Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ugonjwa wa ajabu ulivyomfanya akatwe miguu

17918 Pic+ugonjwa TanzaniaWeb

Wed, 19 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Wahenga walisema hujafa hujaumbika, pia wakasema ulemavu si ugonjwa. Hayo yote yamesadifu kwa Said Mtonga (50).

Japo ilikuwa ngumu kwake kukubaliana na ushauri wa kukatwa miguu yake uliotolewa na madaktari, lakini alijikuta hana namna nyingine anayoweza kuepuka maumivu aliyokuwa akiyapata zaidi ya kukubali ushauri huo wa madaktari.

Mtonga ambaye ni mkazi wa Kimara, Dar es Salaam, baba wa watoto wawili na fundi viatu hususani vya kike na kushona vilivyoharibika, anakiri kuwa kabla ya kufanyiwa upasuaji na kukatwa miguu, maisha yake yalikuwa magumu kutokana na kujiuguza bila mafanikio.

Anasema kabla ya kupata matatizo hayo hakuwahi kuwa na dalili zozote za kuumwa miguu, kutoka vipele, kuwashwa wala kuhisi kuwaka moto kama ambavyo huwatokea watu wengine kwa kuanza na dalili hizo na kwamba alikuwa akifanya kazi zake kama kawaida.

Tatizo lilivyoanza

Anasema ilipofika mwaka 2013 sehemu ndogo ya mguu wake wa kushoto ilijaa maji mithili ya mtu aliyeungua na maji ya moto jambo ambalo lilimlazimu kutumbua sehemu hiyo na kutoa ngozi ya juu ili aweze kuweka dawa.

“Nilipobandua ngozi katika eneo lile na kuweka dawa maji yakawa yanatoka, sikushtuka badala yake nikawa nasafisha na kuweka dawa kila mara, lakini kadri siku zilivyokwenda maji yalizidi kutoka, ndipo nikaamua kwenda katika Zahanati ya Kimara kupata matibabu,” anasema Mtonga.

Anasema kwa muda mrefu alikuwa akihudhuria katika zahanati hiyo na kusafisha kidonda huku akiendelea na shughuli zake za kushona viatu ili aweze kupata fedha za kumudu gharama za maisha na matibabu kwa ujumla.

“Lakini hali ilipokuwa mbaya mwaka huu nilipewa barua ya kwenda Hospitali ya Rufaa Mwananyamala ili nipate matibabu na vipimo kwa kina. Hata hivyo, baada ya kuhudumiwa kwa mwezi mmoja nilipewa barua kwa ajili ya kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

“Wakati naendelea kupatiwa matibabu ya kusafisha kidonda Muhimbili, kidonda kile kilibadilika rangi na kuwa Cheupe, kikaanza kutoa wadudu na harufu,” anasema.

Anasema wauguzi hospitalini hapo walimshauri aende Taasisi ya Saratani ya Ocean Road akafanyiwe uchunguzi wakihisi huenda ana tatizo la saratani.

“Nilipofika Ocean Road walinitoa kinyama na kuniambia nirudi baada ya wiki tatu kwa ajili ya kuchukua majibu. Hata hivyo, majibu yalipotoka niliambiwa sina saratani, ikabidi nirudi Muhimbili na wakati huo mguu ulikuwa umeanza kutoa wadudu,” anasema.

Anasema aliporudi na kufika mapokezi MNH alielekezwa moja kwa moja kwenda Wodi ya Kibasila. Jioni ya siku hiyo Daktari Bingwa alipopita kuangalia hali za wagonjwa alimwambia kuwa mguu wake umepoteza uwezo wa kufanya kazi, hivyo ni lazima utolewe ili awe katika hali ya kawaida.

“Kutokana na fikra zangu zilivyokuwa mbali nilikataa kukatwa mguu, nikaondoka na kurudi nyumbani. Wiki haikwisha mguu wa kushoto nao ulibadilika na kuwa mweusi, umekakamaa na kuweka alama za kuchanika. Nikasikia maumivu makali hadi nikashindwa kutembea hata kwa magongo,” anasema Mtonga.

Anasema kutoka Kimara kurudi Muhimbili ilikuwa ni kazi ngumu, hata wahudumu wa Kituo cha Mabasi Yaendeayo Haraka maarufu ‘Mwendokasi’ walishindwa kumsafirisha kwa kutumia magari yao jambo ambalo lilimlazimu dada anaekatisha tiketi katika kituo cha Kimara kumuombea msaada kwa abiria wengine.

“Baada ya kuniombea msaada niliweza kupata nauli na kuchukua bajaji, hadi kufika hospitalini mwili ulikuwa hauna nguvu, sina damu. Mfamasia aliyekuwa katika Wodi ya Kibasila alimsisitiza daktari kuwa mguu ukatwe kwa sababu unatoa harufu kali na wadudu.

“Nilirudi hospitalini kwa sababu sikuwa na namna ya kufanya, awali nilifikiri nitapona na kurejea katika hali yangu ya kawaida, lakini si kufikia hatua ya kukatwa miguu.

“Kichwani mwangu nilikuwa na wasiwasi nitapata wapi fedha za kulipia baada ya matibabu maana nilipokuwa nikiona jinsi watu wanavyotozwa fedha nilikosa imani, nani wa kunisaidia,” anasema Mtonga kwa simanzi.

Kwa mara ya mwisho alirudi hospitalini hapo Mei 5, mwaka huu, huku upasuaji wa kukata mguu wa kwanza ukifanyika Mei 19, kabla ya upasuaji wa kukata mguu wa pili kufuata Juni 20.

