika huduma za bima ya afya kutaongeza ufanisi na uimara wa mifumo ya fedha katika vituo vya afya hivyo manufaa makubwa ni wagonjwa.

“Kuhifadhi nyaraka na takwimu za muhimu za mfuko wa kitaifa wa bima ya afya kwa mfumo wa kidijitali utawezesha upatikanaji wa takwimu sahihi na thabiti,” alisema Herrea.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz