Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uchunguzi wa afya huepusha maradhi

DSC 2593 Uchunguzi wa afya huepusha maradhi

Wed, 30 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

JANA ilikuwa maadhimisho ya Siku ya Moyo Duniani. Lengo la maadhimisho hayo ni kutoa elimu pia kwa wananchi jinsi ya kuepuka na kupunguza vitu vinavyoweza kusababisha mtu akapatwa na magonjwa ya moyo kwa njia ya mtindo wa maisha.

Wataalamu wa afya wanasema, magonjwa ya moyo kwa kiwango kikubwa yanaweza kuepukwa iwapo tu wananchi watafuata kanuni bora za ulaji, mtindo wa maisha na kujenga tabia ya kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara ambao utabaini viashiria vya tatizo mapema na kuchukua hatua ya kuzuia.

Katika maadhimisho hayo ambayo kila mwaka hufanywa Septemba 29, ni wakati mzuri kwa wananchi kuchukua hatua ya kujitafakari angalau kujenga utaratibu wa kuchunguza afya mara moja kwa mwaka.

Kufanya hivyo kutasaidia kujua mwenendo wa mfumo wa mwili wako na pia kutaonesha iwapo kuna viashiria vyovyote vya kupata maradhi sio lazima yawe ya moyo bali hata maradhi mengine ambayo kama yangegundulika mapema yangetibiwa mapema kabla tatizo halijawa kubwa.

Nakumbuka somo la Ofisa Lishe wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Husna Faraji alilotoa mwaka jana kwenye maadhimisho kama haya, alisema mtindo wa maisha usiofaa una uhisiano mkubwa na maradhi ya moyo.

Husna anashauri wananchi kwanza kabisa kupata elimu ya lishe, kisha wachukue hatua ya kufanya uchunguzi wa afya angalau mara moja kwa mwaka na pia wajenge tabia ya kujitokeza kufanya uchunguzi kupitia kambi mbalimbali zinazoendeshwa na taasisi hiyo au serikali kama sehemu ya kusaidia jamii.

Katika kujali Husna anashauri kama mtaalamu wa lishe, kuwa ni vyema wananchi wakajenga tabia ya kutumia maziwa yaliyopunguzwa au kuondolewa mafuta, kupunguza ulaji wa nyama nyekundu, hususan zenye mafuta.

Aidha, anasisitiza ulaji zaidi wa nyama ya kuku au samaki na kuepuka kula vyakula vilivyokaangwa au vyenye mafuta kama soseji, nyama ya kusaga, keki, maandazi, vitumbua na viazi vya kukaanga.

Sasa basi, pamoja na kuwa siku hiyo imeisha jana, lakini suala la kuchunguza afya ni endelevu, tujenge tabia hiyo na pia ni vyema kufuata ushauri wa wataalamu wa afya kama ambavyo Daktari Bingwa wa magonjwa ya moyo wa JKCI, Samweli Rweyemamu alivyoshauri jana asubuhi wakati akizungumza na vyombo vya habari kuhusu maadhimisho ya siku ya moyo na jinsi ya kuulinda moyo.

Viashiria kadhaa vinaelezwa kuwa visababishi vya maradhi ya moyo ni pamoja na kuwa na shinikizo la juu la damu, tatizo la uzito mkubwa hii na hiyo imetajwa mara kadhaa kuwa inaonesha watu hawana tabia ya kufanya mazoezi na kuzingatia lishe bora. Inashauriwa kuwa angalia kwa siku, mtu afanye mazoezi walau dakika 30.

Lakini mtindo wa maisha yetu, ulaji mbaya usiozingatia makundi yote ya vyakula umetajwa kama kisababishi kimoja cha kupatwa na maradhi hayo.

Chanzo: habarileo.co.tz