Hai. Wananchi wa Tambarare wilayani Hai mkoani Kilimanjaro wataondokana na kero ya huduma za afya baada ya Mkuu wa wilaya hiyo, Lengai Ole Sabaya kuzindua ujenzi wa kituo cha afya kijiji cha Longoi.
Kituo hicho kinachojengwa kwa nguvu za wananchi, wadau kutoka vyama vya ushirika na Halmashauri ya Wilaya ya Hai kitatoa huduma kwa wananchi zaidi ya 19,000 wa kata tatu.
Akizindua ujenzi huo jana Desemba 13, 2019 Sabaya amesema fedha za ujenzi wa kituo hicho cha afya zimechangwa na vyama vya ushirika, kwamba wananchi watakaonufaika ni wa kata ya Masama Rundugai, Weruweru na Mnadani.
"Fedha za ujenzi wa kituo hiki zimetokana na asilimia 50 ya mapato ya vyama vya msingi vya wilaya hiyo katika mwaka wa fedha 2018/19, fedha hizo zilileta msuguano lakini tunashukuru zimepatikana na kazi imeanza," amesema Sabaya.
Amesema tayari zaidi ya Sh338 milioni zimepatikana, kwamba zinatosha katika ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje, mama na mtoto na maabara.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Hai, Dk Irene Haule amesema upungufu wa vituo vya afya katika wilaya hiyo ni asilimia 65.