“Baada ya kukatwa mguu wa kwanza hali ilionekana kuwa mbaya katika mguu wa pili. Ulikuwa na maumivu makali jambo ambalo lililazimu nao ukatwe,” anasema Mtonga.

Ofisa Ustawi wa Jamii kutoka Muhimbili, John Mwakyusa, anasema wakati mgonjwa huyo anapewa matibabu hakuna ndugu yake wa karibu aliyefika hospitalini hapo kwa ajili ya kumhudumia ingawa dada yake alipatikana katika simu, lakini alisema ana hali ngumu kiuchumi.

“Hata watoto wake mmoja aliyoko mkoani Morogoro na mwingine hapa Dar es Salaam walipotafutwa hawakuweza kuonyesha ushirikiano wowote, hivyo ofisi ya ustawi wa jamii ndiyo ilikuwa msaada pekee katika kumsaidia huduma ndogondogo.

“Hali yake haikuwa hivi, wakati akipokelewa alikuwa amedhoofu tukamtafutia maziwa akawa anatumia hadi tulipoona hali imeimarika ndipo tulipoanza kutafuta namna ya kumrudisha nyumbani ikizingatiwa awali alikuwa na miguu miwili,” anasema Mwakyusa.

Familia yake

Mtonga anasema yeye na mke wake walitengana miaka mingi iliyopita kabla hata hajaanza kusumbuliwa na ugonjwa wa miguu na aliondoka na watoto wake wote wawili.

“Awali nilikuwa nikiishi hapa jijini Dar es Salaam, lakini baada ya mama yangu kuugua ilinilazimu nirudi Chalinze ili kumsaidia baadhi ya mambo jambo ambalo mke wangu aligoma kwa madai kuwa hawezi kuishi kijijini, hivyo tukaachana,” anasema Mtonga.

Anasema jamii inayomzunguuka ndiyo msaada wa karibu kwake kutokana na kumpatia chakula, baadhi ya jamaa kumtembelea hospitalini huku mke wa rafiki yake akisema ndiye aliyemsindikiza kituo cha Mwendokasi alipokuwa akienda hospitali.

Asamehewa, apewa msaada

Uongozi wa Muhimbili uliamua kumsamehe fedha aliyokuwa akidaiwa kiasi cha Sh935,000 huku pia wakimpatia msaada wa baiskeli ya magurudumu matatu yenye thamani ya Sh500,000 pamoja na mtaji wa Sh80,000 kwa ajili ya kujiendeleza kimaisha.

“Baiskeli hii itakuwa kama usafiri kwangu na itanipa urahisi wa kwenda kununua vifaa vya kushonea viatu vinapohitajika,” anasema Said.

Mkuu wa Idara ya Ustawi wa Jamii katika Hospitali ya Muhimbili, Emmanuel Mwasota anasema baada ya Mtonga kuruhusiwa kurudi nyumbani walifanya tathmini ili kuweza kujua kama mazingira ya mgonjwa huyo ni salama na ataweza kumudu maisha mapya, lakini waligundua kuwa unahitajika msaada.

“Ilitulazimu kutafuta wafadhili ambao wanaweza kutusaidia ili kupata kitu kitakacho mwezesha kutembea na kufanya shughuli nyingine,” anasema.

Lakini jitihada hizo zilishindikana na baadaye wakafikia mwafaka wa kuomba msaada kwa Mkurugenzi wa MNH ili aweze kuwapatia fedha zitakazotosha kumsaidia.

“Alitupatia Sh500,000 ambayo tulipeleka Sido tukatengenezewa hii baiskeli ya magurudumu matatu na kumpatia mtaji wa Sh80,000 kwa ajili ya kurudisha biashara ya ushonaji aliyokuwa akijishughulisha nayo awali,” anasema.

Mwasota anabainisha kuwa wimbi la utelekezwaji wagonjwa katika hospitali hiyo ni kubwa na wengi wao wanatokea Dar es Salaam.

Mkurugenzi atoa neno

Mbali na Mtonga kusamehewa gharama za matibabu alizokuwa akidaiwa, Mkurugenzi wa MNH, Profesa Lawrence Maseru anasema kila mwezi hulazimika kutoa msamaha wa kati ya Sh450 milioni hadi Sh600 milioni wa matibabu kwa wagonjwa wasioweza kumudu gharama za matibabu na wengine kutelekezwa na ndugu zao.

Mbali na kutoa msamaha huo wengine hulazimika kupatiwa vifaa vya kufanyia kazi na mitaji ili waweze kuendesha shughuli zao za maisha.

Profesa Maseru anasema msamaha huo wa gharama za matibabu unatokana na hali za kiuchumi kwa baaadhi ya watu wanaouguza ndugu zao hospitalini hapo kuwa mbaya jambo ambalo linawalazimu kuwatelekeza katika kipindi chote wanachopatiwa matibabu.

Aomba msaada

Licha ya kuwa katika hali aliyonayo sasa Mtonga anaahidi kujishughulisha kwa bidii ili aweze kujiingizia kipato kitakachotosha kumudu gharama za mahitaji yake endapo Watanzania watamsaidia kuboresha kibanda chake cha biashara alichokuwa akikitumia.

Kama unahitaji kumsaidia Said Mtonga unaweza kuwasiliana naye kupitia namba ya simu 0652 978 463.

Chanzo: mwananchi.co.tz