Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

UTAFITI: Watoto kuanza kutumia ARV kupambana na VVU

81b34f3d5967b1ce7266b50175894ba8.jpeg UTAFITI: Watoto kuanza kutumia ARV kupambana na VVU

Mon, 6 Dec 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

DAWA za kufubaza virusi vya Ukimwi (ARVs) maalumu kwa watoto zinatarajiwa kuanza kutumika nchini baada ya kukamilika kwa miongozo ya matumizi yake.

Mtaalamu wa WHO nchini anayehusika na Ukimwi, kifua kikuu, magonjwa ya zinaa na homa ya ini, Dk Christine Musanhu alisema juzi kuwa, Tanzania imeridhia na kuzingatia miongozo ya Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) ambayo inapendekeze matumizi ya dawa za kufubaza VVU zinazoweza kutumika kwa urahisi na watoto.

Alisema hayo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani yaliyofanyika kitaifa mkoani Mbeya.

Alisema dawa hizo zina sifa kadhaa ikiwamo uwezo wa kufubaza haraka kiwango cha virusi mwilini na uwezekano mdogo zaidi wa VVU kujenga usugu dhidi ya dawa hizo. “Dawa hizi mpya ni rahisi kunywewa, zina ladha nzuri mtoto anapozinywa. Tunategemea watoto watapata furaha kuzitumia na zitatoa matokeo yanayotakiwa ambayo ni kufubaza VVU,” alisema Musanhu.

Alisema watoto na vijana wamekuwa wakiachwa nyuma hivyo hatua hiyo ya kuanzisha dawa maalumu ni uthibitisho wa kuwajali. Musanhu alisema kwa kushirikiana na wadau wengine, wamekuwa wakihimiza serikali kuridhia dawa hizo mpya. “Kwenye hili la dawa tunaendelea kutekeleza taratibu husika kwa ushirikiano na Wizara ya Afya na Taasisi ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA).

Taratibu hizi zitawezesha dawa kusajiliwa nchini, kukadiria mahitaji na pia kuwapa mafunzo wahudumu wa afya wanaozitoa kwa walengwa,” alisema na kuongeza: “Haya yanafanyika kwa ushirikiano na wadau wengine, lakini mwanzoni mwa mwaka ujao tutaweza kuagiza dawa zipatikane kwa watoto, kwa hiyo hii ndiyo njia ambayo tunajaribu kuhakikisha hakuna kundi linaloachwa nyuma.” Dk Musanhu alieleza majukumu ya WHO katika nchi mbalimbali ikiwamo Tanzania ni pamoja na na kufuatilia athari za dawa mpya zinazotengenezwa.

“Kama hakuna athari, hiyo ni furaha kwamba dawa ziko vizuri, kama zipo athari, tunapambana kuzikabili,” alisema. Alisema majukumu mengine ya shirika hilo ni kutoa mwongozo kwa maana ya kukabili virusi vya Ukimwi na magonjwa mengine yanayorandana yakiwamo ya zinaa, kifua kikuu na homa ya ini.

“Kwa hiyo tuna mwongozo katika ngazi ya dunia na pia tunahakikisha inatafsiriwa katika ngazi ya taifa ili itekelezwe na kupata matokeo mazuri katika nchi husika,” alisema. Alisema Tanzania inafanya vyema na iko katika njia sahihi katika kukabili ugonjwa wa Ukimwi katika maeneo yote matatu ya malengo ambayo WHO imeweka.

Malengo hayo ni kubaini watu wanaofahamu hali yao ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi, idadi ya watu wanaopata ARV na kubaini idadi ya watu ambao kiwango cha virusi kimepungua.

Chanzo: www.habarileo.co.tz