Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ufisadi bil 27/- kung’oa vigogo hospitali za rufaa

37e6c5d0dc1a74c5f8d6b4b125bad14f Ufisadi bil 27/- kung’oa vigogo hospitali za rufaa

Tue, 2 Mar 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

KAMATI iliyoundwa na Serikali kuchunguza hospitali 28 za rufaa za mikoa, imebaini kuwepo viashiria vya hujuma, wizi na udokozi wa dawa na vifaa tiba, vyote vikiwa na thamani ya Sh bilioni 26.7.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima amemuagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Mabula Mchembe afanye mabadiliko ya viongozi katika hospitali zote 28 kulingana na nafasi ya kila kiongozi alivyoshiriki kusababisha hasara hiyo.

Dk Gwajima alitoa agizo hilo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari, kuhusu matokeo ya ripoti ya ufuatiliaji wa changamoto za ukosefu wa dawa na vipimo katika hospitali hizo.

“Nimekuwa nikipokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuhusu kukosa huduma ya dawa na vipimo katika vituo vya kutolea huduma za afya ngazi zote, hali ambayo haiendani na matarajio ya Rais John Magufuli baada ya kuongeza bajeti ya dawa kutoka Sh bilioni 31 mwaka 2015/16 hadi Sh bilioni 270,” alisema.

Dk Gwajima alisema Februari Mosi mwaka huu wizara hiyo iliunda kamati ya watalaamu kutoka wizara na taasisi za sekta mbalimbali, kufuatilia katika hospitali hizo kwa kuanzia kwa kipindi cha miezi 18 kuanzia Julai 2019 hadi Desemba mwaka jana.

Alisema kamati hiyo, ilitaka kubaini changamoto za upatikanaji duni wa dawa na vipimo licha ya kuongezeka fedha za dawa. Alisema kwamba jumla ya dawa na vipimo 25 hadi 20, vilifuatiliwa kuanzia ununuzi, mapokezi na matumizi.

Dk Gwajima alisema maeneo yaliyofuatiliwa na kubainika kuwa na mapungufu kuwa ni bidhaa zilizopokelewa kwenye bohari ya hospitali husika na hazikuingizwa kwenye vitabu vya mali Sh milioni 62.7, ankara ambazo hazikuonekana kwenye hospitali za rufaa za mikoa Sh bilioni 1.1, na bidhaa zilizokosa ushahidi kutoka bohari ya hospitali kwenda idara husika ya kutolea huduma Sh bilioni 3.2.

Alitaja maeneo mengine kwa ni bidhaa zilizotolewa hospitali kwenda vituo vingine kama msaada na hazikufika huko Sh milioni 354.7, bidhaa zilizokosa ushahidi wa kufika kwa wateja Sh bilioni 2.4, bidhaa zilizonunuliwa kwa washitiri bila ushahidi wa Bohari ya Dawa (MSD) Sh bilioni 5.6, na bidhaa zilizonunuliwa nje ya MSD na washitiri teule Sh bilioni 1.12.

Dk Gwajima alitaja maeneo mengine kuwa ni bidhaa zilizonunuliwa kwa washitiri kinyume na mkataba Sh milioni 640.2, bidhaa zilizonunuliwa bila kuidhinishwa na Kamati ya Dawa na Tiba Sh bilioni 1.9 na hasara ya fedha itokanayo na kukosekana kwa dawa kwa wateja wa bima na kuelekezwa kupata dawa nje ya hospitali Sh bilioni 6.1.

Alitaja maeneo mengine kuwa ni bidhaa kumalizika muda wake wa matumizi huku vituo vingine vikiwa na uhitaji Sh milioni 714.9, bidhaa kununuliwa kwa kutumia masurufu bila kufuata utaratibu Sh milioni 124.5, na hospitali kutolipwa fedha kwa kuhudumia wateja wa mifuko mingine Sh milioni 321.

Maeneo mengine yaliyobainishwa ni hospitali 26 kati ya 28, kutumia asilimia ndogo ya fedha kununua bidhaa za afya hususani dawa na vitendanishi kwa asilimia 35, badala ya asilimia 50 iliyopendekezwa na mwongozo wa wizara.

Dk Gwajima pia alieleza eneo lingine ni hospitali nyingi kukosa takwimu za wanaotibiwa kwa msamaha; na hospitali saba zilizokutwa na takwimu zikionesha kuwa msamaha ni asilimia tisa hadi 12, tofauti na maelezo kuwa ni asilimia 60 hadi 70.

“Kwa mujibu wa matokeo haya ni dhahiri kuwa huu ni usimamizi dhaifu wa mifumo ya udhibiti wa mali ya umma, dalili za hujuma, wizi na uwajibikaji usiofaa wa baadhi ya viongozi katika ngazi zote za uongozi hadi kwa mtumishi mmoja mmoja,” alisema.

Alimuagiza Profesa Mchembe afanye mabadiliko ya viongozi katika hospitali hizo, kulingana na nafasi za ushiriki wao katika hasara hiyo kuanzia Mganga Mfawidhi wa hospitali husika hadi kila kiongozi wa timu ya uendeshaji wa hospitali husika.

Alimtaka Profesa Mchembe achukue hatua za kinidhamu dhidi ya kila mtumishi au mtu yeyote aliyeenda kinyume na sheria, kanuni na taratibu za ununuzi na ugavi wa bidhaa za afya ; na aunde kamati kwa kushirikiana na ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kupitia mikataba ya washitiri wa bidhaa za afya nchi nzima.

Pia, alimtaka Profesa Mchembe aratibu maboresho na miongozo ya ushirikiano na Tamisemi na makatibu tawala wa mikoa kwenye kuimarisha ufuatiliaji na uangalizi wa uendeshaji wa hospitali hizo.

Aidha, alimpa siku 14 Profesa Mchembe kuanzia jana awe amempatia taarifa inayojibu masuala yote yaliyoibuliwa katika ripoti hiyo.

Hivi karibuni, akiwa kwenye ziara katika mikoa ya Geita na Shinyanga, Rais Magufuli alishtushwa na kuguswa na tatizo la upungufu wa dawa hospitalini, kwa kuwa kila msafara wake ulikopita alipokea malalamiko ya uwepo wa tatizo hilo.

Alitoa siku saba kwa Dk Gwajima na Waziri wa Tamisemi ,Selemani Jafo wahakikishe wanaweka usawa katika ugawaji dawa, kwa kuwa licha ya kwamba bajeti ya dawa imeongezeka, kumekuwa na malalamiko ya kuwepo kwa upungufu hospitalini.

"Inawezekana kuna upunjaji wa mgawo wa madawa katika maeneo ya mkoa huu wa Geita ikiwemo Masumbwe, bajeti ya madawa imeongezeka lakini dawa zinazotolewa katika mkoa huu ni chache, Waziri wa Afya na Waziri Tamisemi mnaopanga bajeti ya madawa mkakae ndani ya siku 7 mje na majibu ni kwa namna gani madawa yataongezeka katika hospitali ya Masumbwe na maeneo mengine", aliagiza.

Chanzo: habarileo.co.tz