Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uchangiaji damu Tanzania bado wasuasua

77653 Dam+pic

Sat, 28 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Serikali  ya Tanzania imesema nchi hiyo haijafikia  lengo la ukusanyaji damu kwa mwaka kwa maelezo kuwa hivi sasa inayokusanywa ni asilimia 60 pekee kulingana na vigezo vilivyowekwa kimataifa.

Hayo yameelezwa leo Jumamosi Septemba 28, 2019 na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alipokuwa akiongoza uchangiaji damu wa hiari katika kongamano lililoandaliwa na kikundi cha maendeleo wa Kibosho Girls Vikoba.

Amesema mahitaji ya damu ni ya dharura wakiwemo waliopata ajali, wajawazito, wagonjwa wa selimundu na saratani.

“Kwa mwaka takribani wanawake milioni mbili wanajifungua nchini na kati yao asilimia 85 wanajifungua bila matatizo lakini asilimia 15 wanahitaji huduma ya damu, kuna wagonjwa wa seli mundu lakini saratani ndiyo zaidi nasi tunakusanya asilimia 60 pekee kwa mwaka hatujafikia lengo, natoa wito Watanzania jitokezeni,” amesema.

Amesema katika kuhakikisha kitengo cha Damu Salama wanakusanya damu ya kutosha, Serikali imefunga mashine za kisasa nane katika kanda mbalimbali nchini ili kupima na kuhifadhi damu kwa usahihi zaidi.

Kaimu mkuu wa kliniki ya tiba kutoka Taasisi ya saratani ya Ocean Road, Dk Caroline Swai amesema wagonjwa wanaotibiwa saratani wana mahitaji makubwa ya damu.

Pia Soma

Advertisement
“Asilimia 80 ya wagonjwa wanategemewa kuongezewa damu hivyo chupa 20-25 zinahitajika kwa siku, na malengo lazima tupate chupa 30 mgonjwa akiwa na upungufu wa damu lazima aongezewe bila hivyo tiba husimama mpaka damu itakapopatikana,” amesema Dk Swai.

Mwenyekiti wa maendeleo Kibosho Vikoba,  Hanifa Mponji amesema kufanyika kwa hafla hiyo ni kuelekea katika maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa shule ya Sekondari Kibosho Girls.

Chanzo: mwananchi.co.tz