Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

UTAFITI: Juisi za miwa zakutwa na bakteria wanaopatikana kwenye haja kubwa

Miwapic Utafiti wa juisi ya miwa waibua hofu

Tue, 16 Nov 2021 Chanzo: mwananchidigital

Utafiti wa awali uliyofanywa na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Sayansi ya Afya (Cuhas) kwenye juisi ya miwa jijini Mwanza umebaini uwepo wa bakteria aina ya escherichia coli anayepatikana kwenye taka mwili za mfumo wa chakula wa binadamu.

Mtafiti wa vimelea vya magonjwa na magonjwa ya kuambukiza kutoka Cuhas, Profesa Jeremiah Seni alisema utafiti huo ulihusisha uchunguzi wa kimaabara katika sampuli 120 zilizochukuliwa kutoka kwa wauza juisi 24 jijini Mwanza na kati ya hizo sampuli 71 zilikutwa na bakteria huyo.

“Pamoja na bakteria aina ya escherichia coli, sampuli 116 sawa na asilimia 96.7 ya sampuli 120 zilizochunguzwa pia zilikutwa na bakteria za aina mbalimbali zinazoweza kusababisha madhara ya kiafya kwa binadamu,” alisema Profesa Seni ambaye pia ni daktari wa binadamu katika Hospitali ya Kanda ya Rufaa Bugando.

Alitaja baadhi ya madhara yanayoweza kusababishwa na bakteria aina ya escherichia coli kuwa ni maambukizi kwenye mfumo wa mkojo (UTI) na maradhi mengine iwapo bakteria hao wataingia kwenye mfumo wa damu.

Profesa Seni alisema Cuhas kwa kushirikiana na wadau wengine watatoa elimu kwa wajasiriamali wanaouza juisi ya miwa baada ya utafiti kubaini kupungua kwa kiwango cha bakteria katika juisi zilizotengenezwa na wajasiriamali waliopewa elimu kuanzia siku ya kwanza hadi siku ya tano ya kukamilisha utafiti.

“Uwepo wa bakteria ulionekana kupungua kutoka asilimia 87.5 kwenye sampuli 24 zilizopimwa siku ya kwanza hadi asilimia 45.8 siku ya tano na ya mwisho wa utafiti. Hii ni ishara kuwa kupitia elimu ya ubora na usalama tunaweza kumaliza tatizo hili,” alisema Profesa Seni.

Akizungumzia taarifa za bakteria wenye madhara kiafya kukutwa katika juisi ya miwa, Zakaria John, mmoja wa wajasiriamali wanaouza bidhaa hiyo eneo la Stendi ya Igombe jijini Mwanza, aliwataka wenzake kuzingatia kanuni ya usafi ikiwemo kunawa mikono, kuparua miwa, kuosha vyombo kwa maji ya moto na kuvihifadhi sehemu safi.

Mmoja wa wateja aliyekutwa akinywa juisi ya miwa eneo la Mkuyuni jijini Mwanza, Suleiman Nassoro aliwaomba watafiti kutafuta kiini cha uwepo wa bakteria hao ili kuwawezesha kuendelea kufaidi juisi hiyo anayoamini ina faida kiafya ikiwemo kusafisha mfumo wa mkojo.

Chanzo: mwananchidigital