Baada ya Wizara ya Afya kuutahadharisha umma juu ya uwepo wa ugonjwa wa macho mekundu (Red Eyes), maambukizi ya maradhi hayo yamezidi kuripotiwa sehemu mbalimbali nchini, huku Mamlaka zikizidi kutoa elimu ya namna ya kujikinga na waathiriwa kulalamikia shughuli zao za kiuchumi kukwama.
Mratibu wa huduma za Macho Mkoa wa Dodoma, Elizabeth Kiula amesema kuna visa 52 vya Ugonjwa huo kutoka Wilaya mbili za Chamwino na Dodoma Mjini na wengi wamepatiwa matibabu huku hali zao zikiendelea vyema na baadhi ya Waathiriwa wamedai wanashindwa kuendelea na utafutaji hivyo kukumbwa na hali ngumu ya kimaisha.
Amesema, “Wagonjwa watano walitibiwa hapa na mapaka sasa katika Mkoa wa Dodoma tumeshawaona wagonjwa kutoka Wilaya ya chamwino na Dodoma Mjini, sasa tukijumlisha wagonjwa 39 waliotoka hospitali ya Mkoa na 13 kutoka chamwino, tunapata jumla ya wagonjwa 52.”
Hata hivyo, mlipuko huo umeanza kubadili ratiba katika baadhi ya hospitali kama njia mojawapo ya kukabiliana na hali hiyo ambapo Datkari Bingwa wa Magonjwa ya Macho Hospitalini hapo Dkt. Sarah Ludovick, alisema idara ya macho imeanzisha mafunzo kwa wagonjwa juu ya njia sahihi ya kujikinga na ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa Taarifa kutoka Wizara ya Afya zinasema, Mkoa wa Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, na Dodoma ndiyo iliyothibitika kuwa na wagonjwa wa Red Eyes ambapo kwa Dar es Salaama pekee ilikumbwa na visa 869.